Rais wa Marekani, Barack Obama (kulia) na rais mstaafu wa nchi hiyo, George Bush wakisalimiana na wanafamilia wa jamaa waliopoteza maisha katika tukio la kupigwa bomu jengo la ubalozi wa Marekani jijini Dar es Salaam mwaka 1998. Obama alikutana na wanafamilia hao alipofanya ziara nchini Julai mwaka jana.
Habari kamili
Nairobi/Dar. Watanzania wanne waliojeruhiwa katika mlipuko wa bomu katika ubalozi wa Marekani mwaka 1998 na wengine watano waliofariki dunia katika mlipuko huo watalipwa fidia ya Sh672 bilioni, kiwango ambacho ni sawa na bajeti ya wizara nne za Tanzania.
Watanzania hao waliuawa na wengine kujeruhiwa
katika moja ya mashambulizi pacha yaliyotokea kwa wakati mmoja jijini
Dar es salaam na Nairobi, Kenya na ambayo yaliratibiwa na Osama Bin
Laden akitumia mtandao wa kundi la Al Qaeda mwaka 1998 kwenye ofisi za
balozi za Marekani.
Katika mashambulizi hayo yaliyotokea saa 4:00
asubuhi Agosti 7, 1998, Wakenya 200, Watanzania 10 na Wamarekani 12
walipoteza maisha na pia magaidi wawili nao walikufa.
Kati ya Watanzania 10, ni kesi za watu wanne tu waliouawa tu zilizofunguliwa kudai fidia ya watu hao kupoteza maisha.
Jaji wa Mahakama Kuu ya Marekani, Thomas Bates
alitoa hukumu hiyo wiki iliyopita, akiagiza pia kwamba serikali za Iran
na Sudan lazima zilipe jumla ya Dola za Marekani 957 milioni (Sh1.53
trilioni) kwa Watanzania hao na Wamarekani 23 waliouawa au kujeruhiwa
katika mashambulizi pacha ya kigaidi.
Jaji Bates alisema kiasi cha Dola 488 milioni za
Marekani (Sh780.8 bilioni) kitalipwa kwa Wamarekani 12 waliouawa na
familia zao. Dola 420 milioni za Marekani (Sh672 bilioni) zitalipwa kwa
Watanzania wanne waliojeruhiwa katika mlipuko na Watanzania watano
waliuawa katika shambulio hilo. Dola milioni 49 (Sh78.4 milioni)
zitalipwa kwa raia wawili wa Marekani waliojeruhiwa katika milipuko
hiyo.
“Milipuko ya mabomu katika balozi hizo mwaka 1998
iliwaathiri wanaoshtaki katika kesi hii, “Jaji Bates aliandika. Kupitia
simulizi zao binafsi, inaonyesha kwamba hata zaidi ya miaka 15 baadaye
kila mmoja bado ana kumbukumbu za kutisha za siku hiyo.
“Fidia hii haiwezi ikarudisha maisha ya wale
waliokufa wala waliopata madhara. Badala yake, ni ya kutoa tu kifuta
machozi. Lakini hiyo ni kidogo sana kwa wale wanaoshtaki.”
Hata hivyo, uamuzi wa Jaji Thomas Bates haujaeleza fedha hizo zitalipwa lini kwa waathirika hao.
Kiwango cha Sh672 bilioni ni sawa na bajeti za
Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki ambayo katika mwaka wa fedha
wa 2013/14 ilitengewa Sh20.4 bilioni, Habari, Vijana, Utamaduni na
Michezo (Sh21.3 bilioni), Uchukuzi (Sh491.1 bilioni ) na Wizara ya Mambo
ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa iliyotengewa Sh138.3 bilioni.
Thomas Fay, wakili aliyewawakilisha Watanzania na
Wamarekani, alisema kuwa juhudi zinazotakiwa sasa ni kuanza kutambua
mali za Iran na Sudan ambazo zinaweza kutaifishwa ili kulipa fidia hiyo.
Mwanasheria Mkuu wa Washington alisema kuwa hukumu
ya Jaji Bates ni hatua muhimu katika kuhakikisha kuwa Wamarekani na
Watanzania walioathirika kwa ugaidi huo wanapata haki kwa mateso
waliyoyapata.
Sudan na Iran zilihusishwa katika hukumu Jaji Bates kwa sababu ya serikali zao zilitoa msaada kwa Osama Bin Laden kufanikisha shambulio hilo kwa kutumia mtandao wa kundi la al-Qaeda.
Chanzo: Mwananchi
Sudan na Iran zilihusishwa katika hukumu Jaji Bates kwa sababu ya serikali zao zilitoa msaada kwa Osama Bin Laden kufanikisha shambulio hilo kwa kutumia mtandao wa kundi la al-Qaeda.
Chanzo: Mwananchi
No comments:
Post a Comment