Pages

Wednesday, April 30, 2014

RAIS KIKWETE ATUMA SALAMU ZA RAMBI RAMBI KWA MKUU WA MKOA WA SINGIDA KUFUATIA VIFO VYA WATU 19

THE UNITED REPUBLIC OF TANZANIA
DIRECTORATE OF PRESIDENTIAL COMMUNICATIONS

Telephone : 255-22-2114512, 2116898
E-mail : ikulumawasiliano@yahoo.com
E-mail : press@ikulu.go.tz
Fax : 255-22-2113425

Rais wa Jamhuri ya Muungano waTanzania, Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete amemtumia Salamu za Rambirambi Mkuu wa Mkoa wa Singida, Mheshimiwa Perseko Kone kufuatia vifo vya watu 19 wakiwemo Askari Polisi wanne (4) na Viongozi watatu wa Kijiji kufuatia ajali ya barabarani iliyosababishwa na basi lililokuwa likitokea Kigoma kuelekea Dar es Salaam katika Barabara kuu ya Singida - Dodoma.

Ajali hiyo ilitokea usiku wa tarehe 27 Aprili, 2014 katika Kijiji cha Utaho, Wilaya ya Ikungi Mkoani Singida baada ya basi la Kampuni ya Sumry lenye Nambari ya Usajili T. 799 BTE aina ya Nissan kuwagonga watu waliokuwa wamekusanyika katika eneo ambapo ajali nyingine ilikuwa imetokea wakiwa pamoja na Askari Polisi kutoa msaada katika ajali nyingine iliyokuwa imetokea katika eneo hilo ambapo mwendesha baiskeli aligongwa na lori na kufariki papo hapo.

“Nimepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za vifo vya watu 19 wakiwemo Askari Polisi wanne na Viongozi watatu wa Kijiji cha Utaho katika Wilaya ya Ikungi Mkoani Singida.  Vifo hivi vimetupotezea kama Taifa nguvu kazi muhimu kwa ujenzi wa nchi yetu na hakika vimeacha simanzi na huzuni kubwa kwa familia, ndugu, jamaa na marafiki wa Marehemu”, amesema Rais Kikwete katika Salamu zake.



Rais Kikwete amemuomba Mkuu wa Mkoa wa Singida, Mheshimiwa Perseko Kone kumfikishia Salamu zake za Rambirambi na pole nyingi kwa watu wote waliopotelewa na ndugu na jamaa zao kutokana na ajali hiyo, na amewahakikishia wafiwa kuwa yuko pamoja nao katika kuomboleza msiba huo mkubwa.

“Ninamuomba Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema awawezeshe kupona haraka na kurejea katika hali zao za kawaida watu wote waliojeruhiwa katika ajali hiyo ili waweze kupona haraka na kuungana tena na ndugu na jamaa zao”, amemalizia kusema Rais Kikwete katika Salamu zake.


Imetolewa na;

Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu – Dar es Salaam.
30 Aprili,2014

No comments:

Post a Comment