Pages

Thursday, April 17, 2014

MVUA NYINGINE KUBWA INAKUJA - MAMLAKA YA HALI YA HEWA


Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), imetoa tahadhari ya mvua kubwa kunyesha tena kuanzia leo na kesho katika ukanda wa Pwani.
Katika taarifa yake kwa umma jana jioni, TMA imesema maeneo ambayo yataathiriwa na mvua hizo za kuanzia leo ni Visiwa vya Unguja na Pemba pamoja na mikoa ya Tanga, Pwani na Dar es Salaam.

Huo ni mwendelezo wa mvua zilizosababisha maafa makubwa ambazo zilianza kunyesha Aprili 10, mwaka huu katika ukanda huo wa pwani. Maeneo yaliyokuwa yameathiriwa zaidi ni Dar es Salaam na Morogoro ambako zaidi ya watu 25 walifariki dunia.

Mbali ya vifo hivyo, mvua hizo zilisababisha uharibifu mkubwa wa miundombinu ya barabara hasa madaraja.

Mawasiliano ya barabara kati ya Mkoa wa Dar es Salaam na mingine nchini yalikatika kwa siku mbili baada ya barabara zake zote zinazouunganisha na maeneo hayo ama kuharibiwa vibaya na mafuriko au kujaa maji na kushindwa kupitika.

Taarifa hiyo ya TMA imesema mvua hizo zinatarajiwa kuwa kubwa kwani zitazidi milimita 50 katika saa 24.

“Wakazi wa maeneo hatari, watumiaji wa bahari pamoja na mamlaka zinazohusika na maafa, wanashauriwa kuchukua tahadhari stahiki,” ilisema taarifa hiyo.

No comments:

Post a Comment