Pages

Showing posts with label Zitto Kabwe. Show all posts
Showing posts with label Zitto Kabwe. Show all posts

Monday, March 23, 2015

SABABU ZA ZITTO KUIHAMA CHADEMA NA KUHAMIA ACT



Aliyekuwa Mbunge wa Kigoma Kaskazini kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Zitto Kabwe, amesema atafanya kazi kukijenga chama  cha Alliance for Change and Transparency (ACT-Tanzania) kwa kukipaisha kama alivyofanya kazi akiwa ndani ya Chadema.
 
Amesema akiwa kiongozi Chadema kwa miaka zaidi ya 20 alifanya kazi ya kukijenga chama na kuhakikisha kinatoka kuwa na wabunge wanne na sasa kimepanda na kuwa na wabunge 48.
 
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Zitto alizitaja sababu tano zilizomfanya ajiunge na ACT-Tanzania ikiwamo kuvutiwa na msingi mama wa chama hicho wa kuweka mbele masilahi ya Taifa.
 
“Nataka kuwakumbusha wakati napewa uongozi huko nyuma nilishiriki kujenga chama ambacho kina wabunge wanne tu na kuna wakati tukienda kwenye mikutano tunakuta watu 20, lakini tulifikisha hadi wabunge 48.
 
“Na mimi ni mchapa kazi na sasa nimeamua kuingia kufyeka pori na nitalifyeka pori na tukikutana Novemba tutakuwa na majibu ya maneno yangu…,” alisema Zitto.
 
Akizitaja sababu tano za kujiunga na ACT-Tanzania alisema katu hatorudi nyumba kupambana kwa ajili ya rasilimali za Taifa na watu wake ikiwa ni pamoja na kuhakikisha nchi inakuwa katika misingi ya uadilifu na uwajibikaji kwa umma.
 
“Nimekuwa nikipigania uzalendo kwa nchi yangu tangu nilipoanza siasa na nimekuwa nikiweka mbele masilahi ya Taifa dhidi ya kitu kingine chochote,” alisema Zitto.
 
Sababu ya pili unatokana na chama hicho kuwa pekee kinachokubaliana na itikadi ya ujamaa na kinaamini katika falsafa ya Nyerere iliyo na lengo la kurudisha nchi katika misingi iliyoasisi taifa.
 
Kutokana na hali hiyo, Zitto alisema anaamini kuwa ACT itasimama katika misingi ya uadilifu na kimeweka miiko na maadili ya viongozi katika kuhakikisha viongozi wa chama hicho wanatakiwa kukubaliana nayo kwa kusaini.
 
Katika miaka yangu ya ubunge nimekuwa nikipigania uwajibikaji na uwazi jambo ambalo ninaliamini kwa moyo wangu kwenye utumishi wangu kwa umma.
 
“Nimefurahi kwamba kati ya misingi 10 ya ACT, uwajibikaji na uwazi ni misingi ambayo naamini inatokana na utumishi wa umma na suala la uwazi limekuwa sehemu ya jina la chama hicho hivyo kwangu ACT ni nyumbani katika siasa na katika utumishi wa umma,” alisema Zitto.
 
Zitto alisema amejiunga ACT kwa sababu amekubaliana na imani yao ya kujitegemea, bidii, umakini na weledi katika kazi kuwa ndiyo msingi wa maendeleo.
 
Sababu nyingine aliyotoa ni kukubaliana na imani ya ACT kwamba umoja ni ngao muhimu katika ujenzi wa taifa na Afrika kwa ujumla.
 
Alisema kwa sababu hiyo ameona upo umuhimu wa kurudisha nchi katika misingi iliyoliasisi taifa.
 
“Lazima tuirudishe nchi katika heshima ya uongozi wa Bara la Afrika hivyo naahidi kufanya kazi na makundi yote, wanaoamini katika siasa safi na siasa za hoja, tunataka kufungua kurasa mpya wa siasa nchini."
 
Usaliti
Akizungumzia kuhusu wanaomtuhumu kufanya usaliti, Zitto alijibu kwa kutumia nukuu za Rais wa kwanza wa Ghana, Kwame Nkurumah akisema haangalii nyuma tena bali anaangalia mbele.
 
