Wananchi wa mkoa wa Mtwara wametakiwa
kuchangamkia fursa zilizopo kutokana na kugundulika kwa kiasi kikubwa
cha gesi katika mkoa huo kilichopelekea uwekezaji katika viwanda ikiwa
ni pamoja na kiwanda cha kusafisha gesi.
Hayo yalisemwa na Katibu Mkuu Kiongozi
Balozi Ombeni Sefue aliyekuwa katika ziara ya siku mbili katika mikoa ya
Lindi na Mtwara kwa ajili ya kujionea maendeleo ya ujenzi wa
miundombinu ya bomba la gesi ikiwa ni pamoja na kiwanda cha kusafisha
gesi cha Madimba na kiwanda cha simenti cha Dangote kilichopo Mtwara.
Katibu Mkuu kiongozi aliambatana na
makatibu wakuu kutoka wizara tofauti ikiwa ni pamoja na Bw. Eliakim
Maswi (Wizara ya Nishati na Madini) Dkt. Servacius Likwelile (Wizara ya
Fedha na Uchumi) Bw. Job Masima (Wizara ya Ulinzi) Dkt. Shaban Mwinjaka
(Wizara ya Uchukuzi) Bw. Alphayo Kidata (Wizara ya Ardhi) na Naibu
Katibu Mkuu, Wizara ya Ujenzi Mhandisi Joseph Nyamhanga.
Wengine alioambatana nao ni Katibu
Mtendaji (Mipango) Dkt. Philip Mpango, Kaimu Kamishna Mkuu kutoka
Mamlaka ya Mapato Nchini (TRA) Bw. Rished Bade ikiwa ni pamoja na
watendaji kutoka katika Wizara ya Nishati na Madini na taasisi zake.
Balozi Sefue alisema kuwa umefika
wakati wa wananchi kuchangamkia fursa hizo ili kujiletea maendeleo kwa
vizazi vilivyopo na vijavyo bila kusahau sekta nyingine muhimu.
“ Nimefarijika sana na kasi ya ujenzi
wa bomba la gesi ikiwa ni pamoja na mikakati mkoa umejiwekea ya
maendeleo lakini rai yangu ni kuwa, tusisahau sekta nyingine muhimu
kwani gesi ni rasilimali inakwisha.’’ Alisema Balozi Sefue.
Balozi Sefue aliongeza kuwa fedha
inayopatikana na gesi inatakiwa kutumika ipasavyo kujenga uchumi kwa
kufungua vitega uchumi vingine vinavyoweza kuiwezesha Mtwara kuendeleza
ukuaji wa uchumi wake hata mara baada ya gesi kwisha kabisa mbeleni.
“Inatakiwa ifikie vizazi vijavyo
vijivunie na vitenga uchumi vilivyotokana na gesi iliyogunduliwa, kwa
maana nyingine gesi iwe imebadilisha historia ya Mtwara, naamini hivyo
inawezekana kabisa iwapo rasilimali hii muhimu itasimamiwa ipasavyo. “
Alisisitiza Balozi Sefue.
Wakati huo huo akiwasilisha taarifa ya
maendeleo yaliyotokana na gesi mkuu wa mkoa huo Mhe. Jospeh
Simbakalia alisema kuwa kutokana na ugunduzi wa gesi fursa nyingi
zimeanza kuonekana katika mkoa huo.
Akitaja fursa hizo Bw. Simbakalia
alisema ni pamoja na benki kuu ya Tanzania kufungua tawi lake katika
mkoa huo, upanuzi wa bandari ikiwa ni pamoja na kujengwa kwa kiwanda cha
simenti cha Dangotte.
Mhe. Simbakalia aliongeza kuwa zaidi ya
ajira 300 zimetolewa kwa vijana wanaoshiriki katika mradi wa ujenzi wa
bomba la gesi na kuongeza kuwa ifikapo mwaka 2025 mkoa wa Mtwara
utakua umepaa sana kiuchumi.
Akizungumzia changamoto zilizopo katika
mkoa wake Mhe. Simbakalia aliongeza kuwa ni pamoja na kutokuwa na
wataalamu wa kutosha kutoka mkoa wa Mtwara wanaoshiriki katika mradi wa
bomba la gesi.
Hata hiyo Bw. Simbakalia alifafanua
kuwa kutokana na changamoto hiyo wameanzisha shule mbili kwa ajili ya
wanafunzi wa masomo ya sayansi na hisabati ili kuzalisha wanafunzi
watakaojiunga na vyuo vikuu vilivyopo nchini ikiwa ni pamoja na nje ya
nchi kwa ajili ya kusomea masuala ya gesi na petroli.
“ Kwa mfano Wizara ya Nishati na Madini
imekuwa ikitoa ufadhili kwa ajili ya wanafunzi wetu kusoma katika vyuo
vikuu vilivyopo ndani na nje ya nchi , lakini changamoto kubwa inakuwa
ni upatikanaji wa wanafunzi wenye sifa hizo yaani waliofaulu katika
masomo ya hisabati na kiingereza, lakini tumejipanga kuzalisha wanafunzi
wenye sifa hizo ili siku za usoni tupeleke wanafunzi wetu nje ya nchi
na kujenga uchumi wa Mtwara.” Alisisitiza Mhe. Simbakalia.
Vilevile Mkuu wa Mkoa huyo alitaja
changamoto nyingine kuwa ni pamoja na kutokuwa na teknolojia ya kisasa
katika utafutaji na uchimbaji wa gesi ikiwa ni pamoja na vifaa vya
kisasa.
Alisisitiza kuwa mradi wa gesi unahitaji uwekezaji mkuwa, kifedha, kiteknolojia na kitakwimu.
Imeandaliwa na:
Asteria V. Muhozya,
Afisa Habari,
Wizara ya Nishati na Madini,
754/33 Mtaa wa Samora
S.L.P 2000 Dar es Salaam
Tel: +255-22-2121606/7, Fax: +255-22-2121606
Email:info@mem.go.tz
Tovuti: www.mem.go.tz
No comments:
Post a Comment