Pages

Showing posts with label Kikwete. Show all posts
Showing posts with label Kikwete. Show all posts

Friday, March 13, 2015

JKT WAAGIZWA KUWAJENGEA NYUMBA WAATHIRIKA WA MVUA YA MAWE KAHAMA

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete ameliagiza Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kuwajengea nyumba 403 mpya waathirika ambao walibomolewa nyumba zao kutokana na mvua kubwa, yenye mawe na upepo mkali iliyonyesha usiku wa Machi 3, 2015, katika vijiji vitatu vya Kata ya Mwakata, Wilaya ya Kahama, Mkoa wa Shinyanga.
Aidha, Rais Kikwete amesema kuwa Serikali itaendelea kuwatunza na kuwapatia huduma zote za msingi watu walioathiriwa na maafa ya mvua hiyo hadi watakapokuwa na uwezo wa kujitegemea wenyewe.
Rais Kikwete pia amesema kuwa maafa ya mvua hiyo yasitumike kama kisingizio cha watu kulipiza kisasi kwa madai kuwa mvua hiyo ilinyesha kutokana na msukumo wa kishirikina.
Rais Kikwete ameyasema hayo, leo, Machi 12, 2015,wakati alipohutubia mkutano mkubwa wa hadhara wa wananchi katika Kata ya Mwakata, Wilaya ya Kahama, Mkoa wa Shinyanga, ambako anafanya ziara maalum ya siku mbili kutoa pole kwa wananchi wa vijiji vitatu vya kata hiyo walioathirika na mvua iliyonyesha usiku wa Machi 3, 2015.
Rais Kikwete amewaambia wananchi hao: “Nimekuja kuwapeni pole kutokana na maafa ya mvua. Napenda kuwahakikishieni kuwa Serikali iko nanyi. Msiba wenu ni msiba wetu, huzuni yenu ni huzuni yetu na machungu yenu ni machungu yetu.”
Rais Kikwete amewaambia wananchi kuwa Serikali itaendelea kuzikarabati nyumba ambazo ziko katika hali ya kukarabatiwa. “Zile za ukarabati tutaendelea kuzikarabati na zile zilizoharibika kabisa tutazijenga. Naambiwa zinahitaji kiasi cha Sh. Bilioni mbili, tutazitafuta na tutajenga kwa vyovyote vile. Naambiwa kuwa ni nyumba 403 mpya. Hakuna atayepewa fedha taslim, na wala mtu asije kuomba fedha, ili ajenge mwenyewe. Na wala zamu hii hakuna tenda kwa sababu tutatumia Jeshi letu la kujenga taifa – tayari nimewaambia waifanye hii kazi. Hii ni dharura na chombo chetu cha dharura ni Jeshi letu.”
Rais Kikwete pia amewashukuru wote ambao wamekuwa wanatoa misaada ya kusaidia wahanga wa mvua hiyo, ikiwa ni pamoja na wale ambao wametoa makazi ya dharura kwa waathirika na misaada mingine.
Rais Kikwete pia amesema kuwa Serikali itaendelea kutoa misaada ya dharura kwa waathirika hadi watakapokuwa na uwezo wa kujitegemea wenyewe: “Tayari Serikali imetoa tani 20 za chakula, tumetoa mafuta na sukari. Tutaendelea kuwaunga mkono mpaka mvuke. Aidha, hakuna yoyote ambaye atapoteza maisha kwa sababu ya ukosefu wa chakula. Tayari kuna chakula cha kutosha mwezi mmoja mpaka mwezi ujao na kikiisha tutaleta kingine.”
Rais Kikwete ameongeza: “Tutakabiliana pia na magonjwa ya mlipuko. Tayari tuna kituo cha dharura cha afya na kinatoa huduma mzuri.”
Rais Kikwete ameamuru uongozi wa Mkoa wa Shinyanga kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Kahama kuhakikisha kuwa yananunuliwa magodoro ya haraka ili watoto waweze kulala vizuri na kuepukana na magonjwa ya vichomi.
“Magodoro yatapatikana kesho, yapo hapa Kahama na kama hakuna yafuatwe hata Shinyanga. Lakini lazima yapatikane kesho (Ijumaa, Machi 13, 2015). Naambiwa mahitaji ya magodoro ni 649, tayari 558 yamepatikana na bado yapo mahitaji ya magodoro 149 na haya tutaleta kesho,”amesema Rais Kikwete.
Kuhusu imani za ushirikina ambazo zinaanza kuandamana na tukio la mvua hiyo, Rais Kikwete amesema: “Msijiingize katika mambo ya ushirikina na ramli. Mvua za mawe ni za kawaida duniani hata kama hazijapata kunyesha hapa. Msitoke hapa kwenda kutafuta waganga kuhusiana na mvua hii ili mpate sababu ya kuua watu.”
Ameongeza: “Mvua za namna hii ni matukio ya kawaida na maisha ya kawaida katika maeneo mengine. Hakuna mchawi hapa, bali ni rehema za Mwenyezi Mungu. Nimesikia sikia mambo haya. Hayana kichwa wala miguu. Hili ni tukio la kawaida.”
Amesisitiza Rais Kikwete: “Napenda kuwahakikishia kuwa Serikali yenu ipo. Acheni kuamanika, acheni kubabaika. Asiwababaishe mtu yoyote. Leo nimekuja mwenyewe mkubwa wa Serikali. Watakuja wengi kuwadanyanga, hawana Serikali. Wakija waambieni hivi – mwenye Serikali tuliyemchangua kaja, keshatuahidi, chakula tunakula, huduma za awali tumezipata na hizo nyingine amesema atatutimizia. Ili kuja kuwapeni pole mwambieni awapeni pole tu, asiwababaishe.”
Imetolewa na;
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu – Dar es Salaam.
12 Machi, 2015
SOMA ZAIDI >>> »