“Naombeni mjaribu kufumba macho yenu mjiulize ni mbunge gani katika Bunge hili ambaye ametoa hoja ambazo zilikitikisa Chama Cha Mapinduzi (CCM).
 
“Mara mbili nimetoa hoja ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu, taarifa yangu wakati ule nikiwa Mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC), mara mbili nimeng’oa mawaziri wa CCM, mwaka 2011 mawaziri wanane.
 
“Juzi juzi katika suala la Escrow nimewang’oa mawaziri watatu na Mwanasheria Mkuu wa Serikali hivyo, swali kama hilo la usaliti lilitakiwa kupewa wale ambao wako bungeni na hawafanyi kazi ya kuiwajibisha serikali si kwa mtu ambaye maisha yake yote ya ubunge amefanya kazi ya kuiwajibisha serikali,” alisema.
 
Mafao  Yake
Alipotakiwa kuelezea kuhusu masilahi yake ya ubunge, Zitto alisema kwake masuala ya fedha halina nafasi kwa sababu yupo kwa sababu ya kusimamia masilahi ya Watanzania.
 
“Tangu mwaka 2011 nimekuwa mbunge pekee ambaye nimekuwa sipokei posho ya Bunge hadi naondoka bungeni kwa hivyo basi uamuzi wangu wa siasa hauangalii fedha bali hoja kwangu ni kuona tunapoelekea,” alisema.
 
Vigogo wajiunga
Wakati wa mkutano huo Zitto jana, chama hicho cha ACT-Tanzania, kilivuna wanachama wapya zaidi ya 10 wakiwamo waliokuwa viongozi wa Chadema katika ngazi ya mikoa na wilaya.
 
Waliojiunga na chama hicho ni pamoja na aliyekuwa mgombea ubunge wa kura za maoni CCM katika jimbo la Kasulu Mjini, Askofu Dk. Gerald Mpango, Mwenyekiti wa Kamati ya Sheria na Haki za Binadamu Kanda ya Magharibi Chadema, Jaji Mstaafu Mussa Kwikima.
 
Mwingine ni Kansa Mbarouk aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Tabora, Jorum Mbogo aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema Wilaya ya Kaliua, mgombea ubunge wa jimbo la Temeke mwaka 2010 Chadema, Dickson Ng’ili.
 
Wengine ni Meck Mzirai aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Tabora na Mjumbe wa Kamati Kuu, Charles Lubala Mwenyekiti wa jimbo la Kahama na mgombea ubunge 2010 Chadema na Diwani wa Mabogini Halmashauri ya Moshi, Albert Msando (Chadema).
 
Pia wamo Dk. Ben Kapwani aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Iringa, John Malaki Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Katavi, Mwasimtwa Mwagongo, Kaimu Mwenyekiti wa TLP Wilaya ya Mbarali na Katibu wa TLP Wilaya ya Mbarali, Selemani Nyumile.
  
Wabunge 10  Kujiunga  na  ACT
Akizungumza na Mwandishi  wetu  jana jijini Dar es Salaam, baada ya kuzungumza na waandishi wa habari, Zitto alisema nyuma yake wapo wabunge zaidi ya 10, watakaojiunga na ACT muda sio mrefu.
 
“Siko mwenyewe wapo wenye mapenzi mema na tunataka kufungua ukurasa mpya kwa nchi yetu wa siasa za kujenga nchi, wabunge mahiri wa CCM na Chadema zaidi ya 10, watajiunga nami, ila sitakutajia majina kwa sasa kwa sababu ya sheria za vyama vyao, acha wamalizie vipindi vyao vya ubunge,” alisema Zitto
SOMA ZAIDI >>> »

