Pages

Thursday, July 10, 2014

TANZANIA NA ALGERIA WAJADILIANA KUANZISHA KAMPUNI YA UBIA

Tanzania na Algeria zinakamilisha majadiliano ya kuanzisha kampuni ya Ubia itakayohusika na ujenzi wa miundombinu ya kusambaza umeme na Kampuni ya Ubia ya kujenga mtambo wa kusindika gesi ya “Liquefied Petroleum Gas” (LPG) na kuiuza gesi kwa wananchi kwa kutumia mitungi.
Makubaliano hayo yamefikiwa katika ziara ya kikazi ya Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo na ujumbe wake nchini Algeria, ambayo inalenga kufuatilia utekelezaji wa makubaliano ya awali ya kushirikiana katika kubadilishana uzoefu kwenye masuala yanayohusu sekta za Nishati na Madini kufuatia Mkataba wa Makubaliano ya ushirikiano wa nchi hizo uliosainiwa tarehe 2 Disemba, 2013 nchini Algeria.
Kwa mujibu wa makubaliano ya mkutano baina ya Mawaziri wa Nishati na Madini wa Tanzania, Profesa Sospeter Muhongo na Waziri wa Nishati na Migodi wa Algeria Mhe. Youcef Yousfi, mawaziri hao wameyaagiza mashirika ya Umeme ya Tanzania (TANESCO) na Shirika la Umeme la Algeria (KAHRIF) kukamilisha majadiliano ya kuanzisha kampuni ya ubia ya ujenzi wa miundombinu ya kusambaza umeme.
Mkutano huo wa mawaziri, ulitanguliwa na kikao cha awali cha wataalamu wa nchi zote mbili, ambacho kiliongozwa na Kamishna Msaidizi anayeshughulikia masuala ya Umeme , Wizara ya Nishati na Madini, Mhandisi Innocent Luoga, ambacho kilijadili maeneo ya ushirikiano yanayohusu umeme, mafuta, gesi na madini.
Katika hatua nyingine, Mawaziri hao wameziagiza kampuni za mafuta na gesi likiwemo Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) na kampuni za mafuta na gesi za Algeria za NAFTAL na SONATRAC kukamilisha majadiliano ya kuanzisha kampuni ya ubia ya kujenga mtambo wa LPG na kuuza gesi hiyo kwa wananchi kwa kutumia mitungi, ambapo kampuni zote za ubia zimetakiwa kuanza kazi ifikapo Januari, 2015.
Wakati huo huo, Waziri Muhongo amekutana na Waziri wa Viwanda na Migodi wa Algeria Mhe. Abdessalem BOUCHOAREB ili kujadili maeneo ya ushirikiano katika sekta ya Madini ambapo wamezielekeza taasisi zinazohusika na madini za nchi hizo, kuandaa mpango wa utekelezaji wa ushirikiano katika kuwajengea uwezo wataalamu wa madini kubadilishana uzoefu na teknolojia, utafutaji na uendelezaji wa madini ya dhahabu, chuma, almasi, phosphates na utunzaji wa taarifa za jiolojia na madini (Management of geological and mining database).
Katika ziara hiyo, Waziri Muhongo na ujumbe wake wamepata nafasi ya kutembelea Mtambo wa kufua umeme wa kutumia gesi asilia wa HAMMA ambao unamilikiwa na serikali ya nchi hiyo kwa asilimia 100 na una uwezo wa kuzalisha megawati za umeme 418, na uwezo wa kutumia mafuta ya dizeli na gesi kwa nyakati tofauti.
Vilevile, ujumbe huo wa Tanzania umepata fursa ya kuona mashine za kuzalisha umeme zinazotembea (mobile generators) ambazo hufungwa kwa dharura sehemu inapohitajika na kuhamishiwa sehemu nyingine, ambapo mashine moja ina uwezo wa kuzalisha megawati za umeme 20.
Katika ziara hiyo, Mhe. Muhongo ameongozana na Kamishna Msaidizi wa Nishati anayeshughulikia masuala ya umeme, Mhandisi Innocent Luoga na wataalamu kutoka Wakala wa Jiolojia Tanzania (GST), TPDC na TANESCO.
Mkataba wa Makubaliano (MoU) ya ushirikiano wa Tanzania na Algeria, ulisainiwa na Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo kwa upande wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Waziri wa Nishatyii na Migodi wa Algeria, Mhe. Youcef Yome wa Algeria wakati walipokwenda kutembelea Mtambo wa kufua umeme kwa kutumia gesi asilia wa HAMMA ,Mtambo huo wenye uwezo wa kuzalisha mewagati za umeme 418 

No comments:

Post a Comment