Serikali imetumia Sh. bilioni 27 kuendesha Bunge Maalumu la Katiba lililohairishwa leo mpaka Agosti mwaka huu mjini Dodoma.
Waziri wa Fedha(pichani chini) ambaye pia ni mjumbe wa bunge hilo, Saada Mkuya Salim, aliliambia Bunge Maalumu jana.
Waziri wa Fedha, Saada Mkuya Salim
Aliwaeleza wajumbe kuwa serikali imesitisha hata kupeleke maji, umeme na huduma nyingine muhimu vijijini ili kuwezesha kuandikwa katiba hiyo.
Kadhalika imejitahidi kila wakati kuwapa wabunge stahili zao na mara nyingi wajumbe hawajacheleweshewa kupata hela zao.
Aliongeza kuwa lengo ni kutaka bunge lifanikiwe kwa sababu taifa linataka wakiondoka kipatikane kitu chenye maana.AWAANGUKIA UKAWA Akiwazungumzia wajumbe wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) waliosusia bunge hilo tangu Jumatano iliyopita alisema anasikitishwa na baadhi ya wajumbe kususia majadiliano hayo.
Alisema kuna changamoto nyingi zinazoikumba nchini na fursa ya kuandika katiba ndiyo inayostahili kutumika kuzipatia ufumbuzi.
“Kote kuna changamoto upande wa Tanzania Bara na Zanzibar zipo kwenye kutekeleza katiba na pia sheria.Lakini hazitatuliwi kwenye mikutano ya Kibanda Maiti ni hapa ndani ya ukumbi wa bunge maalumu,” alisema na kuwataka wajumbe wa Ukawa warejee mkutanoni.
“Mkutano huu jamani ni kama umekwenda kwenye majadiliano usitegemee kupata kila unachokitaka itabidi wakati mwingine ukubaliane na wenzako. Japo si wakati wote kwani unaweza kupata kile ulichokikusudia,” aliwasihi wajumbe hao.Aliongeza kuwa kutoka nje na kufanya katiba nyingine nje ya ukumbi hakulisaidii taifa.
“Kwa ajili ya kuwahurumia wananchi wetu walipa kodi wa nchi hii tutumieni fursa hii tuandike katiba na pia tujali fedha ya wananchi,” alisema Mkuya,
SERIKALI TATU
Aliendeleza wimbo kuwa muundo huo wa serikali utaongeza gharama za uendeshaji kwa vile kila mwaka bajeti ya serikali haitoshi kuendesha hata hizi serikali mbili.
Alisema mapato ya taifa hayajaweza kukidhi haja za mahitaji moja na kila wakati anapokea simu kutoka wilayani zikiulizia fedha za maendeleo ambazo pia ni kidogo.
Alisema Watanzania wanalalamikia kuongezeka kwa matumizi ya serikali kunakoletwa na kuongeza mikoa na wilaya itakuwaje kwa kuongeza serikali ya tatu?
Aliwataka wajumbe waangalie suala la kutatua matatizo ya Muungano kwa kuongeza serikali nyingine kwani ni kitu kinacholeta hali ya ‘kusadikika’ zaidi kuliko uhalisia.
No comments:
Post a Comment