Monday, March 2, 2015

HOTUBA YA MWISHO WA MWEZI FEBRUARI, 2015 YA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA,MHESHIMIWA DKT. JAKAYA MRISHO KIKWETE

17
Utangulizi
Ndugu Wananchi;
Kama ilivyo ada tunamshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kutuwezesha kuzungumza kupitia utaratibu wetu huu mzuri wa hotuba za kila mwisho wa mwezi. Kwa mwisho wa mwezi wa Februari nina mambo matano ninayopenda kuyazungumzia. 
Zoezi la Uandikishaji Wapiga Kura
Ndugu Wananchi;
Jambo la kwanza ni uandikishaji wa Wapiga Kura. Tarehe 24 Februari, 2015 Waziri Mkuu, Mheshimiwa Mizengo Kayanza Peter Pinda alizindua rasmi uandikishaji wa wapiga kura ikiwa ni sehemu ya zoezi la uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura nchini. Zoezi hili lilizinduliwa Makambako, Mkoani Njombe na litaendelea nchini kote mpaka litakapokamilika kwa mujibu wa ratiba itakayopangwa na Tume ya Uchaguzi. Uandikishaji unatumia teknolojia ya kisasa ya utambuzi wa alama za vidole (BVR) na macho ya mtu anayeandikishwa. Teknolojia hii itatusaidia kuondoa kutoaminiana, manung’uniko na madai kuhusu udanganyifu katika chaguzi zetu kwamba wamepiga kura wasiostahili. Kuanza kutumika kwa teknolojia hii ni kielelezo cha utashi wa Serikali kuwa nchi yetu iwe na chaguzi zilizo huru, wazi na haki.

Ndugu Wananchi;
Mtakumbuka kuwa, kabla ya uzinduzi wa zoezi hili, Tume ya Taifa ya Uchaguzi ilifanya zoezi la majaribio ya uandikishaji wa wapiga kura kwa kutumia mashine za teknolojia hii mpya katika kata 10 katika Halmashauri za Kinondoni, Kilombero na Mlele kati ya tarehe 15 hadi 23 Desemba, 2014. 
Habari njema ni kuwa, kwa kutumia mashine za BVR, idadi ya waliojiandikisha ilivuka lengo la uandikishaji kwa kipindi kilichopangwa katika Kata hizo. Katika Halmashauri ya Kilombero walioandikishwa walifikia asilimia 110.9 ya lengo, katika Halmashauri ya Mlele uandikishaji ulifikia asilimia 101 ya lengo na katika Jimbo la Kawe, katika Halmashauri ya Wilaya ya Kinondoni walioandikishwa walikuwa asilimia 105.67 ya lengo. Mafanikio haya ni ya kutia moyo pamoja na changamoto za kiufundi zilizojitokeza na zile zinazotokana na upya wa mfumo wenyewe kwa watumiaji. Changamoto hizo zimefanyiwa kazi na watengenezaji wa vifaa vinavyotumika katika awamu hii ya uandikishaji wa wapiga kura nchi nzima. 
Ndugu Wananchi; 
Nimefarijika na taarifa kuwa zoezi la uboreshaji wa Daftari na uandikishaji wa wapiga kura limeanza vizuri Makambako. Wananchi wamejitokeza kwa wingi kuliko ilivyotarajiwa. Kati ya tarehe 23 hadi 25 Februari, 2015 kwa mfano, Tume ilitegemea kuandikisha wapiga kura 9,541 lakini kutokana na mwamko wa wananchi kuwa mkubwa wameweza kuandikisha wapiga kura 13,042. Kila kituo kilikuwa kinaandikisha kati ya wapiga kura 80 na 150 kwa siku. Lengo la Tume ni kuandikisha wapiga kura 32,000 katika Halmashauri ya Makambako ambako kwa siku wanatarajia kuandikisha watu 4,320. Naambiwa kuwa hesabu za juzi na jana wameandikisha hadi wapiga kura 6,000 kwa siku. Kwa kasi hii na kama mambo yatakwenda kama inavyotarajiwa, lengo hilo litafikiwa na hata kuvukwa.
Ndugu Wananchi;
Hatuna budi kutoa pongeza kwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwa hatua hii ya kutia moyo tuliyofikia katika mchakato huu. Inaondoa hofu iliyoanza kuingia miongoni mwa baadhi ya watu kuwa huenda zoezi hili lisingefanikiwa. Tunachokitaka kwa Tume ni kuona zoezi hili linaendelea na kukamilika kama ilivyopangwa. Napenda kurudia ahadi niliyokwishaitoa kwa Tume kwamba Serikali itafanya kila linalowezekana kuiwezesha kirasilimali ili iweze kutimiza jukumu lake hilo. Nimekwishawakumbusha Hazina kuhusu umuhimu wa zoezi hili kufanikiwa kama ilivyopangwa. Hivyo basi, nimewataka wahakikishe kutoa kipaumbele cha kwanza katika mgao wa fedha. Kama haifanyiki nawaomba Tume waniambie mimi mwenyewe.
Wito wangu kwenu, wananchi wenzangu, ni kujitokeza bila ya kukosa kwenda kujiandikisha kwa mujibu wa ratiba ya uandikishaji katika maeneo yenu kama itakavyotolewa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi. Msifanye ajizi maana hakutakuwepo na fursa nyingine ya kujiandikisha kabla ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu baada ya fursa hii kupita. 
Ndugu Wananchi;
Kama ilivyoelezwa na Tume na mimi kusisitiza mara kadhaa kuwa watakaojiandikisha wakati huu ndio watakaopiga kura ya maoni kuhusu Katiba Inayopendekezwa na ndio watakaopiga kura katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba, mwaka huu. Vitambulisho vya zamani vya mpiga kura havitatumika, hivyo watu wote ambao ni Watanzania na wana umri wa miaka 18 au zaidi lazima wajitokeze kuandikishwa upya. Watu pekee ambao hawatapaswa kujiandikisha tena ni wale tu walioandikishwa katika zoezi la majaribio lililofanyika katika zile kata 10 za Halmashauri za Kinondoni, Ifakara na Mlele mwezi Desemba, 2014. Vitambulisho walivyopata ndivyo vyenyewe.


