Pages

Wednesday, April 2, 2014

KESI YA ZITO YAPELEKWA MBELE

Dar es Salaam. Kesi ya aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, Zitto Kabwe dhidi ya chama chake imepigwa kalenda hadi Mei 29, 2014.
 Kesi hiyo ilipangwa kutajwa jana katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam na Jaji John Utamwa anayeisikiliza, lakini iliahirishwa na Msajili wa Wilaya wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Amir Msumi. Akiahirisha kesi hiyo, Msumi alisema Jaji Utamwa hakuweza kufika jana kwa sababu anaumwa na akapanga kesi hiyo itajwe mahakamani hapo tarehe hiyo.
     Hii ni mara ya pili kwa kesi hiyo kuahirishwa na wasajili kutokana na sababu za ugonjwa wa Jaji Utamwa. Mara ya kwanza iliahirishwa na Msajili William Mtaki Februari 13, 2014.
Zitto ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini alifungua kesi hiyo dhidi ya Bodi ya Wadhamini wa Chadema na Katibu Mkuu wa Chadema, akiiomba mahakama hiyo ikizuie chama kujadili uanachama wake, hadi rufaa anayokusudia kuikata baraza kuu la chama kupinga kuvuliwa nyadhifa, itakaposikilizwa.
   Katika kesi hiyo namba 1 ya 2014, Zitto pia aliiomba mahakama hiyo imwamuru Katibu Mkuu wa Chadema ampatie mwenendo na taarifa za kikao cha kamati kuu ya Chadema kilichomvua nyadhifa zote alizokuwa nazo ndani ya chama na iwazuie walalamikiwa kumwingilia katika utekelezaji wa majukumu yake kama mbunge wa kigoma kaskazini.
  Chanzo: Mwananchi
http://upload.wikimedia.org/wikipedia/sw/2/29/Zitto_Kabwe.jpg
                                             Mh. Zitto Kabwe

No comments:

Post a Comment