Pages

Showing posts with label Escrow. Show all posts
Showing posts with label Escrow. Show all posts

Friday, December 5, 2014

MMILIKI WA IPTL HATIMAYE ATEMA CHECHE

Mwenyekiti Mtendaji wa kampuni ya ufuaji umeme ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL) Bw. Harbinder Singh Sethi (wa pili kulia) akikabidhi hundi ya shilingi milioni 14.5 kwa Fadha Gerald Kamina (wa tatu kilia), kama msaada kwa jumuiya ya Kanisa la Mtakatifu Petro lililopo Oysterbay jijini Dar es Salaam, kusaidia ujenzi wa kanisa hilo. Pamoja nao ni Bi. Rose Rupia, Mwenyekiti wa Kamati ya Ujenzi wa Kanisa hilo (wa tatu kushoto), Katibu na Mwanasheria Mkuu wa IPTL Bw. Joseph Makandege (wa pili kushoto), Mwanasheria wa IPTL Melchisedeck Lutema (wa kwanza kushoto) na wa kwanza kulia ni Rajiv Bhesania, msaidizi wa Mwenyekiti mtendaji wa IPTL.
Mwenyekiti Mtendaji wa kampuni ya ufuaji umeme ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL) Bw. Harbinder Singh Sethi (wa pili kulia) akikabidhi hundi ya shilingi milioni 14.5 kwa Fadha Gerald Kamina (wa tatu kulia), kama msaada kwa jumuiya ya Kanisa la Mtakatifu Petro lililopo Oysterbay jijini Dar es Salaam, kusaidia ujenzi wa kanisa hilo. Pamoja nao ni Bi. Rose Rupia, Mwenyekiti wa Kamati ya Ujenzi wa Kanisa hilo (wa tatu kushoto), Katibu na Mwanasheria Mkuu wa IPTL Bw. Joseph Makandege (wa pili kushoto), Mwanasheria wa IPTL Melchisedeck Lutema (wa kwanza kushoto) na wa kwanza kulia ni Rajiv Bhesania, msaidizi wa Mwenyekiti mtendaji wa IPTL.
Mmiliki wa Kampuni ya Kufua Umeme ya IPTL, Habirnder Seth Singh amesema anafikiria mara mbilimbili iwapo aendelee kuwekeza nchini au la, baada ya kuwapo kwa tuhuma kwamba alihusika na uchotaji wa fedha katika Akaunti ya Tegeta Escrow katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
“Nimeongelewa sana kiasi kwamba naona kama hakuna hata amani ya kuwekeza Tanzania, nitajifikiria mara mbili mbili. Wananchi wanaelewa vingine kabisa kuhusu suala hili kwa sababu ya upotoshwaji,” alisema Singh alipozungumza na gazeti hili jana.
Singh ambaye alituhumiwa kujipatia asilimia 70 ya hisa katika Kampuni ya IPTL isivyo halali, alisema hafikirii kuwekeza zaidi nchini kwa sababu yamekuwapo maneno mengi na shutuma zisizo na ukweli zilizoelekezwa kwake kuhusu sakata hilo.
Kauli ya bosi huyo wa IPTL imekuja wakati Taifa likisubiri utekelezaji wa maazimio ya Bunge na akiwa mmojawapo wa watu wanaotakiwa kuchunguzwa na vyombo vya dola ili akibainika kufanya makosa, afikishwe mahakamani.
Jana, Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba alimtaka Rais Jakaya Kikwete kutekeleza haraka maazimio manane yaliyotolewa na Bunge dhidi ya ufisadi wa sakata la escrow.
