Wakala wa Jiolojia Tanzania (GST) umeshiriki vyema Maonesho na
mkutano wa Kimataifa wa Madini maarufu kama Prospectors and Developers
Association Convection (PDAC) yaliyofanyika Toronto Canada mnamo mwezi
Machi mwaka huu na kuweza kuvutia wawekezaji wengi katika Sekta ya
Madini.
Akielezea ushiriki wa GST katika maonesho hayo, Mtendaji Mkuu wa
Wakala wa Jiolojia Tanzania, Prof. Abdulkarim Mruma amesema kuwa
Maonesho hayo yametumika kama njia mojawapo ya kusambaza takwimu na
taarifa za jiosayansi za kiwango bora kwa gharama stahili kwa wadau nje
ya nchi ili kuongeza ufahamu wa rasilimali za madini zinazopatikana
Tanzania na hivyo kuiwezesha sekta ya madini kuchangia ipasavyo katika
ukuaji wa uchumi wa nchi.
“Hakuna mwekezaji yeyote duniani anayeweza kuwekeza katika sekta
yeyote hususani ya madini bila kuwa na taarifa sahihi za upatikanaji wa
madini, GST imeshiriki maonesho na mkutano huu kama njia ya
kuwafahamisha wadau juu ya uwepo wa takwimu, taarifa na mazingira mazuri
ya uwekezaji nchini Tanzania”. Alisema Profesa Mruma.
Mtendaji Mkuu wa GST alieleza kuwa, pamoja na taarifa mbalimbali za
jiosayansi zilizokuwa zikitolewa kwenye maonesho hayo, Wakala pia
ulichukua fursa hiyo kuwafahamisha wadau walioshiriki mkutano na
maonesho hayo juu ya uwepo wa taarifa mpya zilizotokana na utafiti wa
jiofizikia wa kutumia ndege uliokamilika hivi karibuni na mwezi Januari
mwaka huu.
Prof. Mruma aliongeza kuwa, GST kama mhamasishaji mkubwa wa uwekezaji
Sekta ya Madini kwa kushirikiana na Wizara ya Nishati na Madini
itaendelea kutekeleza kazi zake kwa weledi ili kuhakikisha taarifa za
upatikanaji wa madini zinawafikia wadau kwa wakati.
Mtendaji Mkuu huyo alitoa wito kwa wadau wote wa ndani na nje ya
nchi kutumia taarifa na wataalam wa GST ili kuongeza ufanisi na tija
katika shughuli zao za utafiti na uchimbaji wa madini.
Naye Kaimu Mkurugenzi wa Kazidata(Database) na Mratibu wa mradi wa
SMMRP (GST), Bi Yorkbeth Myumbilwa aliongeza kuwa serikali kupita Wizara
ya Nishati na Madini imeamua kwa dhati kuendeleza Sekta ya Madini
nchini kwani iliwekeza fedha nyingi kwenye mradi wa utafiti wa
jiofizikia ili kubaini maeneo mapya yenye madini ili kuvutia wawekezaji
wa ndani na nje ya nchi.
Bi Myumbila alitoa angalizo kuwa uwekezaji mkubwa katika mradi wa
utafiti wa jiofizikia utakuwa hauna maana endapo taarifa na takwimu
zilizopatikana hazitawafikia wadau mbalimbali hivyo ushiriki wa GST
katika maonesho ya Canada ni utekelezaji wa lengo la Serikali la
kusambaza matokeo ya tafiti (taarifa za jiosayansi) kwa wadau ili
kuongeza uwekezaji Sekta ya Madini.
Naye Afisa Biashara wa GST, Priscus Benard ameeleza kuwa Wakala wa
Jiolojia Tanzania (GST) umepewa majukumu ya kukusanya, kuchambua,
kutafasiri, kuchapisha, kusambaza na kutunza takwimu na taarifa za
kijiosayansi (jiolojia, jiokemia na jiofizikia) ambazo ni muhimu katika
ufahamu wa kuwepo kwa madini mbalimbali nchini na njia bora za kutafuta
na kuchenjua madini.
“GST inafanya uchunguzi wa kimaabara kwa sampuli za miamba, madini,
mchanga, maji, mimea na udongo kwa ajili ya tafiti mbalimbali na kutoa
huduma za kimaabara kwa wadau wa ndani na nje ya nchi pamoja na kufanya
utafiti wa uchenjuaji wa madini”.Alisema Bw Priscus.
Bw. Benard amesema kuwa matokeo ya tafiti huwekwa kwenye ramani za
kijiosayansi zinazoainisha kuwepo kwa aina ya miamba, madini na
mazingira ya kijiosayansi (geoscientific environment) katika sehemu
mbalimbali za nchi yetu na kuzisambaza taarifa na takwimu hizo kwa wadau
ili ziweze kutumika katika sekta mbalimbali za uchumi. Pia matokeo ya
tafiti huchapishwa kama vitabu, vijarida, na vipeperushi na kusambaza
kwa wadau mbalimbali wa sekta ya madini na sekta nyingine.
Wakala wa Jiolojia pia umepewa jukumu la kuratibu majanga ya asili ya
kijiolojia, matetemeko ya ardhi, milipuko ya volcano, maporomoko ya
ardhi, mionzi asilia, kemikali zitokanazo na fukuto la volcano, mashimo
ya asili ya kijiolojia) na kutoa ushauri wa namna bora ya kujikinga
na/au kupunguza athari zake.
No comments:
Post a Comment