Friday, March 20, 2015

HOTUBA YA ZITTO KABWE ALIYOTAKA KUITOA JANA BUNGENI MJINI DODOMA


Mheshimiwa Spika, nilijiunga na Bunge lako tukufu mwaka 2005 nikiwa kijana mdogo mwenye malengo ya kupaza sauti ya vijana kwenye masuala yanayohusu nchi yetu na pia kutetea maslahi ya wananchi wa Jimbo la Kigoma Kaskazini na Mkoa wa Kigoma.
Katika kudumu kwangu kama mbunge nililelewa na kukuzwa na chama cha siasa cha CHADEMA ambacho kupitia chama hiki niliingia Bungeni. Chama hiki kilinilea na kunikuza tangu nikiwa na umri wa miaka 16 na kupitia chama hiki nimejifunza mambo mengi sana. Nimeijua nchi yangu, nimejua siasa na nimejulikana ndani na nje ya nchi. Nitakuwa mwizi wa fadhila nisipotoa shukrani zangu za dhati kabisa kwa CHADEMA na viongozi ambao nimefanya nao kazi muda wote nikiwa mwanachama na kiongozi.
Mheshimiwa Spika, Chama kilinikuza kama mwanasiasa lakini watu wa Kigoma Kaskazini ndio walionipa kiti hiki ninachokalia kama Mbunge. Juzi nilipokuwa nyumbani nilipata fursa ya kuwashukuru rasmi wananchi kwa imani waliyonipa kuwatumikia kwa vipindi viwili mfululizo. Wengi wenu ndugu zangu wabunge mnafahamu, mihula miwili sio jambo la mchezo, sio lelemama. Mola atawalipa wananchi wa Kigoma kwa imani kubwa walioionyesha kwangu na kuniwezesha kulitumikia Taifa langu kwa namna nilivyolitumikia.
Mheshimiwa Spika, nachukua fursa hii leo kuzungumzia suala la muda mrefu sasa la kutoelewana kati yangu na chama changu na hivyo kuleta msuguano kati ya wananchi walionichagua kuwawakilisha na chama nilichopitia na kupeperusha bendera yake wakati wa uchaguzi mkuu. Licha ya msimamo wangu wa siku zote kwamba wananchi pekee waliomchagua mwakilishi wao ndio wawe na mamlaka ya kumwondoa kwenye uwakilishi mchaguliwa huyo, mfumo wetu wa kikatiba na mfumo wetu wa kisiasa haupo hivyo na umeamua vinginevyo.
Mheshimiwa Spika, kwamba chama cha siasa kinaweza kumvua uanachama mwanachama wake na hivyo kupoteza kiti chake cha uwakilishi wa wananchi wake ni moja ya makosa makubwa ya kikatiba ambayo tumeendelea kuyakumbatia, nimekuwa nikipinga na nitaendelea kupinga udikteta wa vyama dhidi ya utashi wa wananchi.
Mheshimiwa Spika, licha ya upinzani wangu mkali wa vifungu kandamizi vya kikatiba, kama mzalendo ninaiheshimu Katiba yetu na mfumo wetu wa sasa na ninaheshimu uamuzi wa mahakama dhidi ya kesi yangu na sitakata rufaa. Hatua itakayofuata ni uamuzi wa chama changu na baadhi ya viongozi wameshatangaza kwa umma kupitia vyombo vya habari kunivua uanachama ingawa sijapewa taarifa rasmi.