“Rais hatakiwi kukaa kimya, atoe tamko la haraka ili kuwaondoa viongozi hao. Hata Waziri Mkuu anatakiwa kuwajibishwa kwa sababu ni chanzo cha udhaifu huo,” alisema Profesa Lipumba alipokuwa akizungumza kwenye Mkutano Mkuu wa Jumuiya ya Wanawake wa CUF (JUKECUF).
Jana, Ngeleja ambaye pia ni Mbunge wa Sengerema alisema: “Kwangu ni kama hukumu imetangulia mashtaka kwa sababu sikuwahi kuitwa kuhojiwa mahali popote, ila ninauheshimu uamuzi wa Bunge.”
Kwa upande wake, Jaji Mkuu wa Tanzania, Mohamed Chande Othman alisema hayuko tayari kuzungumzia masuala ya kashfa ya Akaunti ya Escrow pamoja na mwingiliano wa mihimili miwili, Bunge na Mahakama kwa kuwa siyo wakati wake.
Wakati hayo yakiendelea, uongozi wa Benki ya Stanbic Tanzania nao ulitoa taarifa ya kukana kuhusika katika utakatishaji fedha za Akaunti ya Tegeta Escrow, baada ya Bunge kupitisha azimio la kuitaka mamlaka husika za kifedha kuichunguza.
Malamiko ya Singh
Singh alisema kampuni yake imekuwa ikiuza umeme kwa bei nafuu; senti nane kuliko kampuni nyingine, lakini bado anaonekana kuwa na makosa.
“Kuuza umeme kwa senti nane kwa megawati ni bei nafuu sana lakini mbona naonekana kama nina makosa? Ndiyo maana ninasema nitafikiria mara mbili kuwauzia umeme,” alisema.
Alisema kampuni nyingine za kufua umeme zinauza umeme mara mbili ya bei kuliko yake, lakini bado anaonekana si mwekezaji mzuri huku mazuri yote aliyoyafanya nchini yakisahauliwa.
Alisema anashangazwa na kauli za wabunge na baadhi ya wanasiasa kuwa anatakiwa kukamatwa kwa kukwepa kodi na kujipatia fedha isivyo halali na kusema haoni kosa alilolifanya mpaka sasa.
“Wanikamate kwa lipi? Hata kutaifisha mali zangu au mitambo hawawezi kabisa hiyo ni kazi ya Mahakama,” alisema.
Alisema wanaomtuhumu kuwa kaiba fedha za umma hawana hoja na kwamba kama ingekuwa kweli, waliotakiwa kulalamika ni mmiliki mwenza wa zamani wa IPTL, James Rugemalira na raia wa Malaysia, aliyemtaja kwa jina moja la Barbin… “Wenyewe wahusika hawajasema kama wameibiwa lakini leo naambiwa na Bunge nimeiba na wanataka kutaifisha mali zangu inashangaza sana.”
Alisema ameshangazwa na jinsi Bunge lilivyomhukumu bila kupewa nafasi ya kujitetea… “Wao wanajadili bungeni, Mahakama haijatoa hukumu lakini wanamhukumu mtu ambaye hayupo hapo, hawajasikia utetezi wake. Inashangaza sana, kwa nini Mahakama isifanyie kazi suala hili na kutoa hukumu?”
Kuhusu utata wa uraia wake, Singh alisema hakuna ukweli wowote kuwa yeye ni Mkenya au wa Afrika Kusini na kusisitiza kuwa ni Mtanzania, mzaliwa wa Iringa. “Mimi ni Mtanzania, unafikiri mimi Mhindi?” alihoji Singh.
Kauli ya Ngeleja
Kwa upande wake, Ngeleja naye alilalamikia kutohojiwa na kusema: “Siwezi kufahamu kwa nini sikuitwa kuhojiwa maana hata maaskofu nimesikia kwenye vyombo vya habari kwamba nao wanalalamika hawakuhojiwa, pengine inawezekana muda ulikuwa mfupi, hilo sifahamu.”
