UTANGULIZI
Mheshimiwa Mwenyekiti,
Sura ya Kwanza na Sura ya Sita ya Rasimu ya Katiba ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania (‘Rasimu’) ndizo msingi ambao Rasimu yote imejengwa
juu yao. Wakati Sura ya Kwanza inagusa suala la muundo wa Muungano
katika ibara moja tu kati ya ibara tisa, Sura yote ya Sita inahusu
‘Muundo wa Jamhuri ya Muungano.’ Suala la Muungano na hasa Muundo wake
limetawala mjadala wa kisiasa na kikatiba wa Tanzania kwa zaidi ya miaka
thelathini. Ndio maana katika waraka wake wa siri kwa Halmashauri Kuu
ya Chama cha Mapinduzi (‘CCM’), Idara ya Siasa na Uhusiano wa Kimataifa
ya chama hicho imetamka kwamba “muundo wa Muungano ndiyo moyo wa Rasimu
na ndiyo unaoamua ibara nyingine zikae vipi.”
Suala hili pia limetawala mchakato wa Katiba Mpya tangu ulipoanza
miaka mitatu iliyopita. Kama alivyosema Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko
ya Katiba Joseph Sinde Warioba wakati wa kuwasilisha Ripoti ya Tume
yake kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano na Rais wa Zanzibar tarehe 30
Disemba, 2013: “Moja ya mambo ambayo yamejadiliwa sana na kwa hisia kali
tangu Rasimu ya awali ilipotolewa ... ni Muungano wa Tanzania. Jambo
kubwa limekuwa juu ya muundo wa Muungano.”[1]
Umuhimu wa suala hili unathibitishwa pia na uamuzi wa Kamati ya
Uongozi ya Bunge Maalum kuelekeza kwamba Kamati zake Namba Moja hadi
Kumi na Mbili zianze kujadili Sura ya Kwanza na ya Sita ya Rasimu. Haya
ni maoni ya wajumbe walio wachache wa Kamati Namba Nne juu ya Sura hizi
mbili.
Mheshimiwa Mwenyekiti,
Mjadala wa Kamati Namba Nne kuhusu Sura za
Kwanza na Sita za Rasimu unathibitisha pia umuhimu wa suala la muundo
wa Muungano katika mjadala mzima wa Rasimu. Kama Taarifa ya Kamati yetu
inavyoonyesha, Kamati Namba Nne imeshindwa kufanya uamuzi kuhusu suala
hili katika ibara za 1 na 60 za Rasimu. Katika ibara ya 1 ya Sura ya
Kwanza, wajumbe walio wengi walipata kura 22, ambayo ndiyo theluthi
mbili ya kura za wajumbe wote 33 wa Tanzania Bara wa Kamati Namba Nne.
Kwa upande wa Zanzibar, wajumbe walio wengi walipata kura 9 ambayo ni
pungufu ya kura 13 zinazohitajika ili kufikisha idadi ya theluthi mbili
ya wajumbe wote 19 wa Zanzibar.
Kwa upande wa ibara ya 60,
wajumbe walio wengi walipata kura 22 za wajumbe kutoka Tanzania Bara,
ambazo ni theluthi mbili ya idadi ya wajumbe wote 33 kutoka Tanzania
Bara. Aidha, kwa Zanzibar, wajumbe walio wengi walipata kura 8, ambazo
pia ni pungufu ya kura 13 zinazotakiwa kufikisha idadi ya theluthi mbili
ya wajumbe wote 19 kutoka Zanzibar. Kwa sababu hiyo, ibara za 1 na 60
za Rasimu hazikupitishwa au kuamuliwa na Kamati Namba Nne kama
inavyotakiwa na kifungu cha 26(2) cha Sheria na kanuni ya 64(1) ya
Kanuni.
Mheshimiwa Mwenyekiti,
Sasa tunaomba kwa ridhaa
yako, tuwasilishe hoja na sababu za maoni ya wajumbe walio wachache
katika Kamati Namba Nne kuhusu Sura hizi mbili ambazo ndio ‘moyo wa
Rasimu.’
