Mwenyekiti wa Chama cha Walemavu Tanzania, (Chawata), Shida
Salum, yuko katika chumba cha wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalumu
(ICU) katika Hospitali ya Ami, Masaki, Dar es Salaam akisumbuliwa na
maradhi ya saratani.
Shida ambaye ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema na
mama mzazi wa Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe amelazwa tangu
juzi. Alianza kusumbuliwa na maradhi hayo mapema Agosti mwaka jana
lakini hali yake ilibadilika mapema mwaka huu akiwa mjini Dodoma
akisubiri kuapishwa pamoja na wajumbe wengine wa Bunge Maalumu la
Katiba.
Akizungumza hospitalini hapo jana, Zitto alisema
baada ya hali ya mama yake kuwa mbaya alishindwa kuendelea kukaa Dodoma
kusubiri kuapishwa na alipelekwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili
(MNH), ambako aligundulika kuwa na saratani ya shingo ya kizazi na
kupatiwa tiba kwa mwezi mmoja kabla ya kupelekwa India kwa matibabu
zaidi.
Alisema kabla ya kupelekwa hospitalini hapo,
alikuwa akiendelea kupata matibabu akiwa nyumbani, lakini hali yake
ilibadilika juzi.
Zitto alisema hali ya mama yake haijatengemaa
tangu aanze kusumbuliwa na maradhi hayo. Alisema kutokana na maradhi
hayo ya mama yake, ameshindwa kuhudhuria Bunge la Bajeti linaloendelea
mjini Dodoma.
“Hali ya mama kwa kweli siyo nzuri, lakini nina
imani itakuwa nzuri na kuendelea na shughuli za ujenzi wa taifa kama
zamani,” alisema Kabwe.
Tangu kuanza kwa Bunge la Bajeti, Zitto alionekana
Dodoma mara moja tu, siku ilipowasilishwa Ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti
Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
No comments:
Post a Comment