Ngeleja ambaye aliwahi kuwa Waziri wa Nishati na Madini kabla ya kung’olewa katika nafasi hiyo alisema katika mazingira ya sasa hawezi kuzungumzia fedha zinazodaiwa kuingizwa katika akaunti yake, hadi pale wenye mamlaka zitakapotekeleza maazimio ya Bunge.
Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Usajili wa Vizazi na Vifo (Rita), Philip Saliboko alisema anasubiri uchunguzi ufanyike ili kubaini ukweli juu ya kuhusishwa na mgawo wa Sh40.4 milioni zilizochotwa kutoka akaunti hiyo.
“Unataka nizungumze nini sasa? Taarifa zimesomwa na kutangazwa, tusubiri huo uchunguzi unaotakiwa kufanyika,” alisema.
Jaji Mkuu agoma
Akizungumza baada ya mkutano wa viongozi wa Mahakama na vyombo vya habari uliofanyika Dar es Salaam jana, Jaji Mkuu Chande alisema: “Mambo hayo yameshajadiliwa na hapa tulipo si mahala pake.”
Aliombwa kutoa kauli yake kuhusu baadhi ya majaji kuhusishwa na kashfa ya hiyo na kile kilichoelezwa kuwa kuingiliana kwa mihimili ya Bunge na Mahakama katika kushughulikia suala hilo.
Hata hivyo, mmoja wa maofisa wa Mahakama aliyekuwapo eneo hilo, alisema suala majaji wanaotuhumiwa linanasubiri kuundwa kwa tume ya kijaji kama ilivyoelekezwa na Bunge.
Majaji hao waliotajwa ni Aloysius Mujulizi na Profesa Eudes Ruhangisa ambao wanadaiwa kuhamishiwa fedha kutoka kwa akaunti ya mmojawapo wa watuhumiwa iliyopo Benki ya Mkombozi. Hadi sasa majaji hao hawajatoa maelezo yoyote kuhusu suala hilo.
Stanbic yakana
Benki ya Stanbic jana ilitoa taarifa kwa umma ikisema haihusiki na sakata hilo na kwamba imekuwa ikifuata sheria na kanuni za kifedha katika utendaji wake.
“Tunapenda kuwahakikishia wateja wetu kwamba Benki ya Stanbic siku zote inafuata masharti yote na pamoja na sheria za maadili zilizowekwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” ilisema taarifa hiyo.
Benki ya Mkombozi inayomilikiwa na Kanisa Katoliki ilishatoa taarifa ikikanusha kuhusika kutakatisha fedha chafu.
“Benki inawataarifu wateja wake na Watanzania kwa ujumla kutoyumbishwa na tuhuma hizo ambazo hazina ukweli ndani yake na badala yake waitumie benki yao kwa shughuli za maendeleo ya nchi yetu,” ilisema taarifa hiyo.
Msemaji wa BoT, Lwaga Mwambane alisema tuhuma dhidi ya benki hizo zinafanyiwa kazi na Kitengo cha Intelijensia ya Fedha (FIU) kilichopo chini ya Wizara ya Fedha.
Masele ajigamba
Naye Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Steven Masele amejigamba kuwa tuhuma zilizokuwa zikielekezwa kwake kuhusu sakata hilo ni kama kumpiga chura teke na kumwongezea mwendo.
Akihutubia mkutano wa uzinduzi wa kampeni za Serikali za Mitaa mjini Shinyanga juzi, Masele alisema aliokolewa kutoka kwenye mto uliojaa mamba na kusema wabaya wake walijua tayari wamemwangamiza na kwamba kupona kwake kumempa nguvu ya kufanya kazi kwa bidii ili kuleta mabadiliko katika jimbo lake la Msalala.
SOMA ZAIDI >>> »

