Pages

Thursday, November 6, 2014

CHADEMA WAMSHUKIA ANDREW CHENGE

Chama cha Demokrasia na Maendeleo, (CHADEMA), kimemshukia Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge, (CCM), ambako kimevuna wanachama zaidi ya 50 wakiwemo viongozi wake wa vijiji watatu.

Aidha, wananchi wa jimbo hilo walimlaumu mbunge huyo kwa kushindwa kuwatatulia kero zao za ukosefu wa huduma ya maji safi na salama, ambako amekuwa haonekani jimboni kwa kipindi kirefu.

Tukio hilo lilitokea juzi kwenye viwanja vya halmashauri, ambako wanaCCM hao wakipokewa na Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake CHADEMA, (BAWACHA), Hawa Mwaifunga, wakati wa mkutano wa hadhara.

Viongozi walioikimbia CCM ni pamoja na wenyeviti na vitongoji vyao kwenye mabano, Lazaro Singibara, (Sarunda A), Bahame Maduhu (Sanangu), Sunga Makoro (Somanga), na Katibu Mwenezi kata ya Somanda Ikulu, Ndilanho Maduhu.

Akizungumza kwa niaba ya wenzake, Singibara alisema kuwa wameamua kujiunga na CHADEMA, baada ya kuona ndiyo chama pekee cha siasa nchini kinachopigania maslahi ya wanyonge.

Alisema kuwa wameamua kuondoka CCM baada ya kukitumikia kwa muda mrefu lakini mara zote chama hicho kimewasahau wananchi wanyonge na kuwakumbatia matajiri, hivyo wameona mahali sahihi kwao ni CHADEMA.

Awali akizungumza kwenye mkutano huo, Makamu Mwenyekiti wa BAWACHA, Mwaifunga, alisema kuwa Watanzania wanatakiwa kuunganisha nguvu pamoja kuing’oa CCM madarakani kwa kushindwa kuwapa maisha bora kama walivyoahidi kwenye uchaguzi mkuu uliopita.

Alisema kuwa ugumu wa maisha unawakuta wananchi wote bila kujali itikadi ya vyama, kwani hata ukiwa na kadi ya CCM ukienda hospitali hupati dawa wala matibabu, hivyo kwa sasa njia pekee ni kuikataa CCM ili CHADEMA waingie madarakani, kwani sera zao zimelenga kuwaondolea kero wananchi kwenye sekta zote ikiwemo afya.

Kiwelu amshukia Chenge

Mbunge wa viti maalum, Grace Kiwelu, alisema kuwa inashangaza kuona jimbo linaloongozwa na Chenge ambaye ni maarufu kwa jina la Vijisenti, kukosa huduma muhimu hata ya maji safi.

Alisema kuwa mara zote Chenge amekuwa kimya wakati wabunge wengine wakipigania kutatuliwa kwa kero kwenye majimbo yao, jambo alilodhani kuwa kwenye jimbo lake kila kitu kiko sawa, kumbe wananchi wake wanakabiliwa na kero lukuki.

“Wakati tunazunguka maeneo mbalimbali ya jimbo hili, nimeshangazwa kusikia kuwa kuna wananchi hawajawahi kumuona mbunge wao, hivi kweli mnakuwa na mbunge ambaye hamjamuona sasa matatizo yenu atayajuaje?…

“Niwaombe kwenye uchaguzi ujao mfanye maamuzi sahihi kwa kuchagua mgombea atakayesimamishwa na UKAWA, kataeni kuchagua watu kwa kuchinjiwa ng’ombe na pilau, matokeo yake ndiyo haya hamumuoni mbunge na miaka mitano inakaribia kwisha,” alisema Kiwelu.

Tendega naye amshambulia Chenge kwa ubinafsi

Katibu wa BAWACHA Taifa, Grace Tandega, alisema kuwa mbunge wa jimbo hilo aliwahi kudaiwa kuweka kiasi kikubwa cha fedha nje ya nchi, wakati angeweza kufanya uwekezaji jimboni kwake na kuongeza mzunguko wa fedha.

Alisema kuwa ubinafsi huo wananchi waliukataa, ndiyo sababu walipendekeza kwa Tume ya mabadiliko ya katiba kuwa watu wasiruhusiwe kuweka fedha kwenye benki za nje ya nchi bila kibali maalum, lakini Chenge ambaye aliongoza kamati ya uandishi wa katiba pendekezwa, akishirikiana na wabunge wa CCM wakaamua kuondoa pendekezo hilo kwani linawabana.

Naibu Katibu BAWACHA alia na mfumo wa elimu nchini

Naibu Katibu BAWACHA Taifa, Kunti Yusuph, alisema kuwa serikali ya CCM imeamua kwa makusudi kuharibu mfumo wa elimu nchini, ili kuhakikisha wanakuwa madarakani na wakitoka wanawarithisha watoto wao wanaowasomesha nje ya nchi wanakopata elimu bora.

Alisema kuwa watoto wa wananchi maskini, hawatakwepa kuendelea kutawaliwa kwani hawapati elimu bora kwenye shule za kata wanazopelekwa, hivyo hawawezi kushika nyadhifa kubwa serikalini.

Kunti alisema kuwa shule hizo hazina waalimu, vifaa vya kufundishia hata dawati la kukaa darasani hamna, jambo alilosema kuwa Taifa litaendelea kushuhudia watoto wengi wanaomaliza shule bila kujua kusoma na kuandika.

Alisema kuwa Rais wa awamu ya kwanza, Baba wa Taifa, Julius Nyerere, aliacha nchi ikiwa na mfumo mzuri wa elimu, kwani ilikuwa kitabu kimoja kinatumika kufundisha nchi nzima tofauti na sasa, ambako vinatumika vitabu zaidi ya kimoja kufundishia, jambo linalowachanganya wanafunzi.

Chanzo Tanzania Daima

No comments:

Post a Comment