Ndugu Wananchi;
Napenda kutumia nafasi hii pia kuwaomba viongozi wa vyama vya siasa, Serikali, dini na asasi za kiraia kuungana na Serikali na Tume ya Uchaguzi katika kuwakumbusha na kuwahamasisha wananchi wakajiandikishe. Naomba tusiwachanganye wananchi kwa kutoa taarifa zisizokuwa za kweli na kuwafanya wakaacha kujiandikisha. Sisi katika Serikali tunafanya kila linalowezekana kuhakikisha kuwa kila atakayejitokeza kujiandikisha anaandikishwa. Aidha, tutahakikisha kuwa kila panapojitokeza changamoto zinatafutiwa ufumbuzi kwa wakati mwafaka. 
Tunatambua kuwa mfumo huu ni mpya hivyo panaweza kujitokeza changamoto zinazosababishwa na upya wake. Nawaomba wahusika kuendelea kuwaelimisha watendaji wanaohusika ili wapate uzoefu unaostahili. Aidha, nawasihi wananchi kuwa wavumilivu na waelewa pale ambapo wakati mwingine watalazimika kukaa kwenye mistari kwa muda mrefu kusubiri kujiandikisha, au wakalazimika kuja siku ya pili. 
Ndugu Wananchi;
Kupiga kura kuamua kuhusu Katiba Inayopendekezwa au kuchagua Rais, Wabunge na Madiwani ni haki na wajibu wa kila raia. Lakini, kuipata haki hiyo na kuweza kutimiza wajibu huo kunategemea kuwa na kitambulisho cha mpiga kura. Bila ya hivyo haiwezekani. Haya shime jitokezeni, mjiandikishe, ili muweze kuitumia haki yenu na kutimiza wajibu wenu wa kuipigia kura Katiba Inayopendekezwa na kuchagua viongozi mnaowaona wanafaa kuongoza nchi yetu, jimbo lako na kata yako.
Kura ya Maoni
Ndugu Wananchi;
Jambo la pili ninalotaka kulizungumzia ni kuhusu Kura ya Maoni ya Katiba Inayopendekezwa. Kama mjuavyo, baada ya Bunge Maalumu la Katiba kutunga Katiba Inayopendekezwa na Rais kuchapisha Katiba hiyo katika Gazeti la Serikali na kutangaza siku ya kupiga kura ya maoni, kinachoendelea sasa ni matayarisho ya kufanyika kwa kura hiyo. Yapo majukumu ya Serikali, yapo majukumu ya Tume ya Uchaguzi, na yapo majukumu ya Serikali na Tume kwa pamoja. Utekelezaji umeishaanza na unaendelea. Miongoni mwa mambo yanayotakiwa kufanyika ni uandikishaji wa wapiga kura ambao umekwishaanza na unaendelea. 
Ipo pia kazi ya kuchapisha na kusambaza Katiba Inayopendekezwa ili wananchi waweze kuisoma na kuielewa kabla ya kupiga kura ya maoni. Tayari Katiba Inayopendekezwa imetangazwa katika tovuti za Wizara ya Katiba na Sheria, Wizara ya Habari, Utamaduni, Vijana na Michezo na katika tovuti ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali. Pia imechapichwa magazetini. 
Hadi tarehe 27 Februari, 2015 vitabu 1,558,805 vilikuwa vimechapishwa na nakala 1,341,300 kusambazwa. Nakala 1,141,300 zimesambazwa kwenye mikoa 25 ya Tanzania Bara na nakala 200,000 zimegawiwa kwa Zanzibar. Kwa upande wa Tanzania Bara kila Kata imepewa vitabu 300. Kwa vile Kata zina wastani wa vijiji vitano (5) hii ina maana kwamba kila kijiji kimepata vitabu 60 kwa kila kijiji ambayo si haba. 
Ndugu Wananchi;
Tume ya Uchaguzi itatoa maelekezo kuhusu utaratibu wa kutoa elimu kwa umma. Nimeambiwa tayari asasi za kiraia 420 kwa upande wa Bara na 75 kwa upande wa Zanzibar zimejiandikisha kwa ajili ya zoezi hilo. Halikadhalika, Tume itatoa maelekezo husika kuhusu kampeni ya Kura ya Maoni wakati ukiwadia. Naomba watu wawe na subira na kuzingatia masharti ya Sheria ya Kura ya Maoni na Kanuni zake. Tukifanya hivyo, zoezi hili muhimu na la kihistoria litatekelezwa kwa usalama na utulivu. Watu watafanya uamuzi kwa uhuru, uelewa, amani na usalama. 
Hali ya Usalama Nchini
Ndugu wananchi;
Jambo la tatu ninalotaka kulizungumzia ni hali ya usalama nchini. Kwa jumla hali ya usalama ni nzuri, hata hivyo kuna matukio ya kiusalama ambayo ningependa kuyazungumzia. La kwanza ni mashambulizi yenye sifa za ujambazi na mwelekeo wa kigaidi. Na, la pili ni la mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi.
Katika kipindi cha miezi 12 hivi kumekuwa na matukio ya watu kuvamia vituo vya Polisi, wengine wanachoma moto au wengine wanapora silaha. Pia kumekuwepo na matukio ya kuwashambulia Polisi walioko kwenye doria na wengine kuporwa silaha. Vituo vya Polisi vilivyovamiwa na silaha kuporwa ni vya Newala Mkoani Mtwara silaha tatu ziliporwa, Ikwiriri katika Wilaya ya Rufiji silaha saba, Kimanzichana, Wilaya ya Mkuranga silaha tano, mbili za polisi na tatu za raia waliokwenda kuzihifadhi pale, na Ushirombo Wilaya ya Bukombe silaha 18. Pugu Machinjioni na Tanga, askari waliokuwa katika shughuli za ulinzi na doria walishambuliwa na kuporwa silaha tatu. Kule Songea kulikuwepo na matukio mawili ya Polisi kushambuliwa lakini silaha hazikuporwa.