Monday, December 1, 2014

SAKATA LA ESCROW: TAARIFA KWA UMMA KUTOKA BENKI YA MKOMBOZI


Utangulizi: 
Taarifa hii inatolewa kwa umma kutokana na ripoti mbalimbali zilizotolewa na baadhi ya vyombo vya habari mitandao ya kijamii na taarifa iliyotolewa kwenye mjadala katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

1. Ufunguzi wa akaunti ya VIP engineering and Marketing (VIP)

Kampuni ya VIP engineering and Marketing ni kampuni ambayo imesajiliwa kwa mujibu wa sheria za Tanzania. Kampuni hii ilifungua akaunti katika benki ya biashara ya Mkombozi na hivyo kuwa moja kati ya wateja wa benki. Benki ilijiridhisha na ilizingatia taratibu zote za ufunguzi wa akaunti husika kwa kuzingatia sheria za nchi na kanuni zinazozitaka benki kupata nyaraka muhimu kutoka kwa mteja wakati wa ufunguzi wa akaunti hiyo.

Nyaraka hizo ni pamoja na kuwepo kwa cheti cha usajili wa kampuni, kanuni za kampuni, idhinisho la kampuni kumruhusu moja kati ya wanahisa wake kuendesha akaunti pamoja na picha na hati ya kusafiria ya mhusika wa kuendesha akaunti hiyo.

2.0 Mauzo ya hisa za VIP

Kampuni ya VIP ilileta mkataba kwenye benki ya Mkombozi wa mauziano ya hisa za asilimia 30 baina ya VIP na kampuni ya Pan Africa Power Solutions (PAP) ambazo inamiliki katika kampuni ya IPTL. Mkataba huo ulisainiwa tarehe 19 Ogasti, 2013. Bei ya asilimia 30 ya hisa hizo ilikuwa ni dola za Marekani milioni 75. Katika kifungu namba 2.4 cha mkataba wao kinaelekeza fedha za mauzo ya hisa zilipwe kwenye akaunti ya VIP iliyopo benki ya Mkombozi. Mkataba huo wa mauziano ya hisa baina ya kampuni hizi mbili ulitambuliwa na hukumu ya Mahakama Kuu ya Tanzania iliyotolewa na Jaji J.H.K Utamwa tarehe 5 Septemba, 2013.

3. Mchakato wa kulipa kodi ya serikali

Benki ilitambua kwamba katika mauziano hayo ya hisa ni lazima kodi ya Serikali ilipwe na hivyo iliizishauri pande zote mbili kupeleka mkataba husika katika ofisi za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ili kufanyiwa makadirio ya kodi husika. Tarehe 20 Januari, 2014 TRA iliiandikia barua kampuni ya VIP na nakala ya barua hiyo kuletwa kwenye benki ya Mkombozi. Katika barua hiyo TRA iliitaarifu kampuni ya VIP kuwa makadirio ya kodi yatokanayo na mauzo ya hisa ni shilingi 38,186,584,322.00 ikiwa ni kodi ya mauzo ya hisa ya asilimia 30 za mauzo ya hisa kutoka VIP kwenda kwa PAP.(Capital gains and stamp duty).

TRA pia iliiagiza benki ya Mkombozi kuhakikisha kuwa inalipa kodi hiyo kwa niaba ya VIP mara tu fedha zitakapoingia kwenye akaunti yake. Malipo ya kodi ya shilingi 38,186,584,322.00 yalilipwa TRA kwenye akaunti 11120100 iliyopo katika Benki Kuu ya Tanzania na TRA ilikiri kupokea kodi hiyo kwa barua yake yenye kumbukumbu namba 3-4/100/100/223/4 ya tarehe 24 Januari, 2014.

4. Ufafanuzi wa mambo mbalimbali.

4.1 Benki ya mkombozi kuhusika katika kusafisha fedha chafu

Fedha zote zilizoingizwa kwenye akaunti ya VIP iliyopo kwenye benki ya Mkombozi zilitokana na mauziano ya hisa kati ya VIP na PAP kwa mkataba uliotambuliwa na Mahakama Kuu ya Tanzania. Chanzo cha malipo hayo ni kuhamisha fedha kutoka kwenye akaunti ya PAP iliyopo katika benki ya Stanbic na kuingizwa kwenye akaunti ya VIP iliyopo katika benki ya Mkombozi.