SURA YA KWANZA
Sura ya Kwanza ya Rasimu
inahusu ‘Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.’ Sehemu ya Kwanza ya Sura hiyo
inazungumzia ‘jina, mipaka, alama, lugha na tunu za Taifa.’ Ibara ya 1
inaitambulisha Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; ibara ya 2 inatangaza
‘eneo la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania’; na ibara ya 3 inaweka
utaratibu wa ‘alama na sikukuu za Taifa.’ Vile vile ibara ya 4 inaweka
utaratibu wa lugha ya Taifa na lugha za alama, wakati ibara ya 5 inahusu
‘tunu za Taifa.’
Kwa upande wake, Sehemu ya Pili ya Sura ya
Kwanza inaweka masharti ya ‘mamlaka ya wananchi, utii na hifadhi ya
Katiba. Ibara ya 6 ya Sehemu hiyo inatoa ufafanuzi wa ‘mamlaka ya
wananchi’; ibara ya 7 inafafanua uhusiano kati ya ‘watu na Serikali’;
ibara ya 8 inashurutisha ‘ukuu na utii wa Katiba’; na ibara ya 9 na ya
mwisho inaweka ‘hifadhi ya utawala wa Katiba.’
IBARA YA 1
Mheshimiwa Mwenyekiti,
Kama maelezo yake ya pembeni (marginal note) yanavyoonyesha, ibara ya 1
inaitambulisha ‘Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.’ Ibara ya 1(1)
inatamka kwamba “Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni Shirikisho lenye
mamlaka kamili ambayo imetokana na Muungano wa nchi mbili za Jamhuri ya
Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar ambazo kabla ya Hati za
Makubaliano ya Muungano ya mwaka 1964 zilikuwa nchi huru.”
Kwa
upande wake, ibara ya 1(2) inafafanua kwamba Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania “ni Shirikisho la kidemokrasia linalofuata mfumo wa vyama vingi
vya siasa, usawa wa binadamu, kujitegemea, utawala wa sheria, kuheshimu
haki za binadamu na lisilofungamana na dini.” Mwisho, ibara ya 1(3)
inatukumbusha kwamba “Hati ya Makubaliano ya Muungano ... ndio msingi
mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Katiba hii, kwa kadri
itakavyorekebishwa, itakuwa ni mwendelezo wa Makubaliano hayo.”
Mheshimiwa Mwenyekiti,
Wajumbe walio wachache wa Kamati Namba Nne wanapendekeza mabadiliko ya
jina la nchi yetu kutoka jina la sasa la ‘Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania’ kuwa jina jipya la ‘Shirikisho la Jamhuri za Tanganyika na
Zanzibar.’ Aidha, wajumbe hao wanapendekeza kuacha kutajwa kwa Hati ya
Makubaliano ya Muungano ya mwaka 1964 katika ibara ya 1(1) na (3) ya
Rasimu. Badala yake, inapendekezwa kwamba Katiba hii ndiyo iwe msingi wa
Shirikisho la Jamhuri za Tanganyika na Zanzibar.
Kwa
mapendekezo haya, ibara ya 1(1) itasomeka kama ifuatavyo: “Shirikisho la
Jamhuri za Tanganyika na Zanzibar ni Shirikisho ambalo limetokana na
Muungano wa nchi mbili za Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa
Zanzibar.” Kwa mantiki hiyo, ibara ya 1(2) itasomeka: “Shirikisho la
Jamhuri za Tanganyika na Zanzibar ni Shirikisho la kidemokrasia
linalofuata mfumo wa vyama vingi vya siasa, usawa wa binadamu,
kujitegemea, utawala wa sheria, kuheshimu haki za binadamu na
lisilofungamana na dini.” Aidha, ibara ya 1(3) itasomeka: “Katiba hii
ndio msingi mkuu wa Shirikisho la Jamhuri za Tanganyika na Zanzibar.”
Zifuatazo ni hoja na sababu za mapendekezo haya.
SHIRIKISHO AU MUUNGANO?
Mheshimiwa Mwenyekiti,
Katika nusu karne ya uhai wake, nchi yetu imeitwa ‘Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania.’ Hata hivyo, katika kipindi chote hicho, Katiba na Sheria
za nchi yetu hazijawahi kufafanua kwa uwazi aina au haiba ya ‘Muungano’
huu. Matokeo ya kukosekana kwa ufafanuzi huu ni kwamba katika nusu karne
hiyo, kumekuwa na mjadala mkubwa wa kikatiba, kisiasa na kitaaluma
kuhusu suala la kama Jamhuri ya Muungano ni dola ya muungano (a unitary
state), au ni dola ya shirikisho (a federal state). Majibu ya swali hili
yamekuwa na athari za moja kwa utambulisho, haki, maslahi na wajibu wa
Washirika wa Muungano huo, yaani Tanganyika na Zanzibar, na hasa kwa
wananchi wa nchi hizi mbili.
