Balozi Ombeni Sefue akionyesha hati ya muungano kwa waandishi wa habari ikulu Dar es salaam jana.
Baada ya mvutano wa muda mrefu bungeni kuhusu ilipo Hati ya Muungano, Ikulu jana iliamua kuitoa hadharani huku ikisisitiza kuwa, “ni halisi na haikuchakachuliwa.”
Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue
akizungumza Ikulu jana, alisema madai ya kuonyeshwa kwa Hati ya Muungano
yalianza siku nyingi na hawakufahamu kama yangefika hatua yalipofikia.
“Ukweli ni kuwa hati hiyo ipo na ilikuwapo siku
zote,” alisema Balozi Sefue na kuongeza: “Hata hivyo, tukubaliane kwamba
kuna hati fulani ambazo ni kiini cha uwepo wetu kama Taifa huru, kama
Jamhuri huru, kama Muungano huru ambazo zinahifadhiwa kama mboni ya
jicho.
Balozi Sefue alizitaja kuwa ni Hati ya Uhuru wa
Tanganyika ya mwaka 1961, Hati ya Tanganyika kuwa Jamhuri mwaka 1962 na
Hati ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ya mwaka 1964 na kusema
zinahifadhiwa maeneo maalumu ili zisipotee au kuharibika.
“Maneno yamekuwa mengi mno, tuhuma zimekuwa
nyingi, dhihaka zimekuwa nyingi kiasi cha wananchi kuanza kutia shaka
kuwa hati ya Muungano ipo au la,” alisema na kuongeza:
“Kutokana na agizo na ridhaa ya Rais Jakaya
Kikwete, ninaleta kwenu waandishi wa habari hati halisi ya Muungano wa
Tanganyika na Zanzibar iliyotiwa saini Zanzibar na waasisi wetu Mwalimu
Julius Kambarage Nyerere na Abeid Aman Karume ili muione, mridhike nayo
na muwajulishe wananchi.”
Baada ya kuwaonyesha aliwagawia wanahabari hao
nakala ya hati hiyo na kusema Ikulu itafanya utaratibu wa kuiweka katika
makumbusho ya Taifa ili kila mwananchi anayependa kuiona aende huko.
Kuhusu hati hiyo kupelekwa bungeni mjini Dodoma,
Balozi Sefue alisema iwapo Mwenyekiti wa Bunge la Katiba, Samuel Sitta
ataiomba, Ikulu itaipeleka ili kuondoa mjadala wa uwepo wa hati hiyo.
“Tumesikitishwa, kusononeka na kufadhaika sana na
tuhuma nzito kwamba waasisi wetu hawakuwa makini au walitufanyia kiini
macho. Hatukutarajia Watanzania wenzetu wafikie hapo ni jambo zito,”
alisema Balozi Sefue
Katika kipindi cha maswali, Balozi Sefue
alishindwa kubainisha ilikuwa wapi wakati wote na kusisitiza: “Kazi ya
leo ilikuwa ni kuwaonyesha hati hiyo na ninaomba maswali yenu yajikite
katika hili.”
No comments:
Post a Comment