Pages

Monday, May 19, 2014

TAARIFA KWA UMMA KUTOKA KWA BAADHI YA WAJUMBE WA BARAZA KUU NA MKUTANO MKUU CHADEMA KUHUSU KUPINGA UKAWA




TAARIFA KWA UMMA

TAARIFA YA BAADHI YA WAJUMBE WA BARAZA KUU NA MKUTANO MKUU CHADEMA MIKOA YA DSM, PWANI NA TANGA KUPINGA UHUNI WA KISIASA UNAOITWA UKAWA.


UTANGULIZI.

Ndugu wanaHabari, Tunapenda mtusaidie kufikisha ujumbe wetu huu kwa umma unaotokana na malalamiko na manung’uniko ya wanachama wenzetu wa CHADEMA kuhusu udhaifu mkubwa wa kiuongozi unaoendelea kwa sasa chini ya mwavuli wa UKAWA.Kwa wiki kadhaa sasa, kumeibuka msamiati mpya wa kisiasa wa UKAWA uliopelekea mpaka kuundwa kwa BARAZA KIVULI LA UKAWA pale Bungeni bila kufuata Utaratibu.

Sisi viongozi ambao miongoni mwetu ni Wajumbe wa vikao halali vya chama, ambavyo ni Baraza Kuu na Mkutano mkuu wa chama kutoka mikoa ya Tanga, Pwani na DSM kwa masikitiko makubwa tunasema kuwa hatupendezeshwi na mwenendo huu wa chama unaofanywa na viongozi wetu wakuu.

KUSUSIA BUNGE LA KATIBA.

Ndugu wanaHabari,
Kwa namna ambavyo tumepambana kwa miaka mingi kudai na kuishinikiza serikali kuridhia uandikaji wa katiba mpya, ni mpumbavu pekee anayeweza kususia fursa ya uandishi huo tena kupitia chombo huru (BUNGE LA KATIBA) kwa sababu tu ya mgongano wa kimaslahi.

Tunasikitika sana kuwaona viongozi wetu na wabunge wa chama chetu cha CHADEMA wamesahau kazi tuliyowatuma ya kwenda kuandika katiba mpya yenye kuzingatia maslahi ya wananchi badala yake wamekwenda kupigania vyeo.

Tumefedheheshwa sana na namna ambavyo wawakilishi hawa wamekubali kutanguliza mbele maslahi yao na kuyaacha maslahi ya wananchi ambao ndio waliuowatuma, kwenye Rasimu yenye sura zaidi ya 18 ni uzezeta kususia sura 2 tu za mwanzo kisa tu maslahi yao ya kugawana vyeo wanaona hayawezi kutekelezeka.

Tunaomba ifahamike kwamba, hakujawahi kukaliwa kikao chochote halali cha chama chetu kilichoazimia na kuwaagiza wajumbe wanaotokana na chama chetu wasimamie katiba yenye SERIKALI TATU, na ikionekana haiwezekaniki WASUSE NA KUTOKA NJE YA BUNGE.

Huu ni udhaifu unaotawaliwa na uroho wa madaraka, sisi kama viongozi halali wa kikatiba wa chama hatujawahi kuwaza wala kuamua kuhusu ujinga huu, siku zote tumekuwa tukiwasisitiza wajumbe wetu kwenye fursa yoyote watakayoipata kwenda kusimamia mawazo na misimamo ya wananchi ambao ni wanyonge.

Tunawatuma wajumbe wetu kuhakikisha tunapata katiba itakayosimamia na kuzitunza Rasilimali zetu, na wala si kweli kuwa Idadi ya Serikali kama ni 3 au 2 au 5 au zozote inaweza kuwa muarobaini wa changamoto zetu.

Daima dumu tumekuwa tukiamini kwenye mapambano ya Hoja ambayo ndio msingi mkuu wa demokrasia ya kweli Tunayoisimamia kama CHADEMA.

Hivyo Basi tunasema, si sahihi hata kidogo kwa wajumbe wetu wa Bunge la katiba kususia vikao vile na ndio maana hata baadi ya wabunge wengi wa chama chetu wamekuwa wakilalamika chini chini kwetu sisi wajumbe wa baraza kuu kwamba wamechoka sasa kuburuzwa na viongozi wakuu wa chama na kwamba wao nao wana mawazo na misimamo yao, sasa kwa niaba yao pia tumeona kama viongozi wa chama ulikemehe hili.

Nipo tayari kuyataja majina ya wabunge hawa wanaolalamika kuburuzwa ambao ni zaidi ya wabunge 31 wa kuchaguliwa na wa viti maalum.

