Wednesday, April 23, 2014
CHADEMA WAMPONGEZA RAIS KIKWETE KWA MAENDELEO WILAYANI KARATU
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete kwa kuchangia kwa kiasi kikubwa maendeleo ya Wilaya ya Karatu katika Mkoa wa Arusha.
Aidha, chama hicho kimempongeza Rais Kikwete kwa kusambaza maendeleo kwa Watanzania wote bila kujali msimamo wao wa kisiasa na hata katika maeneo yanayounga mkono upinzani.
Shukurani na pongezi hizo zimetolewa mchana wa leo, Jumanne, Aprili 22, 2014 na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Karatu, Mheshimiwa Lazaro Titus Massey wakati wa sherehe za uzinduzi wa jengo la Halmashauri hiyo mjini Karatu. Halmashauri ya Wilaya ya Karatu inaongozwa na CHADEMA.
“Ni lazima tutoe shukurani nyingi kwako Mheshimiwa Rais kwa sababu bila wewe kuwa Rais wa Tanzania sisi Karatu tusingepata jengo hili. Pamoja na kwamba Halmashauri yetu ni CHADEMA bado umeamua kuchangia sana maendeleo ya Wilaya yetu kwa kuchangia kiasi kikubwa ujenzi wa jengo hili. Sisi hata robo ya fedha za ujenzi huu hatukuweza kuzitoa,” amesema Mheshimiwa Massey huko akishangiliwa na wananchi.
Jengo la Halmashauri ya Wilaya ya Karatu limegharimu kiasi cha shilingi bilioni 1.412 na kati ya hizo, Serikali imetoa shilingi bilioni 1.394 na Halmashauri imechangia shilingi milioni 18 tu.
Akizungumza baada ya kumsikiliza Mheshimiwa Massey, Rais Kikwete amesema kuwa ni sera ya Serikali yake kusambaza maendeleo kwa Watanzania wote bila kujali misimamo yao ya kisiasa wala kuongozwa na hisia nyingine mbali na ukweli kuwa kila Mtanzania anataka na anayo haki ya kupata maendeleo.
“Sisi hatuna wasiwasi, wananchi wa Karatu wamechagua CHADEMA lakini chama hiki hakina Serikali. Wananchi wamechagua chama bila Serikali. Halmashauri mnayo lakini Serikali tunayo sisi. Katika kusambaza maendeleo, sisi hatuwezi kubagua. Hiyo ndiyo demokrasia na Serikali yetu inaheshimu sana demokrasia na misingi ya utawala bora,” amesema Rais Kikwete.
Wakizungumza baadaye kwenye mkutano wa hadhara wabunge wote wawili wa CHADEMA, waheshimiwa Cecilia Paleso na Israel Nanse wamerudia tena kumpogeza Rais Kikwete kwa kusambaza maendeleo katika maeneo yote ya Tanzania yakiwemo yaliyoko chini ya wapinzani.
“Chini ya uongozi wako, maendeleo yamesambazwa na sisi Karatu tumenufaika sana. Ni matumaini yetu kuwa chini yako, tutaendelea kunufaika na sera zako sahihi,”amesema Mheshimiwa Paleso.
Naye Mheshimiwa Nanse amesema: “Mheshimiwa Rais sisi kwetu hapa hatuna ugomvi kati ya vyama vya siasa. Siye CHADEMA tunajua kuwa CCM ni chama tawala Tanzania na CHADEMA ni chama kiongozi hapa kwetu Karatu. Ni uhusiano huu uliowezesha Karatu kuendelea kupata maendeleo.”
“Tunakushukuru na kukupongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kuifungua nchi yetu kwa barabara kila mahali. Aidha, sisi wana-Karatu tunakushukuru sana kwa mradi wa maji ambao umeuzindua leo”. Tunakushukuru sana.
Rais Kikwete alikuwa katika ziara ya siku moja wilayani Karatu, Mkoa wa Arusha na kesho atafanya ziara ya Wilaya ya Mwanga katika Mkoa wa Kilimanjaro.
Imetolewa na;
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu- Dar es Salaam.
22 Aprili,2014
Labels:
Kitaifa
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment