Pages

Wednesday, June 4, 2014

NAIBU MEYA WA JIJI LA ARUSHA APANDISHWA KIZIMBANI KWA KOSA LA SHAMBULIO

msofe300x169
NAIBU Meya wa Halmashauri ya Jiji la Arusha, Prospr Msofe (48) na Diwani wa kata ya Levolosi, Nanyaro Ephata (28) wamepanda kizimbani katika mahakama ya Wilaya ya Arusha / Arumeru, Mkoani Arusha, kujibu shitaka la shambulio la kudhuru mwili wa askari mgambo wa Jiji William Mollel.
Akisoma hati ya mashitaka mbele ya hakimu wa Mahakama hiyo, Patrisia  Kisinda,  Wakili wa serikali, Mary Lucas, alidai kuwa, washitakiwa wote kwa pamoja mnamo Aprili 16 mwaka huu, eneo la Levolosi,walimshambulia mgambo wa Jiji la Arusha kwa kumpiga kifuani.
 Aliendelea kudai kuwa baada ya kumshambulia walimsababishia maumivu makali maeneo mbalimbali ya mwili wake.
Washitakiwa walikana shitaka hilo na wapo nje kwa dhamana, baada ya kudhaminiwa na wadhamini wawili kila mmoja kwa ahadi ya shilingi milioni moja.
Baada ya kusoma wakili mashitaka hayo, hakimu Kisinda alisema wahitakiwa hao hawataruhusiwa kutoka nje ya Mkoa wa Arusha hadi kupata ruhusa ya Mahakama.
Pia alisema kwa kuwa washitakiwa ni watumishi wa serikali, endapo watakuwa na safari za kikazi, wafuate taratibu kwa kuandika barua na kuiwakilisha mahakamani ili kueleza anakwenda eneo lipi.
Awali kabla ya hakimu kuongea Naibu Meya Prosper Msofe, aliomba mahakama imwelekeze njia ya kufuata endapo atasafiri kikazi.
“Mheshimiwa hivi karibuni nitakuwa na ziara ya kikazi, naomba utaratibu wa mahakama natakiwa kufanyaje maana siwezi kuacha kufanya,”alisema.
Wadhamini waliomdhamini Naibu Meya Msofe ni Emmanuel Kessy, mkazi wa Kaloleni na Andrew  Mangi, mkazi wa Arusha na upande wa Diwani Nanyaro waliomdhamini ni  Kayusi Shao, mkazi wa Sombetini na Rayson Ngowi, mkazi wa Kimandolu.
Hata hivyo kesi hiyo ilikuwa na wadhamini zaidi ya 20 mahakaani hapo hali iliyosababisha kuzuka kwa mtafaruku wa kugombea kudhamini washitakiwa, baina ya wadhamini na hakimu kuingilia kati kwa kuwatuliza.
Kesi hiyo imeahirishwa itatajwa tena Julai 8 mwaka huu na washitakiwa wapo nje kwa dhamana.
Chanzo: Matukio na Vijana

No comments:

Post a Comment