Ligi
ya Mabingwa wa Mikoa (RCL) msimu wa 2013/2014 itakayochezwa kwa mkondo
mmoja inaanza kutimua vumbi Mei 10 mwaka huu katika vituo vitatu vya
timu tisa kila kimoja.
Timu
itakayoongoza katika kila kituo cha ligi hiyo itakayomalizika Juni 2
mwaka huu ndiyo itakayopata tiketi ya kucheza Ligi Daraja la Kwanza
(FDL) kwa msimu ujao wa 2014/2015. Vituo hivyo ni Mbeya, Morogoro na
Shinyanga.
Kituo
cha Morogoro ambapo mechi zitachezwa Uwanja wa Jamhuri kitakuwa na timu
za Abajalo FC ya Dar es Salaam, African Sports (Tanga), Bulyanhulu FC
(Shinyanga), Kariakoo SC (Lindi), Kiluvya United (Pwani), Mji Mkuu FC
(Dodoma) Mshikamano FC (Dar es Salaam), Navy FC (Dar es Salaam) na
Pachoto FC (Mtwara).
Uwanja
wa Sokoine ndiyo utakaotumika katika kituo cha Mbeya chenye timu za AFC
ya Arusha, Magereza FC (Iringa), Mpanda United SC (Katavi), Njombe Mji
FC (Njombe), Panone FC (Kilimanjaro), Tanzanite SC (Manyara), Town Small
Boys (Ruvuma), Ujenzi (Rukwa) na Volcano FC (Morogoro).
Timu
za Eleven Stars ya Kagera, Geita Veterans (Geita), JKT Rwamkoma FC
(Mara), Mbao FC (Mwanza), Milambo SC (Tabora), Mvuvumwa FC (Kigoma),
Simiyu United (Simiyu), Singida United (Singida) na Wenda FC (Mbeya)
zitacheza katika kituo cha Shinyanga kwenye Uwanja wa Kambarage.
Orodha
ya usajili wa wachezaji wa timu zote kwa ajili ya RCL imetumwa kwa
vyama vya mpira wa miguu vya mikoa na klabu zote za RCL, FDL na Ligi Kuu
ya Vodacom (VPL) kwa ajili ya kipindi cha pingamizi ambacho
kinamalizika Mei 4 mwaka huu.
Hata
hivyo, katika usajili uliowasilishwa na baadhi ya klabu imebainika kuwa
kuna wachezaji walioshiriki VPL, FDL na wale U20 za VPL waliocheza ligi
msimu wa 2013/2014.
Kiongozi
yeyote atakayebainika katika udanganyifu kwenye usajili huo, awe wa
klabu au chama cha mpira wa miguu cha mkoa atachukuliwa hatua kwa mujibu
wa kanuni ikiwemo kufikishwa katika vyombo vya kimaadili vya TFF kwa
hatua zaidi.
Ligi ya Mabingwa haina mdhamini, hivyo timu shiriki zitajitegemea kwa kila kitu, na zinakumbushwa kuwahi vituoni.
MALAWI KUWASILI MEI MOSI KUIVAA STARS
Timu
ya Taifa ya Malawi (Flames) inatarajiwa kuwasili nchini Mei 1 mwaka huu
kwa ajili ya mechi ya kirafiki dhidi ya Taifa Stars itakayochezwa Mei 4
mwaka huu kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya.
Flames
yenye msafara wa 31 utakaoongozwa na mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya
Chama cha Mpira wa Miguu cha Malawi (FAM) utaingia Mbeya kwa usafiri wa
barabara. Wachezaji katika msafara huo ni 20.

No comments:
Post a Comment