Pages

Tuesday, May 20, 2014

HOMA YA DENGUE HATIMAYE UMEINGIA MBEYA










HATIMAYE ugonjwa wa homa ya  Dengue umeripotiwa kuingia Mkoani Mbeya baada ya kupatikana kwa kesi ya mgonjwa mmoja mwanamke ambaye amelazwa katika Hospitali ya Mkoa wa Mbeya.


Mwanamke huyo ambaye ni mkazi wa Sae,  Jijini hapa, ambaye hata hivyo hakuwa tayari jina lake liandikwe gazetini  inasemekana alipata ugonjwa huo baada ya kung’atwa na  mbu aina ya Aides alipokuwa akiishi ,  Jijini Dar es salaam.


Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo, Dk. Gloria Mbwile, alithibitisha kupokelewa kwa  mgonjwa huyo na kwamba tayari hali yake imeimarika baada ya madaktari kumpatia matibabu baada ya kufikishwa hospitalini hapo.


Amesema mgonjwa huyo alifikishwa hospitalini hapo Mei 17  majira ya mchana,  huku akionesha kuwa dalili zote za ugonjwa huo


Amesema kutokana na hali hiyo madaktari walianza kuchukua hatua za haraka kwa kuchukua sampuli za vipimo kwa ajili ya kuvipeleka Dar es salaam kwa uchunguzi zaidi, wakati huo huo wakimtoa katika wodi ya wagonjwa mchanganyiko na kumpeleka ile ya binafsi.


Dk. Mbwile amesema hali ya mgonjwa huyo imeimarika baada ya kupatiwa matibabu ya kina  na kwamba hiyo jana angeweza kuruhusiwa kutokana hospitalini hapo.


Hata hivyo, Katibu wa afya Mkoa wa Mbeya, Juliana Mawalla, amewataka wananchi wa mkoa wa Mbeya kutoa hofu juu ya ugonjwa huo kwani mgonjwa huyo alipata maambukizi hayo akiwa Jijini Dar es salaam na kwamba tayari serikali imeleta vifaa kwa ajili ya vipimo katika hospitali ya mkoa na ile ya kanda ya Rufaa Mbeya.


Kwa upande wake Mama mzazi wa mgonjwa huyo, ambaye naye aliomba jina lake lihifadhiwe, amesema mwanae alifika Jijini Dar es salaam Mei mosi mwaka huu kwa ajili ya kuhudhuria sherehe ya dada yake na alikaa huko kwa siku nane.


Dengue ambayo tayari imeshaua watu watano mpaka sasa , huku wagonjwa zaidi ya 400 wakiwa wamegundulika kuambukizwa na kupatiwa matibabu ya ugonjwa huu katika mkoa wa Dar es salaam hali ambayo imeibua hofu kubwa kwa wananchi.

No comments:

Post a Comment