Pages

Thursday, April 3, 2014

MLIPUKO WA LORI LA MAFUTA WATOKEA DAR,LAJERUHI WAWILI

   

 Mafundi wa Kampuni ya Oilcom wakiangalia mabaki ya lori la kampuni hiyo lililochanika baada ya kulipuka kwa tanki lake wakati likichomewa katika eneo la Tabata Relini, jijini Dar es Salaam jana.

                                                   Habari Kamili
 Taharuki ya aina yake ilitokea jana eneo la Tabata Relini, Dar es salaam  kwenye yadi ya malori ya Kampuni ya Oilcom baada ya kutokea kishindo kikubwa kilichotokana na kupasuka kwa tanki la mafuta.
Tukio hilo lililotokea saa 11 jioni, lilizua hofu miongoni mwa wakazi na wafanyakazi wa eneo hilo, na lilitokana na hitilafu ya kiufundi wakati wa kulitengeneza tanki hilo.
Mashuhuda wa tukio hilo lililojeruhi watu watatu waliliambia Mwananchi kuwa mlipuko huo ulitokea wakati fundi akichomea sehemu ya tanki katika karakana ya magari ya kampuni hiyo.
“Kuna fundi alikuwa juu ya lori akipima mifuniko na chini alikuwepo dereva wa lori hilo na fundi mwingine wa kuchomea vyuma akichomea, wote walikuwa wakiendelea na kazi.
“Dereva wa lori hilo alikuwa akimuelekeza fundi sehemu ya kuchomea na ghafla ukatokea mlipuko mkubwa,” alisema Omari Wenge, fundi katika karakana hiyo.
Alisema mlipuko huo ulimtupa chini fundi aliyekuwa juu ya tanki na kulikosababisha aumie usoni na sehemu za kifuani.
Shuhuda huyo alisema dereva na fundi wa kuchomea, waliumizwa sehemu mbalimbali za mwili kwa kupigwa na vipande vya mabati ya tanki na kichwa cha gari hilo.
Majeruhi wa ajali hiyo walipelekwa katika Hospitali ya Amana kwa matibabu zaidi. Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni Camillus Wambura alisema kuwa hakuwa amepata taarifa zozote za ajali hiyo hivyo angetujulisha pindi angezipata.
Mwandishi wa habari hizi alishuhudia baadhi ya wafanyakazi wa karakana hiyo wakipewa huduma ya kwanza baada ya kuzimia kwa mshtuko huku wengine wakiweweseka kwa hofu.
Kichwa cha lori hilo kilichakazwa na mlipuko huo ambao moja ya mabati yanayoligawa tanki hilo yalitupwa upande wa pili wa Barabara ya Mandela.
Sehemu ya juu ya mbele ya lori hilo, ilitupwa juu ya paa la moja ya majengo ya karakana hiyo huku chini zikiwa zimetapakaa nyaraka na mabaki mengine ya sehemu ya mbele ya lori hilo.
Naye mmoja wa mashuhuda, Boniface Msisi aliyekuwemo ndani ya karakana hiyo, alisema hali ndani ya eneo hilo ilibadilika ghafla huku kila mfanyakazi akitafuta mlango wa kutokea.
“Mmoja wa mamalishe wanaotoa huduma ya chakula katika eneo hilo, alizimia mara baada ya kusikia kishindo hicho...kila unayemuona hapa ndio kwanza anarudi katika hali yake,” alisema Msisi huku akionyesha sehemu ya tanki iliyokuwa ikichomewa.
Alisema kuwa lori hilo lilikuwa limetoka safari hivyo walikuwa wakilifanyia matengenezo ya kawaida.
Juhudi za kuupata uongozi wa karakana kuzungumzia ajali hiyo uligonga mwamba kutokana na viongozi hao kuwa katika harakati za kuokoa maisha ya majeruhi.

Chanzo: Mwananchi

No comments:

Post a Comment