Familia ya baba wa taifa hayati mwalimu Julius Kambarage Nyerere imeuomba uongozi wa benki kuu ya Tanzania kuiondoa katika mzunguko wa fedha noti ya shilingi elfu moja yenye picha ya Baba kwa maelezo kuwa picha ambayo imetumika katika noti hiyo haifanani kabisha na kiongozi huyo na kwamba kuendelea kutumika ni sawa na kumdhalilisha muasisi huyo wa taifa la Tanzania.
Akizungumza kwa niaba ya familia na ukoo wa Baba wa taifa wakati wa kupokea mradi wa kuboresha makumbusha ya Mwalimu Nyerere na kuzindua onesho la noti na sarafu ambazo zimetumika katika vipindi tofauti kuanzia mwaka 1967 hadi sasa zenye picha na sahihi ya Baba wa taifa, mmoja wa watoto wa Baba wa taifa Bw Madaraka Nyerere, amesema picha iliyopo katika noti hiyo ya shilingi elfu moja haifanani na sura ya kiongozi huyo hivyo kuomba benki hiyo kuangalia uwezekano wa kuiondoka katika mzunguko.
Naye kaimu gavana wa benki kuu ya Tanzania Bw Juma Reli, pamoja na kutoa ahadi ya ukarabati nyumba ya kwanza ya Baba wa taifa ambayo aliitumia kabla ya kujengewa na tanu amesema kuwa benki hiyo imejitolea kuboresha makumbusho hayo ili kuhifadhia kumbukumbu zenye histori ya baba wa taifa kwa ajili ya vizazi vya sasa na vijavyo.
Kwa upande wao mkurugenzi mkuu wa shirika la makumbusho ya taifa Profesa Audax Mabula na mkuu wa wilaya ya butiama Bi Angelina Mabula, wameishukuru benki kuu ya Tanzania kwa kutambua umuhimu wa kuboresha makumbusho hayo katika kuhifadhi kumbukumbu mbalimbali za Baba wa taifa Mwalimu Julius Nyerere ili kulinda historia za kiongozi huyo.
Chanzo:ITV
No comments:
Post a Comment