Bahati mbaya, vijana wetu saba wa Jeshi la Polisi walipoteza maisha katika matukio hayo. Newala alikufa Polisi mmoja, Kimanzichana mmoja, Ikwiriri wawili, na Ushirombo watatu. Wapo Polisi kadhaa waliopata majeraha ya namna mbalimbali katika mashambulizi haya. 
Ndugu Wananchi;
Silaha zote 18 zilizoporwa Ushirombo zimepatikana na watu 10 wanaotuhumiwa kuhusika na uhalifu huo wamekamatwa. Katika tukio la Tanga silaha moja kati ya mbili zilizoporwa imepatikana. Watuhumiwa saba wametiwa mbaroni, wanne kati yao ni wale waliokuwa wamejifisha katika mapango ya Kiomoni katika Kitongoji cha Karasha-mikocheni, kilichoko kijiji cha Mzizima wilayani Tanga. Tayari watu wanne wanaotuhumiwa kuhusika na tukio la Ikwiriri wamekamatwa. Polisi wanaendelea na upelelezi kuwapata watu wengine na kuzipata silaha saba zilizoporwa kituoni hapo. Kwa tukio la Newala silaha zote tatu zimepatikana pamoja na bastola moja ya mtuhumiwa aliyehusikaa na watu wawili wametiwa nguvuni. Hali kadhalika, upelelezi unaendelea wa kuzipata silaha zilizoporwa ambazo hazijapatikana mpaka sasa: yaani Kimanzichana moja, Pugu Machinjioni moja na Tanga iliyosalia moja. 
Ndugu Wananchi;
Matukio haya yana sura mbili. Yana sura ya ujambazi, lakini pia baadhi yake yana dalili za ugaidi. Vyombo vyetu vya usalama vinaendelea kufanya kazi yake ya uchambuzi wa kila tukio na kulipa nafasi yake stahiki. Napenda kutumia nafasi hii kutoa pongezi za dhati kwa Jeshi la Polisi wakishirikiana na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania na vyombo vingine vya usalama kwa kazi kubwa na nzuri waifanyayo kupambana na uhalifu nchini. Mafanikio tunayaona, kama nilivyoeleza na kama tulivyosikia kule Tanga hivi karibuni ni matunda ya ushirikiano huo. Hata hivyo, nimewataka waendelee kuwasaka watu hawa waovu po pote walipo ili wafikishwe mahakamani na kuzirejesha mikononi mwa Polisi silaha zote zilizoporwa. 
Nawaomba wananchi wenzangu wote kushirikiana kwa karibu na vyombo vya usalama hususan Jeshi la Polisi ili tuweze kupata mafanikio zaidi dhidi ya uhalifu huu na uhalifu mwingineo. Nawaomba mfanye mambo mawili: Kwanza, toeni taarifa Polisi mnapozipata habari za vitendo viovu au nyendo za watu waovu wanavyokusudia kufanya wahalifu au taarifa za wale waliokwishafanya uhalifu. 
Pili, naomba watu waache kuwashabikia watu hawa waovu wala kueneza taarifa zao potofu kwenye mitandao ya kijamii. Badala yake tutumie mitandao ya kijamii kuponda fikra zao potofu, fikra zao hasi na vitendo vyao viovu pamoja na kuwafichua wao na mambo yao mabaya wayafanyo. Napenda kutumia nafasi hii kuwashukuru na kuwapongeza wananchi wote walioweza kutoa taarifa zilizowezesha kuzuia uhalifu usifanyike au zilizowezesha kutiwa mbaroni kwa wahutumiwa wa vitendo vya ujambazi na ugaidi. Hatuwezi kushinda uhalifu bila ushirikiano baina ya wananchi na vyombo vya ulinzi na usalama.
Mauaji ya Watu Wenye Ulemavu wa Ngozi
Ndugu wananchi;
Nimesikitishwa sana na taarifa kuwa mauaji ya ndugu zetu wenye ulemavu wa ngozi (Albino) yameibuka upya baada ya hali kuwa tulivu mwaka 2011. Mwaka jana (2014) yalitokea matukio matatu katika mikoa ya Mwanza, Tabora na Simiyu na mwaka huu limetokea tukio moja mkoani Geita. 
Lazima tulaani vikali mauaji ya ndugu zetu albino. Ni vitendo vya kinyama ambavyo havitegemewi kufanywa au kutokea katika jamii yeyote ya watu waliostaarabika, ya watu wanaomuabudu Mungu. Watu wenye ulemavu wa ngozi ni wanadamu wenzetu, wenye haki sawa ya kuishi na kupata hifadhi ya maisha yao kama walivyo wanadamu wengine. Hawastahili kufanyiwa wanayofanyiwa. Hawapaswi kuishi kwa hofu katika kijiji chao, mtaa wao au katika nchi yao. Jamii nzima na sisi sote mmoja mmoja na katika umoja wetu, tunao wajibu wa kuhakikisha usalama wa maisha yao na mali zao kama ilivyo kwa watu wengine wote. 
Kwa kweli, mauaji ya albino ni jambo linalofedhehesha na kulidhalilisha taifa letu. Ni vitendo visivyovumilika. Hatuna budi sote kushikamana na kuhakikisha kuwa tunapambana nao kisawasawa na kuwashinda. Tusikubali kamwe wakaturudisha kule kubaya tulikokuwa zamani. Naungana na Chama cha Albino Tanzania kulaani ukatili huu na kutaka watu wote wanaojihusisha na ukatili huu wasakwe, wakamatwe, wafikishwe Mahakamani na kupewa adhabu kali inayowastahili wanapopatikana na hatia. 
Ndugu Wananchi;
Napenda kuwahakikishia kuwa wakati wote Serikali imelipa uzito mkubwa suala la kudhibiti na kukomesha mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi au kukatwa baadhi ya viungo vyao wenyewe wakiwa hai. Tumefanya hivyo bila ya kuchoka tangu tukio la kwanza baada ya mimi kuingia madarakani Aprili 17, 2006 na miezi mitatu tu kule Nyahunge, Geita alipouawa Alfa Amon ambapo watuhumiwa wawili waliuawa na raia. Mwaka 2007 kulikuwa na matukio saba. Mwaka 2008 ndio ulikuwa mwaka mbaya sana walipouawa watu 18. 
