Kazi ya ulazaji wa bomba la gesi chini
ya bahari kutoka katika kisiwa cha Songo songo kupitia Somangafungu hadi
Dar es salaam inatarajia kukamilika mwezi Juni mwaka huu.
Mbali na mradi wa bomba la gesi
kunufaisha nchi kuondokana na adha ya kukosa umeme wa uhakika pia
ufungua fursa za ajira ikiwa ni pamoja na huduma za jamii kwa wakazi
wanaoishi karibu na mradi huo.
Akizungumza na ujumbe wa makatibu wakuu
ukiongozwa na Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue Meneja Mradi wa
Tanzania Natural Gas Transportation Pipeline Bw. Kapuulya Musomba
aliuambia ujumbe huo kuwa bomba hilo lenye uwezo wa kuzalisha futi za
ujazo milioni 140 linatarajiwa kukamilika mwezi ujao
Futi za ujazo milioni 140
zitaunganishwa na nyingine 210 zilizopo Somangafungu na kuongeza kuwa
mradi utakapokamilika utakuwa na uwezo wa kuzalisha futi za ujazo
milioni 750.
Naye Sultani Pwaga mtalamu kutoka
Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC) ambaye ni msimamizi wa mradi
alisema ujenzi wa kituo cha kusafisha gesi cha Madimba umeleta neeema
kubwa kwa wakazi wa eneo la Madimba kwa kufungua fursa nyingi ikiwa ni
pamoja na ajira.
“Kwa mfano wakati wa ujenzi wa kituo
hiki takribani vijana 350 waliajiriwa ambao wamekuwa wakinufaika na
kipato kinachotokana na mradi huu.” Alilisitiza Bw. Pwaga.
Bw. Pwaga alisema kuwa faida nyingine
itakayopatikana ni pamoja na ajira 60 kwa wataalamu watakaofanya kazi
katika kituo cha kusafisha gesi na kuongeza kuwa kipaumbele kitatolewa
kwa wakazi wa Madimba.
Aliongeza kuwa wafanyakazi 30 watafanya
kazi kwa siku 28 na kupumzika na wengine 30 kuendelea na kazi kwa siku
28 wengine wanapokuwa likizo kutokana na sababu za kimazingira.
Aidha Bw. Pwaga aliongeza kuwa
kumejengwa nyumba za kuishi wafanyakazi zenye uwezo wa kubeba
wafanyakazi 60 na wageni 26 na kusisitiza kuwa wafanyakazi wataishi
kwenye nyumba zao kutokana na kwamba mitambo hiyo inaendeshwa kwa masaa
24 kwa siku saba.
Bw. Pwaga aliongeza kuwa vyumba vingine 24 ni kwa ajili ya wageni mbalimbali wanaotembelea kituo hicho.
Akizungumzia muda wa kuwasili kwa
mitambo hiyo Bw. Pwaga alisema mitambo itawasili kabla ya mwezi Juni,
2014 na mradi unatarajiwa kukamilika mapema Desemba mwaka huu.
Aliongeza kuwa mitambo hiyo kwa sasa inatengenezwa Ujerumani, Canada, Australia na China.
Imeandaliwa na:
Greyson Mwase,
Afisa Habari,
Wizara ya Nishati na Madini,
754/33 Mtaa wa Samora
S.L.P 2000 Dar es Salaam
Tel: +255-22-2121606/7, Fax: +255-22-2121606
Email:info@mem.go.tz
Tovuti: www.mem.go.tz
No comments:
Post a Comment