Shirikisho
la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limepokea kwa masikitiko kifo cha
Mwakilishi wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Mara (FAM) katika Mkutano
Mkuu wa TFF, William Chibura kilichotokea leo asubuhi (Juni 3 mwaka
huu) katika Hospitali ya Mkoa wa Mara mjini Musoma.
Chibura
aliyezaliwa mwaka 1969 alikuwa mjumbe wa Mkutano Mkuu wa TFF
akiwakilisha klabu za Mkoa wa Mara kupitia FAM. Aliwahi kuichezea Musoma
Shooting, na baadaye kuwa kiongozi katika klabu hiyo na ile ya Polisi
Mara iliyoko Ligi Daraja la Kwanza (FDL).
Hadi
mauti yanamkuta alikuwa kiongozi wa Butiama FC, na mwakilishi wa klabu
Chama cha Mpira wa Miguu Wilaya ya Butiama (MUFA) kwenye Mkutano Mkuu wa
FAM.
Msiba
huo ni mkubwa katika fani ya mpira wa miguu nchini kwani, Chibura enzi
za uhai wake alitoa mchango mkubwa katika mchezo huu tangu akiwa
mchezaji na baadaye kiongozi.
TFF
tunatoa pole kwa familia ya marehemu Chibura, Chama cha Mpira wa Miguu
Mkoa wa Mara (FAM), Jeshi la Polisi Tanzania na kuwataka kuwa na subira
na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu cha msiba huo mzito.
Taratibu
za mazishi zinaendelea kufanywa na familia yake kwa kushirikiana na
Jeshi la Polisi Tanzania- Mkoa wa Mara, kwani marehemu Chibura alikuwa
mtumishi wa jeshi hilo. TFF tunasubiri taratibu hizo ili tujipange jinsi
ya kushiriki katika msiba huo.
Bwana alitoa, na Bwana ametwaa. Jina lake lihimidiwe. Amina
No comments:
Post a Comment