Pages

Tuesday, April 8, 2014

UN YAKANA KUWA NA HATI YA MUUNGANO WA TANGANYIKA NA ZANZIBAR

WAKATI serikali ikidai kuwa hati halali za Muungano zipo Umoja wa Mataifa (UN), umoja huo umeikana kwa kuweka wazi kuwa hakuna ushahidi wa jambo hilo.
Taarifa zilizoifikia Tanzania Daima Jumapili kutoka kwa Ofisa wa Masuala ya Sheria na Mikataba wa UN, Andrei Kolomoets, zilibainisha kuwa hakuna ushahidi wa sekretarieti ya umoja huo kuzisajili hati hizo.
Kolomoets alibainisha kuwa kama hati hizo zingekuwa zimesajiliwa na Umoja wa Mataifa kungekuwa na kumbukumbu zake.
Sakata la hati za Muungano liliibuka bungeni wiki iliyopita ambapo wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba walionyeshwa hati ya sheria ya kuridhia mkataba wa Muungano zilizokuwa na saini walizodai zimeghushiwa. Saini za Rais wa Kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hayati Julius Nyerere na aliyekuwa Katibu wa Bunge, Pius Msekwa, zilionekana zina utofauti mkubwa, jambo lililozusha mtafaruku miongoni mwa wajumbe. Baadhi ya wajumbe walizipinga sheria hizo za hati za Muungano wakidai saini za Nyerere na Msekwa zimeghushiwa, kwa sababu zinatofautiana zikionekana kufanyiwa utaalamu wa kompyuta.

bunge1

Mathalani katika hati ya Tanganyika No. 22 ya 1964, herufi mbili za jina la Julius (us) zinatofautiana na herufi nne za mwanzo (Juli) wakati kwenye hati ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania No. 18 ya 1965 herufi zote zimeandikwa kwa ufanano.
Utata mwingine upo kwenye herufi ‘K’ ya jina la katikati la Kambarage, ambapo hati ya mwaka 1964 herufi hiyo inatofautiana na ile ya mwaka 1965.
Hata saini ya aliyekuwa Katibu wa Bunge la Jamhuri wakati huo, Pius Msekwa, zinatofautiana kwenye hati hizo, hivyo wajumbe kadhaa kutaka iletwe halisi (original) badala ya nyaraka za sheria zilizoidhinisha Muungano. Nyaraka hizo za sheria za kuridhia hati za Muungano zimepingwa na wajumbe wengi wa Bunge wakidai zina shaka kutokana na kuridhiwa na upande mmoja wa Bunge la Tanganyika bila Baraza la Mapinduzi kuridhia.
Mkorogano huo ulizidi baada ya Mwenyekiti wa kamati namba mbili inayoongozwa na Shamsi Vuai Nahodha, kudai kuwa aliambiwa na Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar kuwa hati halali za Muungano zipo Umoja wa Mataifa.
Hata hivyo Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar aliiambia kamati namba mbili kuwa hajawahi kuiona hati ya kisheria ya Zanzibar kuridhia mkataba wa Muungano, ila kwa nafasi yake anaamini ipo.
Nahodha alisema mwanasheria huyo hakuwahi kuitafuta kwakuwa hakukuwa na matatizo ya kimuungano yenye kuhitaji azionyeshe hati hizo.
Vuai alisema hati hizo zilipelekwa Umoja wa Mataifa, kwakuwa kabla ya Muungano uliofanyika Aprili 26, 1964 Tanganyika na Zanzibar kila mmoja alikuwa na kiti cha uwakilishi katika umoja huo.
Alisema kutokana na Muungano huo kulilazimika Tanzania kuwa na kiti kimoja, hivyo hati hizo zilipelekwa Umoja wa Mataifa kuthibitisha Muungano huo.
Maelezo hayo yanaonekana kukinzana na yaliyotolewa na Katibu wa Bunge Maalumu, Yahya Hamis Hamad, aliyesema kuwa hati halali ya Muungano ipo na wanaangalia uwezekano wa kutoa nakala (kopi).
Alisema kopi hiyo itapelekwa mahakamani kwa ajili ya kuidhinishwa kisheria ili ipelekwe kwa wajumbe wa Bunge Maalumu. Hamad hata hivyo alisema jambo hilo ni lazima walifanye kwa umakini mkubwa, kwakuwa hati hiyo inaweza kupotea.
Msekwa aitwa
Katibu wa zamani Bunge la Jamhuri ya Muungano aliyekuwa mmoja wa watu waliosaini nyaraka za sheria ya kuridhia hati hizo, Pius Msekwa, wiki iliyopita aliitwa kwenye kamati kutoa ufafanuzi ambao hata hivyo ulipingwa na baadhi ya wajumbe.
Pia saini za Msekwa na Rais wa Kwanza wa Tanganyika, Julius Nyerere, kwenye nyaraka hizo zinatofautiana kati ya mwaka 1964 na 1965, hatua iliyowafanya wajumbe kuomba ziletwe hati halisi za Muungano.
Katika ufafanuzi wake kwa wajumbe wa Bunge Maalumu, Msekwa alisema hati ile inasema kutakuwa na serikali ya Tanganyika na Zanzibar pamoja na Bunge la Jamhuri na Baraza la Mapinduzi, hivyo ni serikali mbili. Kuhusu nyaraka za kisheria za Baraza la Mapinduzi kuridhia hati ya Muungano, Msekwa alisema hajawahi kuziona, bali aliona picha za kikao cha kuridhia suala hilo.
Pia Msekwa alikiri kuwa saini yake na ile ya Nyerere kwenye nyaraka za mwaka 1964 na 1965 ni sahihi, na kwamba hazijaghushiwa kama inavyodaiwa.

No comments:

Post a Comment