Rais Jakaya Kikwete
Katika maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani yaliyofanyika
kitaifa jijini Dar es Salaam, Rais Jakaya Kikwete katika hotuba yake kwa
Taifa alitoa ahadi kwa wafanyakazi katika maeneo mawili makubwa.
Kwanza aliahidi kuongeza mishahara ya wafanyakazi.
Pili aliahidi kupunguza kodi inayokatwa kwenye mishahara hiyo kwa
kiwango cha kuridhisha na kusema kwamba utekelezaji wa ahadi hizo
utaanza katika Bajeti ya mwaka 2014/15 inayotarajiwa kuwasilishwa
bungeni hivi karibuni.
Tamko hilo la Rais bila shaka litakuwa limepokewa
na wafanyakazi wote kwa furaha isiyo kifani. Pamoja na ukweli kwamba
Serikali imekuwa ikitoa ahadi nyingi kwa wafanyakazi na baadaye
inashindwa kuzitekeleza, mara hii Rais ameonekana kuguswa binafsi na
hali mbaya waliyonayo wafanyakazi na kuamua kuingilia kati pale alipoona
kuna mivutano isiyokuwa ya lazima kati ya wizara mbili zinazohusika na
masuala ya wafanyakazi.
Maelezo ya Rais Kikwete yanatoa picha kuwa, kumbe utekelezaji wa nyongeza za mishahara na upunguzaji wa kodi zinazokatwa katika mishahara hiyo limekuwa likikwamishwa na Wizara ya Fedha. Kwa maelezo yake mwenyewe, pamekuwapo na ubishi na mvutano mkubwa kati ya wizara za Fedha na Utumishi kuhusu viwango vya nyongeza za mishahara na punguzo la kodi kwenye mishahara hiyo kwa mwaka ujao wa fedha. Wakati Wizara ya Utumishi ilitaka viwango vya ongezeko la mishahara na punguzo la kodi viwe vya kuridhisha, Wizara ya Fedha, ikiungwa mkono na wafadhili ilitaka viwepo viwango vidogo vya ongezeko la mishahara na punguzo la kodi kwenye mishahara hiyo.
Kama siyo Rais Kikwete kuingilia kati na kuunga
mkono msimamo wa Wizara ya Utumishi, wafanyakazi wangeendelea kusikia
ngonjera na mashairi yaleyale ambayo wamekuwa wakiyasikia kutoka
serikalini kwa miongo kadhaa sasa. Tunampongeza Rais kwa kusimama katika
upande wa wavuja jasho na kutambua kwamba kuendelea kuwakamua hakuwezi
kuleta tija. Kama alivyosema Rais, hata kama mapato ya Serikali ni
madogo, lazima hicho kidogo kiendelee kutolewa kila mwaka ili kuleta
unafuu kwa wafanyakazi.
Sisi tunadhani dhamira hiyo mpya ya Serikali ya
kuanza kutimiza ahadi zake kwa wafanyakazi italeta uhusiano mzuri kati
ya pande hizo mbili ambazo zimekuwa zikizozana na kuvuana nguo hadharani
kutokana na kutoaminiana. Siyo siri kwamba uhusiano uliokuwapo kati ya
pande hizo mbili ulikuwa wa kuviziana kama ulivyo wa panya na paka. Hata
risala za wafanyakazi zilizosomwa kabla Rais hajatoa hotuba yake na
kutoa ahadi tulizotaja hapo juu, zilitoa shutuma na maneno makali kwa
Serikali kwa kutowajali wafanyakazi na kuwadhulumu haki zao.
Risala ya Shirikisho la Wafanyakazi Tanzania
(Tucta), iliikumbusha Serikali kwamba kumlipa mfanyakazi mshahara
unaokidhi mahitaji muhimu ya maisha siyo jambo la fadhila, bali ni
mojawapo ya haki za msingi za binadamu. Risala iliyosomwa mkoani Mbeya
iliitaka Serikali kuacha kuwanyonya wafanyakazi na pia kuacha kuwa
mwajiri msumbufu kuliko wengine nchini.
Risala hizo na nyingine nyingi zilizotolewa na
wafanyakazi wakati wa maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani
zinapaswa kuifumbua macho Serikali ili itambue kwamba jumuiya ya
wafanyakazi nchini siyo ya kupuuzwa. Itakuwa vyema iwapo Tucta
itafuatilia utekelezaji wa ahadi hizo za Rais Kikwete kwa wafanyakazi
ili ufunguliwe ukurasa mpya wa ushirikiano kati ya pande hizo mbili.
No comments:
Post a Comment