Kutokana na jitihada kubwa zilizofanywa na Serikali kwa kushirikiana na wananchi mauaji yalipungua na kuwa tisa mwaka 2009. Mwaka 2010 kukawa na tukio moja na mwaka 2011 hapakuwepo na tukio lolote. Mwaka 2012 kukawa na tukio moja, mwaka 2013 aliuawa mtu mmoja na wawili kujeruhiwa. Mwaka 2014 waliuawa watu watatu na wawili kujeruhiwa, na Januari, 2015 kumetokea tukio moja kule Geita. 
Ndugu Wananchi;
Tangu mwaka 2006 mpaka 2015, watuhumiwa 139 wametiwa nguvuni, miongoni mwao wako watuhumiwa 16 wa matukio ya Desemba na Januari mwaka huu. Mashauri 35 yamefunguliwa mahakamani na kati ya hayo 10 bado yanaendelea na yapo katika hatua mbalimbali. Watuhumiwa 73 wameachiliwa na 15 wamepatikana na hatia. Kati ya hao waliopatikana na hatia 13 wamehukumiwa kifo na wawili wamepata kifungo cha miezi 6. Watuhumiwa kwa matukio sita bado wanasakwa.
Matukio ya mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi yametokea katika mikoa kumi kati ya mikoa 30 hapa nchini. Mikoa hiyo ni hii ifuatayo: Mwanza matukio 13, Kagera sita, Tabora matano, Geita manne, Mara manne, Kigoma manne, Simiyu matatu, Shinyanga mawili, Arusha moja na Mbeya moja. Utaona matukio 41 kati ya 43 yametokea katika ukanda wa ziwa ambapo pia wanaongoza kwa mauaji ya vikongwe na wanawake kwa sababu za ushirikina. 
Ndugu Wananchi;
Inawezekana kuwa matukio ya hivi karibuni yanaashiria kuwa uhalifu huu unataka kuibuka upya. Napenda kuwahakikishia ndugu zetu wenye ulemavu wa ngozi na Watanzania kwa jumla, kuwa hatutaacha hali iwe mbaya kama ilivyokuwa miaka ya nyuma. Tutatumia mbinu na maarifa tuliyoyatumia kukabili wimbi kubwa la mauaji lililokuwepo mwaka 2007 na 2008 na kwa sababu hiyo tukaweza kupunguza hadi kufikia kutokuwa na tukio lolote la mauaji mwaka 2011. 
Tunachokiomba kutoka kwa wananchi ni ushirikiano na msaada wa kuwafichua watu wanaofanya vitendo vya mauaji na kukata viungo vya watu wenye ulemavu wa ngozi. Pia wasaidie kutoa taarifa kuhusu wanunuzi wa viungo hivyo na waganga wanaochochea mahitaji ya viungo vya albino. Ushirikiano wa wananchi wa wakati ule uliwezesha kupatikana kwa mafanikio niliyaeleza. Naamini safari hii tukifanya hivyo tutafanikiwa pia.
Ndugu Wananchi; 
Kutokomeza kabisa matukio ya mauaji na ukataji wa viungo vya watu wenye ulemavu wa ngozi ni jambo linalowezekana. Hata hivyo, litategemea watu kuacha imani za ushirikina. Imani potofu, ati kuwa mtu akiwa na kiungo cha mtu mwenye ulemavu wa ngozi atafanikiwa katika shughuli zake za biashara, uvuvi na uchimbaji wa madini ndicho kichocheo cha uovu wote huu unaoendelea. Ni ujinga ulioje kwa mtu kuamini kuwa mafanikio yake hayatategemea juhudi zake na maarifa yake bali kuwa na kiungo cha mwanadamu mwenzake mwenye ulemavu wa ngozi. 
Nilisema katika hotuba yangu ya mwisho wa mwezi Machi, 2008 kwamba, kama kuwa na kiungo cha albino ndiko kutakakomfanya mtu kufanikiwa katika shughuli zake za kibiashara na kiuchumi basi ndugu zetu wenye ulemavu wa ngozi wangekuwa ndiyo matajiri wakubwa nchini na duniani. Maana wao sio tu wana viungo bali wana mwili mzima. Kwa sababu ya kuwepo imani hizi za hovyo, juhudi za kuelimisha jamii kuachana na imani hizi potofu ziongezwe. Naomba hili ndilo liwe jambo la msingi katika mapambano haya. Tukifanikiwa katika hili, matatizo yote haya yatakoma. Serikali na jamii haitalazimika kushughulikia mambo haya ambayo siyo tu ni fedheha hata kumsimulia mtu bali yanatisha na kusikitisha.
Ndugu Wananchi;
Wiki ijayo nitakutana na baadhi ya viongozi na wanachama wa Chama cha Watu Wenye Ulemavu wa Ngozi. Nimekubali maombi yao ya kukutana nao ili niweze kusikiliza maoni yao na tubadilishane mawazo juu ya namna bora ya kumaliza tatizo hili. Mimi naamini kuwa ushirikiano wa karibu kati ya Serikali na jamii utatuwezesha kutokomeza mauaji ya ndugu zetu wenye ulemavu wa ngozi na kuliondolea taifa letu aibu hii. 
Ziara ya Zambia
Ndugu Wananchi;
Tarehe 25 na 26 Februari, 2015 nilifanya ziara ya siku mbili ya kiserikali nchini Zambia kwa mwaliko wa Rais mpya wa nchi hiyo, Mheshimiwa Edgar Lungu. Ziara ilikuwa na mafanikio makubwa. Mimi na ujumbe wangu tulifarijika sana kuona kuwa mawazo ya nchi zetu mbili yanashabihiana sana kuhusu namna ya kuimarisha na kuboresha uhusiano wetu na ushirikiano na uhusiano wa nchi zetu mbili. Kimsingi tumekubaliana katika masuala yote muhimu tuliyoyazungumza. 