Fedha hizo zilihamishwa katika mafungu mawili. Fungu la kwanza ilikuwa ni shilingi 73,573,500,000.00 zilihamishwa kwa njia ya TISS kwa kumbukumbu namba 000000050720 ya tarehe 23 Januari, 2014 na fungu la pili ni dola za Kimarekani 22,000,000.00 zilihamishwa kwa TISS kwa kumbukumbu namba000000050812 ya tarehe 23 Januari, 2014. Malipo mengine ya asilimia kumi ya mauzo ya hisa yalilipwa kwenye akaunti ya Mkombozi iliyopo Benki Kuu ya Tanzania. Kutokana na mchakato huo benki ya Mkombozi ilijiridhisha kuwa fedha hizo ni malipo halali na siyo fedha chafu.

Benki ya Mkombozi haijihusishi na utakasishaji wa fedha chafu na haramu katika uchumi wa Tanzania.

4.2 Malipo yatokanayo na akaunti ya VIP

Malipo toka kwenye akaunti ya mteja hufanywa kutokana na maelekezo ya mteja. Benki ikishajiridhisha kuwa fedha ya mteja ni halali na ipo kwa mujibu wa sheria na hamna zuio lolote toka katika mahakama hapa nchini hutekeleza malipo kwenye akaunti ya mteja kutokana na maelekezo yake.

Benki ilijiridhisha kuwa malipo yote yaliyofanywa kutoka kwenye akaunti ya VIP ni halali kwa kuwa chanzo cha pesa hizo ilikuwa ni halali kutokana na mauzo ya hisa na ulipwaji wa kodi ya Serikali kama ilinyoelezwa hapo juu. Kutokana na sababu hiyo benki haikuwa na shaka juu ya malipo hayo.

4.3 Malipo taslimu kwa wateja na kubeba fedha kwenye viroba, mifuko ya rambo na magunia.

Benki inatoa tamko kuwa malipo yote yaliyofanywa katika akaunti ya VIP yalilipwa kupitia akaunti za walipwaji. Hakuna fedha zilizolipwa taslimu kwa wateja na kubebwa kwenye viroba au magunia kama ilivyoripotiwa Bungeni. Pesa iliyotoka kwenye akaunti ya VIP tarehe 6 Februari, 2014 kiasi cha shilingi 3,314,850,000.00 ililipwa kwenye akaunti nane za wateja tofauti na siyo kubebwa kwenye viroba au magunia.

Na zile zilizotoka toka benki ya Stanbic zilizotajwa hapo juu zilitumwa kwa njia ya TISS na siyo kubeba kwenye magunia au viroba.

4.4 Malipo kwa mfanyakazi wa benki ya Mkombozi

Gazeti la Mawio la tarehe 20-26, Novemba, 2014 tolea namba 0122 liliandika kuwa mwanasheria wa benki ya Mkombozi ajulikanaye kwa jina la Rweyengeza Alfred alipokea malipo toka akaunti ya VIP ya shilingi milioni 40.2.

Benki inatoa tamko kuwa haina mfanyakazi anayetambuliwa kwa jina hilo na wala hakuna mfanyakazi yeyote wa benki aliyelipwa fedha toka kwenye akaunti ya VIP.

Wito kwa umma.

Benki ya Mkombozi inachukua fursa hii kuwatarifu wateja wake na umma kutopotoshwa na taarifa au tuhumma zilizofafanuliwa hapo juu na kuwataka wateja wake wote kutokuwa na hofu yeyote kwani benki ipo imara na inafanya kazi kwa kufuata misingi ya sheria, taratibu na kanuni zilizowekwa na Benki Kuu ya Tanzania. Benki inawataarifu wateja wake na Watanzania kwa ujumla kutoyumbishwa na tuhumma hizo ambazo hazina ukweli ndani yake na badala yake waitumie benki yao kwa shughuli za maendeleo ya nchi yetu.

