Bei ya samaki aina ya kayabo imepanda kutoka Sh4,000 mwaka jana hadi Sh6,000 mwaka huu, kutokana na upatikanaji wake kwenye Ziwa Victoria kupungua na hivyo kuwa adimu kwenye Soko la Mwaloni, Kirumba.
Hali hiyo imesababisha wateja kupungua kwenye soko hilo licha ya walaji na masoko kuongezeka.
Mfanyabiashara wa samaki, Siraji Mbaze aliliambia
gazeti hili kuwa bei haijapanda kutokana na mahitaji kuongezeka, bali
kuadimika kwa samaki.
“Samaki wamekuwa adimu ndiyo maana wamepanda
bei.Hata sisi tunapenda bei ishuke ili wateja wawe wengi kwani
Watanzania hawana uwezo wa kununua samaki,” alisema Mbaze.
Mikoa ya Mtwara, Dar es Salaam na Tanga ndiyo
wateja wakubwa wa samaki hao. Wateja wengine wakubwa ni kutoka Jamhuri
ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
Kulingana na takwimu za Benki Kuu ya Tanzania
(BoT) zilizotolewa na mchumi mkuu wa benki hiyo, Mussa Mziya katika
kikao cha maendeleo ya Mkoa wa Mwanza hivi karibuni, samaki wameendelea
kupungua Ziwa Victoria. Mwaka 2012/13 walivuna tani 44,423 na 2013/14
walivuna tani 42,827.4.
Imedaiwa pia kuwa hali ya uzalishaji kwenye
viwanda vya samaki ilishuka kwa asilimia 11.1 Juni mwaka jana, huku
minofu ya samaki inayosafirishwa nje ikipungua hadi tani 21,337.2 kutoka
tani 22,513.4 sawa na asilimia 14.1.
Kupungua kwa samaki pia kunahusishwa na uvuvi haramu, unaosababisha kuua mazalia, pamoja na mabadiliko ya tabia nchi.
No comments:
Post a Comment