Mheshimiwa Spika, ningeweza kukata rufaa kuhusu maamuzi ya mahakama kwani kuna sababu lukuki ya kushinda rufaa hiyo. Lakini ninadhani nimepigania haki zangu kwa muda mrefu sasa. Nimepigania kupanua wigo wa demokrasia ndani ya chama changu kwa muda mrefu sasa. Lakini ugomvi huu hauna manufaa kwa pande zote husika, kwa hakika unatuumiza wote. Mimi ni mwanademokrasia. Naamini katika siasa za ushindani ndani ya chama na katika mfumo mzima wa siasa kitaifa. Lakini sitakuwa tayari kudhoofisha harakati na kazi kubwa walizofanya wanamageuzi waliotutangulia kwa kuendeleza ugomvi unaotuumiza. Hivyo niko tayari kukubali kukaa pembeni. Ninaamini kuwa mapambano ya kuleta mabadiliko ya kweli na demokrasia katika nchi yetu Tanzania ni makubwa kuliko mimi, kuliko kiongozi yoyote wa Chadema na kuliko wanachama wa Chadema. Mapambano haya ya mabadiliko si kwa ajili ya kizazi hiki tu bali kwa vizazi vijavyo. Ndiyo maana siku zote nimesema Nchi kwanza, vyama baadae. Kuona makundi yanajitokeza ndani ya harakati hizi, na kuwa na uhasama mkubwa uliopindukia, unawakatisha tamaa wananchi wanaotutumaini kuleta siasa iliyo tofauti na siasa za sasa. Muda umefika wa kupiga mstari na kuanza upya. Hivyo nimeamua kuwa nitatii maamuzi ya chama ya kunivua uanachama na kung’atuka ubunge.
Mheshimiwa Spika, naomba niweke wazi kuwa nimefikia uamuzi huu kwa utashi wangu mwenyewe na nimepewa Baraka zote na wananchi wangu na wazee wa Jimbo la Kigoma Kaskazini. Najua Watanzania wengi ambao nimewatumikia kwa moyo wangu wote katika kipindi cha miaka hii 10 wanaweza wasikubaliane na uamuzi huu. Hata hivyo Watanzania wajue kuwa mfumo wetu wa siasa na katiba unatoa nguvu kwa vyama vya siasa kudhibiti wabunge wake. Naamua hivi kwa sababu wenzangu ndani ya chama ambao nimehangaika nao usiku na mchana kujenga chama na kukifisha hapa kilipo hawapo tayari kufanya kazi tena na mimi. Nimesoma na kusikia kauli nyingi zinazoweka wazi kuwa hawanitaki ndani ya chama. Nimejitahidi kwa njia zangu zote kuona kama tunaweza kuendelea kufanya kazi pamoja ya kujenga mfumo madhubuti wa vyama vingi nchini lakini imekuwa ngumu kama mwanachama mwenzao. Ninaheshimu uamuzi wao huo.
Mheshimiwa Spika, kwa miaka kumi hii si yote niliyafanya sahihi, yapo ambayo niliyakosea kama mwanadamu katika kufanya kazi kwangu, kwa namna yeyote ile naomba radhi Watanzania wote kwa yote ambayo sikuyafanya kwa usahihi. Mimi ni binadamu, kiumbe dhaifu, sijakamilika. Ni Mola peke yake amekamilika.
Mheshimiwa Spika, siwezi kuanza maisha yangu mapya bila ya kulishukuru Bunge lako tukufu, Bunge la Tisa chini ya Mzee Samwel Sitta na Bunge la Kumi chini yako Mama Anna Simamba Makinda. Bunge limekuwa ni nyumbani kwangu kwa takribani muongo mmoja. Nimekuzwa, nimejifunza, nimepambana, nimefurahi na nimelia ndani ya Bunge hili. Kwa pamoja tumepigania maslahi ya wananchi wetu na kupingana na kufanya mambo kwa mazoea na hivyo kuleta mabadiliko kadhaa. Ni kipindi hiki ambapo wabunge tumekuwa na sauti, Bunge la Tisa lilijenga ‘Bunge lenye Meno’ katika kupambana na ufisadi. Bunge la Kumi limejenga ‘Bunge lenye nguvu’ katika mfumo wa Bajeti ya nchi yetu. Kupitia Bunge hili tumeweka misingi ya kujenga mfumo madhubuti wa uwajibikaji katika nchi yetu.