Kuhusu TAZARA tumekubaliana kuchukua hatua thabiti kutatua matatizo ya kiungozi, kifedha na kiufundi yanayolikabili shirika letu hilo hivi sasa. Tumeelewana kuwa hatuna budi kufanya marekebisho ya kimfumo na kiutendaji ili kutatua matatizo ya kimuundo na kimenejimenti yanayochangia kuzorota kwa ufanisi wa Shirika. Tumekubaliana pia kuwa, Serikali zetu mbili zitekeleze ipasavyo wajibu wake kwa TAZARA ikiwa ni pamoja na kutoa mchango wake wa fedha kwa ajili ya kulifufua Shirika hili muhimu kwa uchumi wa nchi zetu mbili. 
Ndugu Wananchi;
Tumekubaliana pia, kwamba, tuangalie uwezekano wa kuruhusu makampuni au mashirika mengine ya reli kutumia reli ya TAZARA kusafirishia mizigo yao kwa kulipa ushuru kwa TAZARA kwa huduma hiyo. Tumeagiza Baraza la Mawaziri kulifanyia kazi wazo hili jema ili litekelezwe mapema iwezekanavyo. 
Kwa upande wa sekta ya nishati, tumekubaliana kuwa, nchi zetu mbili ziendelee kushirikiana kuimarisha bomba la mafuta la TAZAMA. Ndugu zetu wa Zambia walitueleza dhamira yao ya kutaka kujenga bomba la kusafirisha gesi kutoka Dar es Salaam hadi Zambia. Wameomba tukubali kuwauzia gesi asilia. Niliwaeleza ni jambo linaowezekana, tumekubaliana nchi zetu zilifanyie kazi ombi hilo. 
Serikali ya Zambia, imeahidi kuimarisha njia ya umeme kutoka Kasama hadi Mbala Zambia inakoanzia njia inayoleta umeme Sumbawanga. Kufanya hivyo kutaondoa matatizo ya sasa ambapo umeme unaofika Sumbawanga kutoka Mbala huwa mdogo kiasi kwamba hauna nguvu ya kutosha kwa matumizi ya nyumbani, maofisini na viwandani. Kwa sababu hiyo, hata mpango wa kuupeleka umeme huo Namanyere, Nkasi na Mpanda haukuweza kutekelezwa kama ilivyokuwa imekusudiwa awali.
Ndugu Wananchi; 
Kuhusu kuboresha huduma kwa abiria na mizigo katika mpaka wa Tanzania na Zambia pale Tunduma, tumekubaliana kuwa, Serikali ya Tanzania ikamilishe ujenzi wa jengo litakalowezesha huduma zote muhimu za mpakani kutolewa katika jengo hilo (One Stop Border Post). Wakati tunasubiri kukamilisha ujenzi huo, tumekubaliana tuwe na jengo la muda la kurahisisha taratibu za usafiri wa abiria na usafirishaji wa mizigo katika mpaka wetu na Zambia. 
Vilevile, tulizungumzia njia za kuimarisha na kuboresha taratibu za forodha kwa mizigo itokayo bandari ya Dar es Salaam kwenda Zambia na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kupitia Zambia. Tumekubaliana kuwa, Mamlaka ya Kodi ya Mapato ya Zambia iangalie uwezekano wa kuwaweka maafisa wake katika Bandari ya Dar es Salaam kama inavyofanyika kwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Hii itarahisisha taratibu za forodha kwa bidhaa za Zambia katika bandari yetu. Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imeshaanza mchakato wa kupata fursa hiyo. Kwa jumla, ziara ilikuwa ni yenye mafanikio makubwa.
Rambirambi
Ndugu Wananchi;
Wakati tulipokuwa tunajiandaa kurekodi hotuba hii tukapata habari ya huzuni na majonzi makubwa ya kifo cha Mbunge wa Mbinga Magharibi, Mheshimiwa Capt. John Damian Komba. Kifo chake kimeliondolea taifa letu mmoja wa viongozi wake wazuri, msanii mahiri, raia mwema na mzalendo wa kweli. Marehemu alitumia muda mwingi wa maisha yake kuelimisha jamii kuhusu mambo mema, amefanya hivyo akiwa mwalimu na baadaye Kiongozi wa Kikundi cha Sanaa cha JWTZ na hapa mwishoni kiongozi wa kikundi cha Tanzania One Theatre cha Chama Cha Mapinduzi. Kwa kutumia kipaji alichojaaliwa na Mola wake ametoa mchango mkubwa kwa maendeleo ya nchi yetu na ustawi wa Chama Tawala. Daima tutamkumbuka kwa mambo mengi mema aliyoifanyia jamii ya nchi yetu na taifa kwa jumla.
Ndugu Wananchi;
Katika salamu zangu za rambirambi kwa Spika wa Bunge na Katibu Mkuu wa CCM niliwaomba kupitia kwao salamu ziwafikie Wabunge wote na viongozi na wanachama wa Chama Cha Mapinduzi. Hali kadhalika, niliomba kupitia kwao salamu ziwafikie familia ya marehemu Capt. John Komba. Kwa familia ya ndugu yetu mpendwa, napenda kuwahakikishia kuwa tuko pamoja nao katika kipindi hiki kigumu cha majonzi na maombolezo. Tunawaombea kwa Mola awape moyo wa subira na uvumilivu. Wananchi wa Wilaya ya Nyasa tunawapa pole nyingi kwa msiba mkubwa uliowakuta na pengo kubwa mlilolipata. Nawaomba watambue kuwa namna bora zaidi ya kumlilia Mbunge wao aliyewapenda ni kudumisha mema yote aliyofanya na kukamilisha zile kazi ambazo alikusudia kuzifanya lakini hakuweza kufanya hivyo kwa sababu ya kukutwa na umauti.
Mwisho nawaomba, Watanzania wote tuungane na familia yake kumwombea marehemu Capt. John Damian Komba mapumziko mema. Amin.
Mungu Ibariki Afrika!
Mungu Ibari ki Tanzania!
Asanteni kwa kunisikiliza.
SOMA ZAIDI >>> »