Mheshimiwa Mwenyekiti,
Kukosekana kwa ufafanuzi wa aina ya muungano wetu haujawa suala la
mijadala ya kisiasa na kikatiba peke yake, bali kumekuwa ni chanzo cha
migogoro mikubwa ya kisiasa baina ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano na
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar. Migogoro hii ilianza tangu mwanzo kabisa
wa Muungano wakati wa sakata la kuwa na ubalozi wa iliyokuwa Ujerumani
Magharibi kwa upande wa Tanganyika na ubalozi wa iliyokuwa Ujerumani
Mashariki kwa upande wa Zanzibar.
Aidha, kati ya mwaka 1964-1967
ulizuka mgogoro mkubwa kuhusiana na uwakilishi wa Zanzibar katika
iliyokuwa Bodi ya Sarafu ya Afrika Mashariki na uanzishwaji wa Benki Kuu
ya Tanzania; kuunganishwa kwa vyama vya ASP na TANU na kuundwa kwa CCM
mwaka 1977, na katika mjadala wa marekebisho ya Katiba wa mwaka na
baadae ‘kuchafuka kwa hali ya hewa ya kisiasa Zanzibar’ mwaka 1983/1984.
Baadae mwaka 1988 ulitokea mgogoro mkubwa uliopelekea kung’olewa
madarakani kwa Waziri Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Maalim
Seif Shariff Hamad na baadae kufukuzwa katika CCM; wakati wa harakati za
kudai kura ya maoni kuhusiana na Muungano mwaka 1989/1990; wakati wa
mjadala wa kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa mwaka 1991;
wakati wa sakata la Zanzibar kujiunga na Umoja wa Nchi za Kiislamu
(Organization of Islamic Countries - OIC) mwaka 1993; wakati wa mjadala
wa G-55 na madai ya kuanzishwa kwa Serikali ya Tanganyika ndani ya
Muungano mwaka 1994, na Uchaguzi Mkuu wa 1995 huko Zanzibar.
Milenia Mpya ilipoanza ilianza na mgogoro kuhusu matokeo ya Uchaguzi
Mkuu wa mwaka 2000 uliopelekea mauaji ya Januari 2001 huko Zanzibar.
Mgogoro huo ulifuatiwa na mgogoro juu ya suala la ugunduzi wa mafuta
visiwani Zanzibar; harakati za kuanzishwa kwa Shirikisho la Afrika
Mashariki na hivi karibuni kupitishwa kwa Marekebisho ya Kumi ya Katiba
ya Zanzibar ya 1984 mwaka 2010.
Zaidi ya migogoro hii, Serikali
ya Jamhuri ya Muungano na ile ya Mapinduzi zanzibar zimeunda tume na
kamati nyingi ili kupata dawa ya ‘Kero za Muungano.’ Serikali ya
Mapinduzi Zanzibar peke yake imeunda tume na kamati 13 katika kipindi
kifupi cha miaka 12 kuanzia mwaka 1992 hadi 2004; wakati Serikali ya
Jamhuri ya Muungano imeunda tume na kamati nane kushughulikia matatizo
hayo. Licha ya jitihada zote hizo, ‘Kero za Muungano’ hazijapatiwa
ufumbuzi wa kudumu.
