WEKUNDU wa Msimbazi, Simba wamekamilisha usajili wa kipa namba moja wa Mtibwa Sugar, Hussein Sharrif `Iker Casillas` na kumsainisha mkataba wa miaka miwili.
Kwa muda mrefu Simba ilionesha nia ya kumsajili mlinda mlango huyo bora wa ligi kuu soka Tanzania bara msimu uliopita, lakini ilimkosa mara kadhaa na sasa ndoto zimetimia.
Casillas aliyekuwa tegemeo katika klabu ya Mtibwa Sugar ameungana na makipa Ivo Mapunda na Abuu Hashim katika kikosi cha Simba.
Simba ilimtema kipa wake, Mghana, Yaw Berko baada ya kumalizika kwa msimu wa 2013/2014 wa ligi kuu Tanzania bara, hivyo kubakiwa na makipa wawili tu.
Kusajiliwa kwa Casillas ambaye aliwahi kuitwa katika kikosi cha Taifa stars chini ya Kim Poulsen kutaleta upinzani mkubwa baina yake na kipa namba moja wa Simba, Ivo Mapunda.
Uwezo mkubwa aliouonesha kwa wakati wote akiidakia Mtibwa Sugar, Casillas anatarajiwa kuisaidia Simba inayohitaji mafanikio msimu ujao.
Wakati huo huo, Simba imemsainisha kipa kinda, Peter Manyika Junior ili ajiunge na Simba B.
Kipa huyo ni mtoto wa kipa wa zamani wa Yanga na timu ya Taifa ya Tanzania, Peter Manyika senior.
Usajili huo ulisimamiwa na makamu wa rais wa Simba, Geofrey Nyange Kaburu akishirikiana na mjumbe wa kamati ya usajili inayoongozwa na Zacharia Hans Poppe, bwana Said Tully.
Mbali na kipa huyo, pia Simba imemsajili beki kinda wa Mwadui ya Shinyanga, Ibrahim Hajibu Migomba ikiwa ni sehemu ya mikakati ya kuimarisha kikosi B.
Moja ya ahadi za Kaburu ni kujenga soka la vijana katika klabu hiyo na hata alipokuwa sehemu ya uongozi wa Ismail Aden Rage alifanya jitihada ya kuijenga Simba B iliyozalisha akina Ramadhan Singano `Messi`, Haruna Chanongo, Said Ndemla na wengineo.
Wachezaji wote hao wawili wamesainishwa mikataba ya miaka mitatu na watakuwa wanakomazwa wakiwa kikosi B na watakapokuwa tayari watapandishwa kikosi B.
Mwenyekiti wa kamati ya Usajili ya Simba, Zacharia Hans Poppe alikuwa nchini Brazil na kulitokea taarifa kuwa amekwenda kusaka kifaa ili kuwalipa wapinzani wao Yanga walioajiri wabrazil watatu akiwemo kiungo mshambuliaji, Andrey Coutinho.
Poppe alikaririwa akisema ameenda kuangalia kombe la dunia na si vinginevyo.
Akaongeza kuwa mambo yao yanafanywa kimya kimya. Bila shaka kuna usajili mwingine mkubwa upo njiani.
No comments:
Post a Comment