Muungano wetu huu wa UKAWA ni muungano wa kinafiki usiokuwa hata na hadidu za rejea, hakunaga muungano duniani kote ambao waunganaji wake wanaungana kiujanja ujanja tu kama walivyofanya viongozi wetu hawa. Hatuungi mkono na tunawataka wasiendelee na upuuzi wao huu, warudi bungeni kama hawataki wajitoe tuchague wabunge wengine watakaowawakilisha wananchi wanaotuamini.

Ni sawa na ndoa ya mkeka, hakuna maridhiano, hakuna vikao, asubuhi wapenzi jioni wana ndoa, ndoa ya namna hii kamwe haiwezi ikadumu hata kidogo.

BARAZA KIVULI LA UKAWA.

Tunasikitika sana na kitendo cha mwenyekiti wa CHADEMA ndugu Freeman Mbowe, kutufanya sisi wajumbe wa Baraza Kuu na Mkutano Mkuu hatuna maana kwenye kufanya maamuzi ya chama.

Walituaminisha kwamba CUF wamefunga ndoa na CCM na kwamba wao ni sehemu ya serikali hivyo hawawezi kushirikiana na chama ambacho ni sehemu ya serikali, kwa msingi huu tukaazimia kwenye vikao vya chama ambavyo ni halali kwamba chama chetu hakitashirikiana na chama kingine chochote cha siasa kwa kuwa ni washirika wa CCM na kwamba wao ni CCM-B

Tumemkashigu na kumtuhumu James Mbatia na NCCR nzima kuwa ni Tawi la CCM na ndio maana hata Mbatia ameteuliwa kuwa Mbunge, inakuwaje leo tunashirikiana na watu hawa ambao wanatumiwa na CCM?

Ni lini Muungano wa CCM na CUF umevunjika rasmi? Ni lini ushirikiano wa NCCR ya MBATIA na CCM umekufa rasmi?

Je mazingira yaliyofanya tuwahesabu wenzetu hawa kuwa ni CCM B leo yamebadilika?, na kama yamebadirika yamebadilika lini na yamebadilikaje?

Je sio kweli kwamba tuliwatenga wenzetu na kuwakashifu kwa sababu tu ya uchu wa madaraka?

Yaani sio kweli kwamba tuliwafedhehesha wenzetu hawa kwa sababu ya UWAZIRI KIVULI? Na leo tunawasafisha wenzetu hawa kwa UWAZIRI KIVULI HUO HUO.

Kwa nini viongozi wetu wanakuwa na UCHU na UROHO wa MADARAKA kiasi hiki?.

Kama tunaweza tukawaita wenzetu MASHETANI asubuhi na jioni tukawaita MALAIKA kwa sababu ya UWAZIRI KIVULI, je tukipewa nchi na kushika dola, si Tutawaita wenzetu majina mabaya zaidi?

Si tutakuwa na serikali mbovu na ya ajabu zaidi ya hivi sasa tulivyo kwenye siasa za upinzani tu tulio nao?

Kwa misingi huu, Tunaamini kuwa UKAWA ni UNAFIKI WA KISIASA, na umebuniwa kwa sababu moja tu nayo ni kugawana vyeo, hakuna sababu yoyote yenye mantiki iliyopo kwenye uundwaji wa UMOJA huu na ndio maana hauna hadidu za rejea wala hauna hati za makubaliano miongoni mwetu.

Napenda kuwaambia watanzania kuwa sisi baadhi yab wajumbe wa Baraza kuu na mkutano mkuu wa mikoa ya Pwani, Dsm na Tanga hatuungi mkono upuuzi wowote wenye lengo la kusimamia ugawanaji wa vyeo na madaraka, watu wa namna hii tunawaita WALAFI wa MADARAKA.

Tunaunga mkono watanzania wote wanaoitakia heri Tanzania yetu.

Mungu ibariki Tanzania

Imeandaliwa na Baadhi ya Wajumbe wa Baraza Kuu na Mkutano Mkuu wa Mikao ya Pwani, Dar es Salaam  na TANGA na imesomwa nami

……………………………………………………
JOSEPH YONA PATRICK
+255713802226

Mwenyekiti wa CHADEMA WILAYA YA TEMEKE
Mwenyekiti wa BAVICHA mkoa wa TEMEKE
MJUMBE WA BARAZA KUU CHADEMA TAIFA
MJUMBE WA MKUTANO MKUU CHADEMA TAIFA
MJUMBE WA KAMATI YA UTENZAJI BAVICHA TAIFA

No comments:

Post a Comment