POLISI
mkoani Tanga imesema imefanikiwa kupata bunduki aina ya SMG, ikiwa na
risasi 20 ndani ya mapango ya Majimoto katika eneo la Amboni, inayodaiwa
ilikuwa ikitumiwa na wahalifu waliorushiana risasi na askari mwishoni
mwa wiki.
Aidha, imesema inashikilia watu kadhaa akiwemo aliyesababisha
kupatikana kwa bunduki hiyo. Baadhi ya watu wanaendelea kuhojiwa, kupata
taarifa kwa lengo la kukamata waliopora silaha kwa askari na kurushiana
risasi kwenye mapango hayo.
Kupatikana kwa silaha hiyo, kunafuatia msako maalumu uliodumu kwa
siku nne sasa, uliolenga kusaka silaha na wahalifu wanaodaiwa kujificha
ndani ya mapango ya mawe yaliyopo Amboni, nje kidogo ya mji wa Tanga.
Kamishna wa Operesheni na Mafunzo wa Jeshi la Polisi, Paul Chagonja alitoa taarifa hiyo jana kwa waandishi wa habari mjini hapa.
Alisema mafanikio hayo, yametokana na subira ya wakazi wa Tanga na
ushirikiano mkubwa wanaoendelea kuuonesha kwa Polisi inayoshirikiana na
vikosi vingine vya ulinzi na usalama, kufanya operesheni ya pamoja
kwenye eneo hilo.
“Kutokana na taarifa kutoka kwa wananchi Februari 16 mwaka huu katika
kitongoji cha la ‘Kona Z’ kilichopo Amboni, tulifanikiwa kumkamata mtu
mmoja ambaye kwa sasa sitamtaja jina kwa sababu upelelezi unaendelea,
tulimhoji kwa kina akatupa taarifa kuhusu silaha hii,” alisema.
Alieleza, “Tulikwenda mpaka pangoni na kufanikiwa kupata SMG hii
ikiwa na magazini moja na risasi 20… silaha hii ni miongoni mwa
zilizoporwa kwa askari mwezi uliopita”.
Alisema licha ya kupatikana kwa silaha hiyo, watu kadhaa
wanashikiliwa wakihusishwa na tukio hilo. Alisema upelelezi unaendelea
kupata taarifa za kuwezesha kupatikana kwa silaha nyingine na vitu
mbalimbali vilivyowahi kuibwa.
“Naomba wakazi wa Tanga na Watanzania kwa ujumla muendelee kuvuta
subira na kutoa ushirikiano…endelezeni utulivu na mshikamano kwa jeshi
la polisi, ili kwa pamoja tuweze kumaliza tatizo hili,” alisema.
Alisema upo umuhimu mkubwa kwa wananchi, kuendeleza utulivu kwa
kutokubali kuamini taarifa potofu zenye kujenga hofu, zinazosambazwa na
baadhi ya mitandao ya kijamii kwa kuwa zinalenga kuwavuruga.
“Kimsingi jeshi la polisi pamoja na vyombo vingine vya usalama,
linaamini na kuthamini kazi ya vyombo vya habari hasa vile makini,
ambavyo vimeendelea kuwaarifu wananchi habari sahihi ambazo hazina
ghilba wala kuwachanganya”, alisema.
Alikanusha taarifa zilizoenea mjini kwamba ipo miili ya
wahalifu,iliyokutwa ndani ya mapango hayo, kutokana na mapigano
yaliyofanyika mwishoni mwa wiki.
“Ndugu zangu mwanzoni tulikuwa tukisikia harufu kali ya kama miili
iliyooza, kweli tulijitahidi kutafuta na tukafanikiwa kuona mizoga ya
ngedere na siyo binadamu ...wanyama hao walikuwa watatu na walikuwa na
majeraha makubwa sana. Kwa hiyo hawakuwa watu, bali ni ngedere ndio
walikokuwa wamekufa na kuoza humo pangoni,” alisema.
Akizungumzia mkakati wa kupata silaha iliyosalia na vifaa vingine
vilivyoporwa, Chagonja alisema jeshi lake na kikosi cha operesheni
hakitalala usingizi mpaka vitu vyote vipatikane.
No comments:
Post a Comment