Pamoja tunajenga nchi na uchumi wa nchi yetu.

Hitimisho

Benki ya biashara ya Mkombozi haijihusishi na haitajihusisha na utakasishaji wa fedha chafu.

Imetolewa na:

MKURUGENZI MTENDAJI BENKI YA BIASHARA YA MKOMBOZI
SOMA ZAIDI >>> »

Friday, November 28, 2014

JERRYSON TEGETE AFUNGUKA KUHUSIANA NA SAKATA AKAUNTI YA TEGETA ESCROW

KILA unapokatiza kwenye mitaa habari ni juu ya sakata la fedha za Escrow, kila mtu anazungumza lake, lakini hiki kilichosemwa na straika wa Yanga, Jerryson Tegete, mmmh!

Tegete amesema kuwa wahusika wote walioiba mabilioni ya fedha za mradi wa umeme, wanatakiwa kunyongwa kwa sababu imekuwa mazoea yao kuiba fedha za wananchi.

Sakata hilo limekolea hasa baada ya juzi Kamati ya Hesabu za Serikali na Mashirika ya Umma (Pac) chini ya mwenyekiti wake, Zitto Kabwe, kumtaka Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, mawaziri na viongozi wengine kuwajibika kutokana na kashfa hiyo.
“Hali inayoendelea sasa katika nchi yetu inasikitisha kwa sababu bado Watanzania wengi wanaishi katika maisha magumu kutokana na kodi kuwa kubwa, uchumi wenyewe unazidi kudidimia kila kukicha lakini cha kushangaza, viongozi ambao tunawategemea ndiyo wamegeuka kuwa wezi wa mabilioni ya fedha."

Fedha hizo zingeweza kusaidia wananchi kupata huduma muhimu kama elimu, maji na umeme.

 “Nadhani hatua nzuri ambayo inapaswa kuchukuliwa kwa sababu imekuwa kawaida kwa viongozi kufanya mambo kama hayo ni kunyongwa kwani itasaidia kuwafanya wengine waogope kufanya kama hivyo kwani mambo hayo yanaturudisha nyuma katika maendeleo ya nchi,” alisema Tegete.

Alipoulizwa Rais wa Simba, Evans Aveva juu ya suala hilo alifunguka: “Hayo mambo ni makubwa mno kwani hadi waziri mkuu yumo, mpira na siasa ni vitu viwili tofauti, hivyo siwezi kusema chochote. Nina imani sheria itafuata mkondo.”

Upande wa Katibu Mkuu wa Klabu ya Yanga, Beno Njovu, alishikwa na kigugumizi na kusema: “Mimi naangalia familia yangu jamani, watoto bado wadogo sana na wananihitaji. Sitaki kuzungumzia hizo habari. Escrow ina mambo mengi sana.
SOMA ZAIDI >>> »

Wednesday, November 26, 2014

RIPOTI YA SAKATA LA KASHFA YA WIZI WA FEDHA KWENYE AKAUNTI YA ESCROW YAWEKWA WAZI

Ripoti ya kashfa ya fedha zilizochotwa kwenye Akaunti ya Tegeta Escrow zaidi ya Shilingi Bilioni 300 kutoka Benki Kuu (BoT), imewasilishwa Bungeni mjini Dodoma hii leo na kusomwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) Zitto Kabwe na Makamu wake Deo Filikunjombe kusoma mapendekezo ya Kamati hiyo dhidi ya wote waliotajwa katika sakata hilo.
Katika mapendekezo yake miongoni mwa viongozi wa juu wa Serikali waliotolewa maamuzi kuwa wajiuzulu nyadhifa zao za kuteuliwa na kuchaguliwa ni pamoja na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, waziri wa Nishati na Madini, Prof. Sospeter Muhongo, Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Katibu Mkuu wa Nishati na Madini, Elaichim Maswi.
SOMA ZAIDI >>> »