Jaji Warioba
Habari
Dar na Dodoma. Ofisi ya Rais (Ikulu) imesema haikuwatupia virago wajumbe wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu ilitoa
taarifa hiyo jana ikirejea taarifa zilizomnukuu aliyekuwa Mwenyekiti wa
Tume hiyo, Jaji Joseph Warioba akisema: “Ikulu imetutupia virago.”
Jaji Warioba alikaririwa akilalamikia jinsi yeye
na makamishna wa tume, walivyoondolewa ofisini na kunyang’anywa magari
kwa haraka bila kusubiri siku waliyokuwa wamepanga kufanya makabidhiano.
Taarifa ya Ikulu ilisema kifungu cha 31 (1) cha
Sheria ya Mabadiliko ya Katiba kinasema shughuli za tume zinakoma baada
ya Mwenyekiti wake kuwasilisha Rasimu ya Katiba kwenye Bunge Maalumu la
Katiba.
Ilifafanua kuwa Jaji Warioba aliwasilisha Rasimu
ya Katiba bungeni Machi 18, 2014 na siku iliyofuata Machi 19, 2014 na
kwa mujibu wa Sheria Rais alitia saini tangazo la Serikali kuvunja tume
hiyo.
Ilisema tangu mwanzo wajumbe, mwenyekiti,
Sekretarieti ya Tume na Watanzania wote waliijua siku ya mwisho ya Tume
kukamilisha shughuli zake, hivyo kwa mtu “kujitia ameisahau siku hiyo ni
kiwango cha juu sana cha unafiki.”
“Siku hiyo ya mwisho iliwekwa kwa mujibu wa Sheria
ya Mabadiliko ya Katiba, na Ikulu haikuwa na madaraka wala mamlaka
yoyote kubadilisha tarehe hiyo.
Hivyo, madai ya Ikulu kuitupia virago Tume ya
Mabadiliko ya Katiba hayana msingi wowote na ni jambo la kutunga tu,”
ilisema taarifa hiyo.
Ilisema tangu Tume ilipovunjwa, haikuwa tena na kazi ya kuandaa ripoti au Rasimu kwa sababu kazi hiyo ilikuwa imekwisha.
Kuhusu muda wa kuandika ripoti ya makabidhiano,
taarifa hiyo ilihoji kuwa tangu Desemba 30, mwaka jana sekretariati
ilikuwa na muda wa siku 77, ilishindwa nini kuiandaa wakati maofisa wake
walikuwa wanaendelea kulipwa mshahara na Serikali.
Kurudisha magari
Kuhusu wajumbe kutakiwa kurudisha magari Ikulu,
taarifa hiyo imekiri ikitoa sababu kuwa kazi ya tume ilikuwa imemalizika
na kwamba magari hayo yanatakiwa kupelekwa kwenye Bunge la Katiba mjini
Dodoma.
Hata hivyo Makamu Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji Mkuu Mstaafu
Augustino Ramadhani na mmoja wa wajumbe, Profesa Mwesiga Baregu
wameungana na Jaji Warioba wakieleza kutofurahishwa na jinsi Serikali
ilivyowatendea.
Jaji Ramadhani alisema wenzake walipokutana
Jumatano iliyopita, yeye alikuwa Arusha na dereva aliyekuwa akimwendesha
kwenye gari la tume alimwarifu kuwa gari hilo linatakiwa kurejeshwa,
hivyo akamruhusu atekeleze alivyoagizwa.
“Nimeingia Dar es Salaam Jumamosi saa 11:00 jioni,
gari nililokuwa natumia lilichukuliwa nikiwa Arusha na niliporejea sasa
natumia gari langu mwenyewe,” alisema Jaji Ramadhan.
Kwa upande wake Profesa Baregu alisema hatua
zilizochukuliwa na Serikali katika kuvunja tume hiyo zimewafanya
wajihisi kama wahaini.
Profesa Baregu alisema, “Heri yetu wengine lakini
kwa mzee wetu (Warioba) kutokana na kuwa Waziri Mkuu mstaafu, analindwa
na walinzi wanaopata maelekezo kutoka kwa Serikali ambayo imetuondoa
kwenye kazi iliyotukabidhi kisheria kama wahalifu, sifahamu hatima
yake.”
Alisema Jumatano iliyopita wajumbe wote wa tume
walikutana wakakubaliana Ijumaa wakabidhi vifaa mbalimbali yakiwamo
magari lakini alipoingia kwenye gari lake kurudi nyumbani, dereva
akamfahamisha kuwa wameelekezwa siku inayofuata asubuhi magari yote
yapelekwe Ikulu.
Alisema hali ilikuwa mbaya kwa waliokuwa wakiishi
na familia zao kwenye nyumba walizokuwa wamepangiwa kwa ajili ya kazi za
tume, kwani walitakiwa wazirejeshe mara moja lakini kwa kuwa zilikuwa
zimelipiwa mpaka Machi 31 wakaachwa wakabaki mpaka siku hiyo.
Alipoulizwa kama ameitwa Dodoma kutoa ufafanuzi wa
Rasimu yao, Profesa Baregu alisema: “Tuliyotendewa tunahisi
tunachukuliwa kama wahaini, leo niitwe Dodoma niende kwa imani gani?
Sijaitwa na hata ningeitwa nisingeenda.”
Kukabidhi ofisi
Naibu Katibu wa Tume, Kashmir Kyuki alithibitisha jana kuwa makabidhiano kati ya Tume na Serikali yamekamilika.
Kyuki ambaye pia ni Mwandishi Mkuu wa Sheria
Tanzania, alisema hata madeni ya Tume yamekabidhiwa kwa Serikali na
wameafikiana na Wizara ya Katiba na Sheria itangaze kuwa yapo chini
yake, ili kuwaondolea hofu wadai.
Alizungumzia suala la aliyekuwa mjumbe, John Nkolo
aliyeugua wakati tume ikiendelea na kazi, alisema pia limekabidhiwa kwa
Katiba Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria.
“Tumewaeleza kuwa tuna mgonjwa tuliyekuwa tukimuhudumia, ataendelea kuhudumiwa kwa mujibu wa sheria na kanuni za ajira serikalini kwa sababu aliugua akitumikia Serikali, watamuhudumia tu,” alisema Kyuki.
Chanzo: Mwananchi.
“Tumewaeleza kuwa tuna mgonjwa tuliyekuwa tukimuhudumia, ataendelea kuhudumiwa kwa mujibu wa sheria na kanuni za ajira serikalini kwa sababu aliugua akitumikia Serikali, watamuhudumia tu,” alisema Kyuki.
Chanzo: Mwananchi.
No comments:
Post a Comment