Mheshimiwa Mwenyekiti,
Tangu miaka ya
mwanzo ya Jamhuri ya Muungano kulikuwa na mitazamo miwili tofauti
miongoni mwa waasisi na viongozi wakuu wa Jamhuri ya Muungano. Mitazamo
hii tofauti inathibitishwa na kauli ya Mwalimu Julius K. Nyerere,
mwasisi na Rais wa Kwanza wa Jamhuri ya Muungano katika Mkutano Maalum
wa Halmashauri Kuu ya CCM uliofanyika Dodoma kati ya tarehe 24-30
Januari, 1984: “... Muungano wa Tanzania ukiangalia kwa jicho la
Zanzibar ni wa shirikisho lakini ukiangalia kutoka upande wa Tanzania
Bara ni Serikali moja.”[2]
Mwalimu alikuwa akimjibu Makamu
Mwenyekiti wa CCM, Makamu wa Rais na Rais wa Zanzibar wakati huo, Alhaj
Aboud Jumbe Mwinyi aliyesema kwamba Muungano wa Tanzania umeunda
Shirikisho (Federation) na sio Serikali moja (Unitary State). Mjadala
huo ulipelekea ‘kuchafuka kwa hali ya hewa ya kisiasa Zanzibar’ na
kung’olewa madarakani kwa Jumbe, Waziri Kiongozi wake Ramadhani Haji
Faki na Mwanasheria Mkuu Bashir Kwaw Swanzy. Aidha, Wolfgang Dourado,
aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar wakati Hati ya Muungano
inasainiwa, na mkosoaji mkubwa wa Muungano huo, aliwekwa kizuizini kwa
kuunga mkono hoja za Rais Aboud Jumbe.
Mheshimiwa Mwenyekiti,
Miaka kumi baada ya ‘kuchafuka kwa hali ya hewa ya kisiasa Zanzibar’
Jamhuri ya Muungano ilikabiliwa na mgogoro mwingine tena wa kikatiba na
kisiasa, mara hii ukitokana na Zanzibar kujiunga na OIC. Kitendo hicho
kilizua tafrani kubwa ya kisiasa pale Bunge la Jamhuri ya Muungano
lilipopitisha Azimio la kutaka kuanzishwa kwa Serikali ya Tanganyika
ndani ya Muungano mwezi Agosti, 1993. Azimio hilo liliungwa mkono na
Serikali ya Jamhuri ya Muungano, kitendo kilichomfanya Mwalimu Nyerere
kuingilia kati na kuzima jaribio hilo.
Baadae Mwalimu aliandika
kitabu alichokiita Uongozi Wetu na Hatima ya Tanzania kilichochapishwa
mwaka 1994. Katika kitabu chake, Mwalimu anarejea mkanganyiko ambao
umekuwepo kuhusu aina ya Muungano huu kwa maneno yafuatayo:
“Nchi zinapoungana na kuwa nchi moja mifumo ya kawaida ya miundo ya
Katiba ni miwili: Kwa mfumo wa kwanza kila nchi itafuta serikali yake,
na nchi mpya inayozaliwa itakuwa ni nchi moja yenye serikali moja.
Katika mfumo wa pili kila nchi itajivua madaraka fulani ambayo
yatashikwa na serikali ya shirikisho, na itakuwa na serikali ambayo
itakuwa na mamlaka juu ya mambo yaliyobaki. Mambo yatakayoshikwa na
serikali ya shirikisho ni yale ambayo yakibaki katika mamlaka ya nchi
zilizoungana, basi kwa kweli nchi hizo zitakuwa hazikuungana kuwa nchi
moja, bali zinaendelea kuwa nchi mbili zenye ushirikiano mkubwa katika
mambo fulani fulani.... Shirikisho halisi la nchi mbili litakuwa ni nchi
moja yenye serikali tatu, Serikali ya shirikisho na serikali mbili za
zile nchi mbili za awali zilizoungana kuzaa nchi mpya moja.”[3]
Mheshimiwa Mwenyekiti,
Mwaka ambao Mwalimu Nyerere alichapisha Uongozi Wetu na Hatima ya
Tanzania, Makamu Mwenyekiti wake wa CCM na Makamu Rais wake hadi Januari
1984, Alhaj Aboud Jumbe, aliyekuwa pia Waziri wa Afya wa Zanzibar
wakati Muungano unazaliwa na baadae Rais wa Pili wa Zanzibar, naye
alichapisha The Partnership: Muungano wa Tanganyika na Zanzibar: Miaka
30 ya Dhoruba.[4] Katika kitabu hicho, Alhaj Jumbe anathibitisha kwamba
“Ibara za Mkataba wa Muungano ziliweka bayana mfumo ambao serikali kuu
na serikali shiriki katika Muungano kuwa na nguvu zinazoendeana, yaani,
mfumo wa shirikisho ambao kuna mgawiko wa mahakama, baraza la kutunga
sheria na urais baina ya serikali kuu na serikali mbili au zaidi, na
kila serikali ikiwa na nguvu kamili ndani ya mamlaka yake.”[5]
Mheshimiwa Mwenyekiti,
Aina ya dola iliyotokana na Hati ya Makubaliano ya Muungano
haikuwahangaisha waasisi wa Muungano ama viongozi wake wakuu peke yao.