Mheshimiwa Spika, wakati Bunge la Tisa litakumbukwa kwa hoja ya Buzwagi iliyopelekea nchi yetu kufanya mabadiliko makubwa katika mfumo wa uendeshaji wa sekta ya madini (Sera mpya ya Madini na Sheria mpya ya Madini ) na hivyo mapato ya sekta ya madini kuongezeka kutoka Tshs 32 bilioni kwa mwaka mpaka Tshs 450 bilioni kwa mwaka hivi sasa; Bunge la Kumi litakumbukwa kwa hoja maalumu ya Tegeta Escrow iliyopelekea mfumo wetu wa maadili ya Viongozi kupitia Baraza la Maadili kuanza kufanya kazi kwa namna ambayo haijawahi kushuhudiwa katika miaka iliyopita. Mimi kuwa sehemu ya mabunge yaliyotekeleza hatua hizo za mabadiliko ni jambo la kujivunia sana.
Mheshimiwa Spika, kwa familia yangu, wajumbe wa PAC, tumekuwa nguzo kubwa ya kujenga uwajibikaji wa Serikali kwa Bunge na wananchi. Napenda kuwashukuru kwa dhati kabisa kwa kuniunga mkono na kwa kunipa ushirikiano kama Mwenyekiti wao. Changamoto na malezi mliyonipa kwa miaka yote hii yamejenga Mtanzania mmoja mwenye dhati ya kuitumikia nchi yake, muda wowote, wakati wowote na kwa namna yeyote ile bila woga wala upendeleo. Nawashukuru kwa kujitoa kwenu kwa nchi yetu na dhamira isiyo na mawaa ya kujenga Taifa imara zaidi.
Nitaendelea kuwatumikia wananchi wa Kigoma Kaskazini na Taifa langu hata kama nimelazimika kuachia nafasi yangu ya ubunge kwa kipindi hiki kilichosalia kwa kusimamia ukweli, kutetea demokrasia ya kweli na kupigania maendeleo ya kweli kwa mwananchi wa kawaida bila ubaguzi wowote.
Mheshimiwa Spika, Kwa CHADEMA, licha ya tofauti zetu ambazo zimekua kiwango cha kutosameheka, najivunia kwa fursa mliyonipa kuwa sehemu ya Baraza hili la Taifa ambalo leo ninalihutubia kwa mara ya mwisho kama mbunge wa Kigoma Kaskazini. Fursa iliyonifanya niweze kuitumikia nchi yangu na mkoa wangu wa Kigoma. Inawezekana tusiweze kuelewana katika masuala ya uongozi, misingi na itikadi, lakini ninaamini tunapaswa kuelewana na kukubaliana katika kubwa ya kuijenga nchi yetu kuwa Taifa linalojitegemea na lisilo na aina yeyote ya ubaguzi. Taifa lenye uchumi shirikishi wenye kuzalisha ajira na kuondoa umasikini, ujinga na maradhi, Taifa la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Na ni matumaini yangu kuwa tutakuwa bega kwa bega katika harakati hizi katika siku zijazo. Yaliyopita si ndwele tugange yajayo, nafasi hii ya kihistoria tuliyopewa haihitaji siasa za ubinafsi na unafsi! Uzalendo wetu utapimwa kwa uwezo wetu wa kuweka tofauti zetu binafsi pembeni kwa lengo lililo kubwa zaidi yetu.
Mheshimiwa Spika, Mwisho kwa wananchi wa Jimbo langu, wana Kigoma na raia wote wa Tanzania ambao kwa ridhaa yao nimekaa katika viti hivi kwa miaka takribani kumi, nawahakikishia kuwa dhamira yangu kuwatumikia, nia yangu na sababu za kutoa utumishi wangu kwenu vimekuwa na nguvu zaidi kuliko wakati mwingine wowote ule. Huu ni mwanzo mpya. Ngugi aliandika ‘a grain of wheat’ kwa maana ya kwamba ‘Ili Mbegu iweze kumea lazima ife kwanza’.
Asanteni sana.
SOMA ZAIDI >>> »

