Mvua kubwa zinazoendelea kunyesha nchini mbali na kusababisha vifo na maafa mengine, zimeutenga Mkoa wa Dar es Salaam na maeneo mengine ya nchi baada ya madaraja muhimu katika barabara zinazoingia kukatika.
Kutokana na athari za mvua hizo, njia kuu za
kuingia Dar es Salaam, ikiwamo barabara za Morogoro, Bagamoyo na Kilwa
zilifungwa jana na kusababisha usumbufu mkubwa kwa wasafiri.
Maeneo yaliyoharibika ni karibu na Daraja la Mto
Ruvu lililofurika maji na kusababisha magari kwenda mikoa ya Kaskazini,
Magharibi na Nyanda za Juu Kusini na nchi jirani kukwama.
Ukiacha barabara, safari za anga nazo ziliathirika
kwa muda kuanzia mwishoni mwa wiki kutokana na barabara za ndege kutua
na kurukia kujaa maji kutokana na mvua hizo zilizoambatana na upepo
mkali.
Abiria wanaosafiri kwenda mikoani na nchi jirani
walikwama katika Kituo Kikuu cha Mabasi Ubungo (UBT) kutokana na
kukatika kwa mawasiliano ya barabara.
Barabara ya Morogoro
Rais Jakaya Kikwete alitembelea eneo ya Ruvu
Darajani na kukutana na maelfu ya wasafiri waliokwama kutokana na
mafuriko. Aliwapa pole na kuahidi kuwa Serikali itapambana kurekebisha
uharibifu huo.
Hata hivyo, Rais Kikwete aliyewasili mchana
akiambatana na mkewe, Mama Salma alisema: “Serikali ina uwezo wa kuzuia
mambo mengine lakini haina uwezo wa kuzuia mafuriko na kinachotakiwa ni
kumwomba Mungu ili hekima zake zifanye kazi na kuepusha hali ya hatari
kwa wananchi.”
Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mwantumu Mahiza aliwataka
wamiliki wa magari makubwa yaliyoko Dar es Salaam kusitisha safari hadi
hapo hali itakapotengamaa.
Katika Mto Mzinga unaotenganisha Dar es Salaam na
mikoa ya Lindi na Mtwara, ilibidi magari yazuiwe kuvuka baada ya daraja
lilipo kati ya Mbagala na Kongowe kumegwa upande na mvua. Jana abiria
walikuwa wakivuka taratibu katika upande uliosalia, lakini baadaye
lilizolewa kabisa.
Kabla ya daraja lote halijazolewa na mvua,
waandishi wetu walishuhudia mamia ya wasafiri wenye mizigo wakivuka
katika daraja hilo huku wakiongozwa na polisi ili kupita.
Baada ya polisi kuona daraja hilo linazidi kubomoka, waliwazuia watu na baada ya muda mfupi likazolewa na maji.
Barabara ya Bagamoyo
Wizara ya Ujenzi, jana ilianza kujenga Daraja la
Mapinga lililokatika juzi. Malori yalionekana yakimwaga mawe ili
kulirudisha katika hali ya kawaida.
Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, Mhandisi Mussa
Lyombe alisema wizara yake ina upungufu wa nyenzo za kazi lakini
inajitahidi kuhakikisha mawasiliano yanarejea.
Awali, Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli alisema
ameagiza makandarasi wake kufanya kazi usiku na mchana kuhakikisha
mawasiliano yanarudi.
Safari za anga zaathirika
Mvua hizo zimesababisha kukwama kwa muda kwa
baadhi ya safari za ndege za ndani na za kimataifa, baada ya kushindwa
kutua na kuondoka katika Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere (JNIA).
Msemaji wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania
(TCAA), Bestina Magutu alisema jana kwamba walilazimika kusimamia
kusitisha baadhi ya safari na kuzuia baadhi ya ndege kutua kutokana na
hali ya hewa kutokuwa nzuri.
“Uamuzi huo ulikuwa ni muhimu kwa sababu ya usalama wa ndege na abiria,” alisema.
Kutokana na hali hiyo, ndege ya Shirika la Ndege
la Emirates ilielekezwa kutua Mombasa, Precision Air ilisitisha safari
wakati ndege ya ATCL ilishindwa kuondoka juzi.
Ofisa Uhusiano wa Shirika la Fastjet, Lucy Mbogoro
alisema baadhi ya safari za ndege zake zilikwama kwa muda juzi kutokana
na hali ya hewa.
No comments:
Post a Comment