Mbunge wa Jimbo la Nzega Mkoani Tabora kupitia CCM, Hamis Kigwangala.
MBUNGE wa jimbo la Nzega Mkoani
Tabora kupitia CCM, Hamis Kigwangala, ametanabaisha kuwa anatafakari
kama anaweza kugombea Urais kwenye uchaguzi mkuu ujao kupitia chama cha
mapinduzi CCM.
Akijibu maswali ya waandishi wa habari waliotaka kujua fununu zilizo
enea kwenye baadhi ya mitandao ya kijamii ambayo imekuwa ikiibua
mijadala mara kwa mara inayomshawishi kugombea Urais mwaka 2015, Dk.
Kigwangala amesema anatafakari jambo hilo zito na kuongeza kuwa muda
utakapofika atayazingatia maoni ya wananchi.
Akizungumzia maelezo kwamba haoni kama ni hatari kwake kutangazwa
mapema kwamba anataka kuwa kugombea Urais ni kujipunguzia sifa katika
chama chake, Dk. Kigwangala alisema yeye hajatangaza kama anataka Urais
na wala hajamtuma mtu kuanza kumfanyia kampeni, kwani watanzania
wanaongozwa na katiba yenye Uhuru wa kujieleza na kutoa maoni, hivyo
hayo ni mawazo yao na wana haki ya kufanya hivyo na yeye binafsi hawezi
kuwapinga.
Hivi karibuni kumeibuka mijadala mizito kwenye mitandao ya kijamii na
baadhi ya wanaharakati kutengeneza vuguvugu la kumshawishi Dk.
Kigwangala kuchukua fomu ya kugombea Urais wa Jamhuri ya muungano wa
Tanzania ifikapo mwaka 2015.
Mijadala hiyo mizito imeanzishwa katika mitandao ya Internet na simu
za mkononi walio ipachika jina "Citizens for Kigwangala" ambapo katika
mijadala hiyo wamekuwa wakishawishiana na kumwagia sifa Dk Kigwangala
kwamba ndiye kiongozi pekee anayefaa kuwakilisha chama cha Mapinduzi
katika uchaguzi mkuu ujao.
Baadhi ya vijana wamekuwa wakijadili kuwa Dk Kigwangala ndiye
anayeweza kuleta upinzani wa kweli kwa vyama vya upinzani, wakijenga
hoja kuwa amekuwa na misimamo na uwezo wa kujieleza kwa ufasaha ndani ya
vikao vya bunge.
Dk Kigwangala ni mbunge wa jimbo la Nzega mkoani Tabora, mwenye
taaluma ya udaktari wa tiba ambaye pia ni mwenyekiti wa kamati ya kudumu
ya bunge ya tawala za mikoa na serikali za mitaa.
No comments:
Post a Comment