Hata ndani ya makorido ya mamlaka, mjadala juu ya suala hili umekuwa
mkubwa na umeundiwa Tume na Kamati mbali mbali za kulichunguza. Kwa
mfano, hata kabla ya kuchapishwa kwa Uongozi Wetu na Hatima ya Tanzania
na The Partner-ship, tarehe 6 Aprili, 1992, Rais wa Zanzibar na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Zanzibar, Dk. Salmin Amour aliunda
Kamati ya Baraza la Mapinduzi ya Kujenga Hoja Juu ya Masuala ya Muungano
wa Tanzania, maarufu kama Kamati ya Amina Salum Ali kutokana na jina la
Mwenyekiti wake. Mheshimiwa Ali Juma Shamuhuna, ambaye ni mjumbe wa
Bunge hili Maalum, alikuwa Katibu wa Kamati hiyo.
Pamoja na
mambo mengine, Kamati ya Amina Salum Ali ililichunguza suala la aina ya
Muungano uliozaliwa na Hati ya Makubaliano ya Muungano. Jibu la Kamati
hiyo lilikubaliana na nusu ya hoja ya Mwalimu Nyerere na nusu ya hoja ya
Alhaj Aboud Jumbe: “... Muungano wa Tanzania, haidhuru unaitwa ‘Union’,
lakini uko kati na kati baina ya ‘Union’ na Shirikisho. Kuwepo kwa
Serikali ya Muungano yenye madaraka makubwa ni kielelezo cha sura ya
‘Union’. Sura hii inazidi kutiliwa nguvu na kile kitendo cha Tanganyika
kuvua madaraka yake yote na kuyaingiza katika Serikali ya Muungano. Kwa
upande mwengine kuwepo kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar yenye
madaraka kamili Zanzibar juu ya mambo yote yasiyokuwa ya Muungano, ni
kielelezo dhahiri cha sura ya Shirikisho. Kwa hivyo, Muungano huu ni wa
aina yake.”[6]
MTAZAMO WA KITAALUMA
Mheshimiwa Mwenyekiti,
Hati ya Makubaliano ya Muungano wa Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya
Watu wa Zanzibar imejadiliwa sana na kwa miaka mingi katika ulingo wa
kitaaluma. Mjadala huu umehusu, kwa kiasi kikubwa, aina na muundo wa
Muungano huu. Katika kitabu chake Tanzania: The Legal Foundations of the
Union, kilichochapishwa kwa mara ya kwanza mwezi Januari, 1990, Profesa
Issa Shivji alisema, baada ya uchambuzi wa kina wa Hati ya Muungano,
kwamba Makubaliano ya Muungano yalitengeneza katiba ya shirikisho. Kwa
mujibu wa Profesa Shivji, katiba za shirikisho zina sifa kuu zifuatazo
ambazo alisema zipo katika Hati ya Muungano:[7]
a. Kuna mgawanyo wa wazi wa madaraka kati ya serikali kuu na serikali za sehemu za muungano ambayo yapo katika ngazi moja;
b. Mamlaka ya serikali kuu yaliyowekewa mipaka ya wazi wakati mamlaka
yaliyobaki yako mikononi mwa serikali za sehemu za muungano;
c.
Serikali zote, yaani serikali kuu na serikali za sehemu za muungano
zinagusa maisha ya wananchi wao moja kwa moja tofauti na serikali ya
mkataba (confederation) ambako serikali za sehemu ndizo zinazogusa
maisha ya wananchi moja kwa moja.[8]
Kwa maneno ya Profesa
Shivji, kwa kuyaangalia Makubaliano ya Muungano kutoka upande wa
Zanzibar na Tanganyika na kwa ujumla wao, “... msingi wa shirikisho ndio
wenye nguvu na Makubaliano ya Muungano yanaweza kutafsiriwa kwa usahihi
kama katiba ya shirikisho.”[9] Kwingineko katika kitabu hicho, Profesa
Shivji alidai kwamba: “Kwa vyovyote vile, ni wazi kwamba Makubaliano ya
Muungano sio katiba ya muungano (unitary constitution).”[10]
No comments:
Post a Comment