Saturday, March 14, 2015

ZITTO KABWE APOKELEWA KAMA SHUJAA JIMBONI KWAKE

 
Mh zitto kabwe baada ya chama chake cha CHADEMA kutangaza kumfukuza uanachama ndani ya chama hicho ameamua kufanya ziara ya siku tatu ndani ya kigoma kuzumgumza na wananchi wake juu ya hali ya kisiasa inayomkabili kwa sasa,hizi hapa ni baadhi picha za mapokezi yake kigoma 

Ikiwa bado sakata la kufukuzwa uanachama kwa mbunge wa kigoma kaskazini (CHADEMA) mh ZITTO KABWE linaendelea kuchukua nafasi katika vichwa vya watanzania na wapenda siasa,mbunge huyo ameanza kufanya ziara ya siku tatu jimboni kwake kuzungumza na watanzania mbalimbali.
Akiwa katika ziara yake MBUNGE wa Kigoma Kaskazini,Zitto Kabwe(Chadema),amewataka wakazi wa mkoa wa kigoma wasisikitishwe na mambo yanayomkabili kwa sasa kwa kile alichoeleza kuwa asilimia kubwa ya wanasiasa makini walishapitia misuko suko kama yake.
Amewaeleza kuwa jambo la msingi ni kumuunga mkono katika hatua yoyote atakayochukua kwa ajili ya wanakigoma na Taifa kwa ujumla katika kumaliza mgogoro uliopo baina ya Chama chake na yeyeZitto ametoa kauli hiyo leo mjini Kigoma alipokutana na viongozi 250 kwenye mkutano wa ndani uliohusisha viongozi kutoka katika kila kijiji kwenye jimbo la Kigoma kaskazini yenye jumla ya vijiji 45.Aliwataja baadhi ya wanasiasa waliopita katika hatua kama yake na baadae wakageuka washindi kuwa ni Maalim Seif Sharif Hamad(Tanzania),Mahathir Mohamed(Malaysia na Indira Gandhi wa India.“Msinililie mimi kwa kuwa haya ni mapito ya kila mwanasiasa Makini,wengi walio makini walitofautiana na vyama vyao kwa sababu ya maslahi ya mataifa yao,wapo walioanzisha vyama baada ya hali hiyo na wakashinda na wapo waliopigiwa magoti na vyama vyao baada ya kugundua walichofanya si sahihi, hivyo jukumu kubwa ni kuniunga Mkono”alisema Zitto.
Alisema mpaka sasa hajapewa taarifa yoyote ya kusitishwa kwa Ubunge wake na kama hali hiyo ikijitokeza atarudi kuwafahamisha juu ya hatua atakayochukua
Zitto yupo mjini Kigoma kwa ziara ya siku tatu,ambapo atawatembelea wakulima wa mradi wa Kahawa walio katika mfuko wa hifadhi ya Jamii(NSSF), pamoja na kukabidhi gari aina ya Ambulance katika kituo cha Afya Nyarubanda na kisha kufanya mikutano miwili ya hadhara.
Juzi Mwanasheria mkuu wa Chadema Tundu Lissu,alitangaza hadharani kuvuliwa uanachama kwa Zitto kutokana na kushindwa katika kesi aliyofungua kupinga asijadiliwe na Chama Chake
SOMA ZAIDI >>> »

Tuesday, March 10, 2015

ZITTO KABWE ABWAGWA MAHAKAMANI KWENYE KESI YAKE DHIDI YA CHADEMA


Chama  cha  Demokrasia  na  Maendeleo (CHADEMA)  kimeshinda kesi dhidi ya aliyekuwa mwanachama wake Zitto Kabwe.

Katika  hukumu  hiyo  iliyotolewa  leo  na  Jaji  Mziray,Mahakama imewaruhusu  CHADEMA kuendelea na taratibu zake  za  Awali. Aidha, Mahakama imeamuru Zitto Kabwe alipe gharama zote za kesi.

Ikumbukwe  kuwa, mwaka jana Zitto Kabwe aliweka pingamizi mahakamani kuzuia kikao cha Kamati Kuu ya  chama  hicho  kumjadili  mpaka  pale  shauri  lake  litakaposikilizwa  na  Baraza  Kuu  la  Chama  hicho.

Credits: Mpekuzi
SOMA ZAIDI >>> »

Wednesday, December 3, 2014

ZITTO AMTAMBULISHA MCHUMBA WAKE KIGOMA


MBUNGE Jimbo la Kigoma Kaskazini Zitto Zuberi Kabwe amemtambulisha mchumba wake mpya anayetarajia kufunga nae pingu za maisha hivi karibuni. Mchumba huyo
Utambulishio huo wa mchumba wa Zitto ulifanywa na Mbunge wa Kigoma Kusini David Kafulila (NCCR-Mageuzi) wakati wa sherehe ya Harusi yake iliyofanyika kwenye ukumbi wa Annex.
hali ilikuwa hivi; baada ya Kafulila kutambulisha ndugu zake pamoja na wazazi wake ndipo alianza kutambulisha wageni wengine na kuanza na mchumba mtarajiwa wa Zitto Kabwe aliyemtaja kwa jina la Anna.
“Huyu wa kwanza anaitwa Anna anafanya kazi Ubalozi wa Ireland ni mchumba mtarajiwa wa Zitto Zuberi Kabwe, anayefuata kutoka kushoto kwa Anna wote mnamfahamu ndiyo Zitto mwenyewe na anayemfuata ni Mwalimu wangu wa chuo kikuu Kitila Mkumbo na mwisho ni mbunge mwenzangu David Silinde hao ndo walio nisindikiza,” alisema Kafulila.
SOMA ZAIDI >>> »