Wednesday, February 25, 2015

RAIS KIKWETE AFANYA ZIARA YA KIKAZI NCHINI ZAMBIA

ZAM1 
Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete na mkewe Mama Salma wawasili katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Kenneth Kaunda jijini Lusaka Zambia na kupokewa na mwenyeji wao Rais Edgar Lungu wa Zambia leo asubuhi kwa ziara ya kikazi ya siku mbili.(PICHA NA FREDDY MARO WA IKULU)ZAM2 
Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete na mkewe Mama Salma wawasili katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Kenneth Kaunda jijini Lusaka Zambia na kupokewa na mwenyeji wao Rais Edgar Lungu wa Zambia leo asubuhi kwa ziara ya kikazi ya siku mbili
  
   ZAM3
   ZAM4 
Rais Kikwete na Rais Lungu wa Zambia wakipokea heshima ya mizinga 21 mara baada ya kuwasili.
SOMA ZAIDI >>> »

Tuesday, December 2, 2014

RAIS KIKWETE AMWAPISHA CAG MPYA IKULU DAR ES SALAAM LEO

Rais Jakaya Mrisho kikwete akimuapisha Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG) Profesa Musa Juma Assad Ikulu jijini Dar es salaam leo Desemba 2, 2014
Rais Jakaya Mrisho kikwete akitia sahihi yake kwenye nyaraka baada ya kumuapisha Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG) Profesa Musa Juma Assad Ikulu jijini Dar es salaam leo






SOMA ZAIDI >>> »

Monday, December 1, 2014

RAIS KIKWETE AMTEUA PROFESA MUSSA JUMA ASSAD KUWA MDHIBITI NA MKAGUZI WA HESABU ZA SERIKALI (CAG)

THE UNITED REPUBLIC OF TANZANIA
DIRECTORATE OF PRESIDENTIAL COMMUNICATIONS

PRESIDENT’S OFFICE,
STATE HOUSE,
1 BARACK OBAMA ROAD,
11400 DAR ES SALAAM.
Tanzania.

Telephone: 255-22-2114512, 2116898
E-mail: ikulucommpress@googlemail.com
Website : www.ikulu.go.tz
Fax: 255-22-2113425

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amemteua Profesa Mussa Juma Assad kuwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).

Taarifa iliyotolewa leo, Jumatatu, Desemba Mosi, 2014 na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, inasema kuwa uteuzi wa Bwana Assad ulianza Novemba 5, mwaka huu, 2014.

Taarifa hiyo imeongeza kuwa Bwana Assad ataapishwa kesho, Jumanne, Desemba 2, saa nne asubuhi, Ikulu, Dar es Salaam.


Kabla ya uteuzi wake, Bwana Assad alikuwa Profesa Mshiriki, Idara ya Uhasibu, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na anachukua nafasi ya Bwana Ludovick Utouh ambaye amestaafu kwa mujibu wa Sheria za Utumishi wa Umma.

Profesa Assad ni msomi, mwenye weledi, ujuzi na uzoefu mkubwa wa uhasibu na udhibiti wa fedha ambaye ana Shahada ya Uzamivu wa Uhasibu (PHD in Accounting) kutoka Chuo Kikuu cha Southampton, Uingereza mwaka 2001 na Shahada ya Uzamivu katika Udhibiti wa Fedha (MA in Financial Accounting) kutoka Chuo Kikuu cha Dublin City, Jamhuri ya Ireland mwaka 1991.

Profesa Assad pia ana Stashahada ya Kitaaluma ya Uhasibu (Professional Diploma in Accounting) kutoka Chuo Kikuu cha Dublin City mwaka 1990 na Shahada ya Biashara (Bachelor of Commerce) ya Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam mwaka 1988.

Pamoja na uzoefu wa kitaaluma, Profesa Assad anao uzoefu mkubwa katika eneo la uhasibu na ukaguzi. Alikuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wahasibu na Wakaguzi (NBAA) kwa miaka saba (2007 - 2014); ni Rais na Mjumbe wa Chama cha Wahasibu Afrika (Pan African Federation of Accountants) tangu mwaka 2012; na ni mjumbe wa Bodi kadhaa za Wakurugenzi nchini Tanzania.

