Serikali ya Rwanda imezuia kurushwa matangazo ya Shirika la Utangazaji la Uingereza BBC kwa lugha ya 'Kinyarwanda' nchini humo, baada ya shirika hilo kurusha filamu inayokana mauaji ya kimbari yaliyotokea mwaka 1994 nchini humo.
Taarifa kutoka Kigali zinaeleza kuwa, uamuzi huo umechukuliwa baada ya shirika la BBC kutayarisha na kurusha hewani filamu hiyo iliyopewa jina la 'Rwanda's Untold Story' na kumuandama moja kwa moja Rais Paul Kagame wa nchi hiyo.
Rais Kagame amekuwa akilituhumu mara kwa mara shirika la BBC kwa kukana mauaji ya kimbari yaliyofanywa na Wahutu dhidi ya Watutsi wachache nchini humo.
Duru za habari kutoka Kigali zimesema, uamuzi huo umechukuliwa baada ya wabunge na makundi ya kiraia katika siku za hivi karibuni kuitaka serikali kuzuia urushwaji wa matangazo ya BBC nchini humo.
Mnamo mwaka 2009, Rwanda ilikatisha matangazo ya redio na televisheni ya BBC nchini humo, kutokana na kupotosha kile kinachoelezwa kuwa uhakika wa mambo kuhusiana na mauaji ya kimbari ya mwaka 1994.
Zaidi ya Watutsi 800,000 waliuawa kinyama mbele ya macho ya wanajeshi wa Umoja wa Mataifa na askari wa Ufaransa waliokuwepo nchini humo mwaka 1994.
No comments:
Post a Comment