Pages

Sunday, May 18, 2014

TAIFA STARS YAICHAPA ZIMBABWE 1-0 LEO

Mshambuliaji wa timu ya Taifa ya Tanzania, Mbwana Samatta (juu) akikwepa kwanja wakati akijaribu kumtoka beki wa timu ya Taifa ya Zimbabwe, katika mchezo wa kwanza wa mchujo kuwania kupangwa kwenye makundi ya kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Mataifa ya Afrika 2015 zinazotarajia kufanyika nchini Morocco, wakati wa mtanange huo uliopigwa kwenye uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam. Katika mchezo huo Taifa Stars, ilishinda bao 1-0.

Mshambuliaji wa Taifa Stars,Mrisho Ngassa akijaribu kumtoka mchezaji wa timu ya Zimbabwe.
TIMU ya soka ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars leo imeiichapa timu ya Taifa ya Zimbabwe bao 1-0, katika mchezo wa kwanza wa mchujo kuwania kupangwa kwenye makundi ya kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Mataifa ya Afrika 2015 zinazotarajia kufanyika nchini Morocco, wakati wa mtanange huo uliopigwa kwenye uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.

katika mchezo huo uliochezeshwa na mwamuzi, Joseph Odartei Lamptey aliyesaidiwa na Malid Alidu Salifu na David Laryea wote wa Ghana, hadi mapumziko Taifa Stars walikuwa mbele kwa bao hilo 1-0, lilofungwa na John Boko katika dakika ya 13 na kudumu hadi mwisho wa mchezo huo.


John Bocco ‘Adebayor’ alifunga bao hilo akiunganisha kwa guu la kushoto krosi maridadi ya mshambuliaji wa TP Mazembe ya DRC, Thomas Ulimwwengu.


Kocha wa Tanzania, Mholanzi Mart Nooij alisema baada ya mchezo huo kwamba vijana wake wamecheza vizuri, lakini wangeweza kupata mabao zaidi kama wangetumia vizuri nafasi walizotengeneza.



Kwa upande wake, kocha mzalendo wa Zimbabwe, Ian Gorowa alisema vijana wake walicheza vizuri, lakini walikosa bahati ya kupata mabao licha ya kutengeneza nafasi zaidi ya tatu nzuri.


 Kikosi cha Tanzania kilikuwa; Deo Munishi ‘Dida’, Shomary Kapombe, Oscar Joshua, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Kevin Yondan, Frank Domayo/Amri Kiemba dk71, Mrisho Ngassa/Haroun Chanongo dk77, Mwinyi Kazimoto, John Bocco/Khamis Mcha ‘Vialli’ dk85, Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu. 


Zimbabwe; George Chigova, Partson Jaure, Danny Phiri, Hardlife Zvirekwi, Stephen Alimenda, Rendai Ndoro, Milton Ncube, Kudakwashe Mahachi, Cuthbert Malajila, Peter Moyo na Eric Chipeta.


Katika mechi nyingine jana, mabao mawili ya Frank ‘Gabadinho’ Mhango yaliipa Malawi ‘The Flames’ ushindi wa 2-0 dhidi ya Chad Uwanja wa Kamuzu mjini Blantyre, nao Sao Tome Principe walifungwa 2-0 nyumbani na Benin, Namibia iliilaza 1-0 Kongo na Mauritania iliibwaga 1-0 Equatorial Guinea.


Mechi nyingine zilizotarajiwa kuchezwa ni kati ya Jamhuri ya Afrika ya Kati na Guinea Bissau, Swaziland na Sierra Leone, Msumbiji na Sudan Kusini, Madagascar na Uganda, Burundi na Botswana, Liberia na Lesotho, Kenya na Comoro na Libya vs Rwanda.


Na mechi za marudiano zinatarajiwa kuchezwa  mwisho wa wiki ya mwezi Mei 30 na washindi wataingia kwenye hatua ya mwisho ya mchujo ili kuwania kupangwa kwenye makundi tayari kwa mbio rasmi za Morocco 2015.

No comments:

Post a Comment