TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete ameliagiza
Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kuwajengea nyumba 403 mpya waathirika ambao
walibomolewa nyumba zao kutokana na mvua kubwa, yenye mawe na upepo mkali
iliyonyesha usiku wa Machi 3, 2015, katika vijiji vitatu vya Kata ya Mwakata,
Wilaya ya Kahama, Mkoa wa Shinyanga.
Aidha,
Rais Kikwete amesema kuwa Serikali itaendelea kuwatunza na kuwapatia huduma
zote za msingi watu walioathiriwa na maafa ya mvua hiyo hadi watakapokuwa na
uwezo wa kujitegemea wenyewe.
Rais
Kikwete pia amesema kuwa maafa ya mvua hiyo yasitumike kama kisingizio cha watu
kulipiza kisasi kwa madai kuwa mvua hiyo ilinyesha kutokana na msukumo wa kishirikina.
Rais
Kikwete ameyasema hayo, leo, Machi 12, 2015,wakati alipohutubia mkutano mkubwa
wa hadhara wa wananchi katika Kata ya Mwakata, Wilaya ya Kahama, Mkoa wa
Shinyanga, ambako anafanya ziara maalum ya siku mbili kutoa pole kwa wananchi
wa vijiji vitatu vya kata hiyo walioathirika na mvua iliyonyesha usiku wa Machi
3, 2015.
Rais
Kikwete amewaambia wananchi hao: “Nimekuja kuwapeni pole kutokana na maafa ya
mvua. Napenda kuwahakikishieni kuwa Serikali iko nanyi. Msiba wenu ni msiba
wetu, huzuni yenu ni huzuni yetu na machungu yenu ni machungu yetu.”
Rais
Kikwete amewaambia wananchi kuwa Serikali itaendelea kuzikarabati nyumba ambazo
ziko katika hali ya kukarabatiwa. “Zile za ukarabati tutaendelea kuzikarabati
na zile zilizoharibika kabisa tutazijenga. Naambiwa zinahitaji kiasi cha Sh. Bilioni
mbili, tutazitafuta na tutajenga kwa vyovyote vile. Naambiwa kuwa ni nyumba 403
mpya. Hakuna atayepewa fedha taslim, na wala mtu asije kuomba fedha, ili ajenge
mwenyewe. Na wala zamu hii hakuna tenda kwa sababu tutatumia Jeshi letu la
kujenga taifa – tayari nimewaambia waifanye hii kazi. Hii ni dharura na chombo
chetu cha dharura ni Jeshi letu.”
Rais
Kikwete pia amewashukuru wote ambao wamekuwa wanatoa misaada ya kusaidia
wahanga wa mvua hiyo, ikiwa ni pamoja na wale ambao wametoa makazi ya dharura
kwa waathirika na misaada mingine.
Rais
Kikwete pia amesema kuwa Serikali itaendelea kutoa misaada ya dharura kwa
waathirika hadi watakapokuwa na uwezo wa kujitegemea wenyewe: “Tayari
Serikali imetoa tani 20 za chakula, tumetoa mafuta na sukari. Tutaendelea
kuwaunga mkono mpaka mvuke. Aidha, hakuna yoyote ambaye atapoteza maisha kwa
sababu ya ukosefu wa chakula. Tayari kuna chakula cha kutosha mwezi mmoja mpaka
mwezi ujao na kikiisha tutaleta kingine.”
Rais
Kikwete ameongeza: “Tutakabiliana pia na magonjwa ya mlipuko. Tayari tuna kituo cha
dharura cha afya na kinatoa huduma mzuri.”
Rais
Kikwete ameamuru uongozi wa Mkoa wa Shinyanga kwa kushirikiana na Halmashauri
ya Wilaya ya Kahama kuhakikisha kuwa yananunuliwa magodoro ya haraka ili watoto
waweze kulala vizuri na kuepukana na magonjwa ya vichomi.
“Magodoro
yatapatikana kesho, yapo hapa Kahama na kama hakuna yafuatwe hata Shinyanga. Lakini
lazima yapatikane kesho (Ijumaa, Machi 13, 2015). Naambiwa mahitaji ya magodoro
ni 649, tayari 558 yamepatikana na bado yapo mahitaji ya magodoro 149 na haya
tutaleta kesho,”amesema Rais Kikwete.
Kuhusu
imani za ushirikina ambazo zinaanza kuandamana na tukio la mvua hiyo, Rais
Kikwete amesema: “Msijiingize katika mambo ya ushirikina na ramli. Mvua za mawe ni za
kawaida duniani hata kama hazijapata kunyesha hapa. Msitoke hapa kwenda
kutafuta waganga kuhusiana na mvua hii ili mpate sababu ya kuua watu.”
Ameongeza:
“Mvua
za namna hii ni matukio ya kawaida na maisha ya kawaida katika maeneo mengine.
Hakuna mchawi hapa, bali ni rehema za Mwenyezi Mungu. Nimesikia sikia mambo
haya. Hayana kichwa wala miguu. Hili ni tukio la kawaida.”
Amesisitiza
Rais Kikwete: “Napenda kuwahakikishia kuwa Serikali yenu ipo. Acheni kuamanika,
acheni kubabaika. Asiwababaishe mtu yoyote. Leo nimekuja mwenyewe mkubwa wa
Serikali. Watakuja wengi kuwadanyanga, hawana Serikali. Wakija waambieni hivi –
mwenye Serikali tuliyemchangua kaja, keshatuahidi, chakula tunakula, huduma za
awali tumezipata na hizo nyingine amesema atatutimizia. Ili kuja kuwapeni pole
mwambieni awapeni pole tu, asiwababaishe.”
Imetolewa
na;
Kurugenzi
ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu – Dar es Salaam.
12
Machi, 2015
No comments:
Post a Comment