Pages

Monday, October 13, 2014

WAZIRI MKUU AMPA MKURUGENZI MTENDAJI WA UYUI SIKU 60 KUHAMA NA TIMU YAKE


Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akifungua kituo cha polisi cha wilaya ya Uyui akiwa katika ziara ya kikazi mkoani Tabora, Oktoba 11, 2014. Kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Mhe Fatuma Mwasa na Kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Uyui, Mhe. Lucy Mayenga.(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu) 
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akizungumza na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Tabora, ACP Suzan Kaganda (kulia) baada ya kufungua kituo cha polisi cha wilaya ya Uyui akiwa katika ziara ya kikazi mkoani Tabora, Oktoba 11, 2014.(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu) 
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akizungumza na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Tabora, ACP Suzan Kaganda (kulia) baada ya kufungua kituo cha polisi cha wilaya ya Uyui akiwa katika ziara ya kikazi mkoani Tabora, Oktoba 11, 2014. Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu.

WAZIRI MKUU Mizengo Pinda amempa miezi miwili Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Uyui, mkoani Tabora, Bi Khadija Makuani kuhakikisha kuwa watumishi wote wa wilaya hiyo wanahamia Isikizya yalipo makao makuu ya wilaya hiyo.

Ametoa agizo hilo juzi jioni (Jumamosi, Oktoba 11, 2014) wakati akizungumza na mamia ya wakazi wa Isikizya waliofika kushuhudia uzinduzi wa makao makuu ya polisi ya wilaya hiyo.

“DED nimekagua nyumba ya mkuu wa Wilaya na kuzindua nyumba zile nane, miundombinu iliyopo inatosha, hamia wewe na watu wako. Ninataka ifikapo Desemba 31, mwaka huu wote muwe Isikizya. Atakayegoma, RC niletee jina lake,” amesema Waziri Mkuu.

“Shauku ya wananchi kuwasubiri mhamie hapa imetosha. Mtumishi ambaye atagoma ni ishara kuwa hataki kuwahudumia wananchi, na sisi tutasema hatukutaki. Tatizo la watumishi wengi ni kujifanya wakubwa mno kuliko wananchi mnaowahudumia,” alisema huku akishangiliwa na wakazi wa Isikizya.

Waziri Mkuu ambaye aliwasili mjini Tabora jana mchana, alitembelea makao makuu ya wilaya hiyo ili kukagua mradi wa ujenzi wa makazi ya watumishi wa wilaya hiyo. Mara baada ya kuwasili wilayani humo, Waziri Mkuu alizindua nyumba nane za watumishi zilizojengwa kwa gharama ya sh. milioni 555 ambazo kati yake, sh. milioni 400 ni ruzuku kutoka Serikalini.

Pia alikagua ujenzi wa nyumba ya Mkuu wa Wilaya ya Uyui ambayo iko katika hatua za mwisho za ujenzi. Kabla ya kuzungumza na wananchi hao, Waziri Mkuu alikagua ujenzi wa jengo la ghorofa moja la ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ambalo awamu ya kwanza ya ujenzi itagharimu sh. bilioni 1.1/- na awamu ya pili itagharimu sh. bilioni 1.4/-.

Alisema wakati wakisubiri ujenziwa ofisi yao ikamilike, watafute nafasi kwenye ofisi ya Mkuu wa Wilaya ili waweze kuwa karibu na wananchi na kuwahudumia kutatua changamoto zinazowakabili.

“Mnakaa Tabora mjini halafu mnadai mnawatumikia wnanchi wa Uyui. Haiwezekani kabisa. Hayo mafuta mnayotumia kwenda na kurudi mjini si mngetembelea wananchi wa vijijini na kuhimiza shughuli za maendeleo?” alihoji.

“Hamieni hapa muweze kutatua changamoto za wananchi. Kama mngehamia mapema hata tatizo la maji lingekwishatatuliwa na ujenzi wa nyumba za watumishi wote ungeshakamilika.”

Kuhusu changamoto ya uhaba wa maji, Waziri Mkuu aliahidi kuwatafutia sh. milioni 200/- kutoka wizara husika ili ziwezeshe kuvuta maji kutoka chanzo cha Igombe kilichopo km. 35 kutoka Isikizya.

Aliwapongeza askari ambao wameamua kuhamia katika wilaya hiyo na kuishi Isikizya licha ya mazingira magumu waliyoyakuta. Alisema atawasiliana na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP) ili waone namba ya kuwasaidia kuapata walau nyumba pacha mbili au tatu (two in one) zinazojengwa na Shirika la Nyumba la Taifa wilayani humo.

Alimtaka pia Mkuu wa Mkoa huo, Bibi Fatma Mwassa aangalie uwezekano wa kuwatumia vijana waliojiunga na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) ili kupata utaalamu wao na kuuhamishia kwa wananchi. “RC tafuteni namna ya kutumia utaalamu wa hawa vijana wa JKT ili wawafundishe wananchi mbinu za kilimo bora, ufugaji bora ama ujenzi wa nyumba bora. Siyo mnawatumia kwa kuimba tu,” alifafanua.



IMETOLEWA NA:

OFISI YA WAZIRI MKUU,

JUMAPILI, OKTOBA 12, 2014.

Chanzo: Michuzi.

No comments:

Post a Comment