Katika kumteua Profesa Mussa Juma ASSAD kuwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, Rais anayo imani kubwa kuwa elimu, weledi, ujuzi na uzoefu ambao Profesa Assad anao utamwezesha kutekeleza vema majukumu ya nafasi hiyo muhimu sana katika utawala bora wa nchi yetu.

Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu – Dar es Salaam.

1 Desemba,2014
SOMA ZAIDI >>> »

Thursday, November 6, 2014

RAIS DKT. JAKAYA KIKWETE AENDA MAREKANI KUCHUNGUZWA AFYA YAKE


TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete ameondoka nchini jioni ya leo, Alhamisi Novemba 6, 2014, kwenda Marekani kwa ajili ya uchunguzi wa afya yake.

Rais Kikwete atakuwa Marekeni kwa muda wa siku kumi.

Mwisho.

Imetolewa na;
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu – Dar es Salaam.
06 Novemba,2014
SOMA ZAIDI >>> »

RAIS KIKWETE AWAAPISHA MAKATIBU WAKUU,WAKUU WA MIKOA,MABALOZI NA MAKATIBU TAWALA WA MIKOA IKULU JIJINI DAR ES SALAAM LEO

Rais Jakaya Mrisho Kikwete akimuapisha Mhe Samwel William Shellukindo kuwa Balozi na Msaidi wa Rais Masuala ya Diplomasia leo Ikulu jijini Dar es salaam

Rais Jakaya Mrisho Kikwete akimuapisha Mhe John Vianney Mongella kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kagera leo Ikulu jijini Dar es salaam.
Fais Jakaya Mrisho Kikwete akimuapisha Mhe Halima Omary Dendego kuwa Mkuu wa Mkoa wa Mtwara leo Ikulu jijini Dar es salaam.
Rais Jakaya Mrisho Kikwete akimuapisha Dkt Ibrahim Hamisi Msangi kuwa Mkuu wa Mkoa wa Katavi leo Ikulu jijini Dar es salaam
SOMA ZAIDI >>> »

Wednesday, November 5, 2014

RAIS KIKWETE AMEFANYA MABADILIKO YA BAADHI YA WAKUU WA MIKOA NCHINI








THE UNITED REPUBLIC OF TANZANIA
DIRECTORATE OF PRESIDENTIAL COMMUNICATIONS

Telephone: 255-22-2114512, 2116898
Website : www.ikulu.go.tz              

Fax: 255-22-2113425


PRESIDENT’S OFFICE,
      STATE HOUSE,
              1 BARACK OBAMA ROAD,  
11400 DAR ES SALAAM.
Tanzania.
 

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amefanya uteuzi wa wakuu wapya wanne wa Mikoa, amewahamisha wengine sita na ameamua kuwa wengine watatu watapangiwa kazi nyingine.
Taarifa iliyotolewa mjini Dodoma jioni ya leo, Jumatano, Novemba 5, 2014 na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue inasema kuwa, Wakuu wapya wa Mikoa ni Bi. Halima Omari Dendego ambaye anakuwa Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Dkt. Ibrahim Hamisi Msengi ambaye anakuwa Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Bi. Amina Juma Masenza ambaye anakuwa Mkuu wa Mkoa wa Iringa na Bwana John Vianney Mongella ambaye anakuwa Mkuu wa Mkoa wa Kagera.
Taarifa inasema kuwa kabla ya uteuzi wake Bi. Dendego alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Tanga, Dkt. Msengi alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Bi. Masenza alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Ilemela na Bwana Mongella alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Arusha.
Taarifa hiyo inasema kuwa Wakuu hao wapya wa Mikoa wataapishwa kesho, Alhamisi, Novemba 6, 2014 saa saba mchana, Ikulu, Dar es Salaam.
Aidha, taarifa hiyo imesema kuwa Wakuu wa Mikoa ambao watapangiwa kazi nyingine ni Kanali (Mst) Fabian Massawe wa Kagera, Dkt. Christine Ishengoma wa Iringa na Kanali Joseph Simbakalia wa Mtwara.
Wakuu wa Mikoa ambao wamehamishwa vituo vya kazi ni Bwana Magesa S. Mulongo ambaye anakwenda Mkoa wa Mwanza kutoka Arusha, Dkt. Rehema Nchimbi ambaye anakwenda Mkoa wa Njombe kutoka Dodoma, Bwana Ludovick John Mwananzila anakwenda Tabora kutoka Lindi, Kepteni (Mst) Anseri Msangi anayekwenda Mkoa wa Mara kutoka Njombe na Mhandisi Everist Ndikilo ambaye anakwenda Arusha kutoka Mwanza.
Wengine waliohamishwa ni Luteni (Mst) Chiku A.S. Galawa ambaye anakuwa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma kutoka Tanga, Dkt. Rajab Rutengwe ambaye anakwenda Mkoa wa Tanga kutoka Katavi, Bi Fatma Mwasa ambaye anakuwa Mkuu wa Mkoa wa Geita kutoka Tabora na Bwana Magalula S. Magalula ambaye anahamishiwa Lindi kutoka Geita.
Taarifa hiyo imesema kuwa Wakuu wa Mikoa ya Dar es Salaam, Kigoma, Kilimanjaro, Manyara, Mbeya,Morogoro, Pwani, Rukwa, Shinyanga, Ruvuma, Singida na Simiyu watabakia kwenye vituo vyao vya sasa.
Aidha, Rais Kikwete amefanya uteuzi wa Wakuu wapya wa Wilaya, kuhamisha baadhi yao na kutengua uteuzi wa baadhi. Taarifa kamili itatolewa na Waziri Mkuu baada ya kuwa wamepangiwa vituo vya kazi.

Mwisho.
Imetolewa na;
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu – Dar es Salaam.
05 Novemba,2014

SOMA ZAIDI >>> »