Mwenyekiti Mwenza wa Umoja wa Katiba ya Wananchi na Mjumbe wa Bunge la
Katiba, Profesa Ibrahim Lipumba akisalimiana na wananchi kwenye Viwanja
vya Kibanda Maiti Zanzibar jana, baada ya kuwasili Visiwani humo kwa
ajili ya mkutano wa hadhara ambao haukufanyika baada ya Jeshi la Polisi
kuzuia
Wakizungumza na wanahabari mjini Zanzibar
jana, viongozi wa umoja huo walisema kuwa wataeleza namna CCM
inavyopinga mawazo ya wananchi kwenye Bunge hilo, yaliyomo katika Rasimu
ya Katiba iliyowasilishwa kwa mujibu wa sheria na aliyekuwa Mwenyekiti
wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba.
Katika mkutano huo uliokuwa chini ya Mwenyekiti
wake Profesa Ibrahim Lipumba kwa lengo la kuuelezea umma kuhusu uamuzi
wao wa kutoka katika Bunge Maalumu la Katiba linaloendelea mjini Dodoma,
umoja huo ulisema hauwezi kufanya maridhiano wakidai kuwa CCM siyo
wakweli na wanafiki.
“Tunasikia kwamba juhudi zinafanywa ili kuwepo kwa
maridhiano, lakini sisi hatuna nafasi hiyo, bali tunajiimarisha
kuhamasisha wananchi kuhusu mawazo yao,” alisema Mwenyekiti wa
Chadema, Freeman Mbowe ambaye pia ni kiongozi wa umoja huo.
Alifafanua kwamba mpango wao wa sasa ni kuonana na
wananchi, lakini siyo kuzungumza na watu aliosema hawako tayari
kutengeneza Katiba ya wananchi bali kwa masilahi ya chama chao.
Mbowe alisema kuwa wanaodai kuwa Ukawa wana mvurugano ni watu walioishiwa mawazo akiwataka wananchi wasiamini propaganda hizo.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa NCCR –Mageuzi,
James Mbatia alieleza kwamba kuna watu wanaopita na kutangaza kwamba
ukipitishwa mfumo wa Muungano wa serikali tatu ni kuleta dola ya
Kiislamu Zanzibar.
“Hatuna haja hiyo, wasiitumie kudanganya umma kwa
masilahi yao. Sisi tutawaeleza wananchi yote kuhusu fitina zao,”
alisema Mbatia.
Katika hatua nyingine Mbowe amesema kuwa CCM
inaeneza ubaguzi kwa kusema kuwa Wapemba wakifukuzwa Tanzania Bara,
hawatakaa Unguja na kwamba jambo ambalo Ukawa inaliona siyo sahihi.
“Sisi hatutaki ubaguzi kwa sababu ni wamoja na
Serikali tatu wananchi walizipendekeza wakiamini kwamba zitajenga
Muungano ulio imara,” alisema Mbowe.
Umoja huo ulitoka nje ya vikao vya Bunge la Katiba
kwa kile walichodai kuendelezwa ubaguzi na matusi katika mtiririko wa
uchangiaji pamoja na kutosikilizwa kwa hoja za msingi zinazotolewa na
walio wachache kwa manufaa ya taifa huku CCM iking’ang’ania hoja zake
kwa masilahi binafsi.
No comments:
Post a Comment