MWILI wa mwimbaji mahiri nchini aliyefariki dunia wiki
iliyopita nchini Thailand, Amina Ngaluma ‘Japanese’ unatarajiwa kuwasili Dar es
Salaam Ijumaa wiki hii.
Kwa mujibu wa mume wa marehemu, Rashid Sumuni tayari
taratibu muhimu kuhusiana na kuuleta mwili huo nyumbani zimefanyika na wana
amini mambo yataenda kama wanavyotarajia.
“Naomba niwajulishe kuwa mwili wa mke wangu utaondoka
Thailand Alhamisi wiki hii kwa ndege ya KLM na utawasili Dar es Salaam siku
inayofuata saa tatu usiku.
“Tunaamini kama mambo yataenda kama tulivyopanga baada ya mwili
kuwasili basi Jumamosi tutamhifadhi mwenzetu. Msiba upo kwa wazazi wa marehemu Kitunda,
Machimbo, Dar es Salaam ambako ndiko maziko yatafanyika.
“Kimsingi imekuwa ngumu kusema tutazika lini, kwa sababu
bado mwili haujaletwa, lakini tayari familia kwa kushirikiana na sehemu
alikokuwa anafanya kazi na Watanzania wengine waishio kule tumeshamaliza
taratibu zote zilizokuwa zikihitajika ili kuuleta mwili nchini,” alisema Sumuni
kwa masikitiko.
Pia alivishukuru vyombo vya habari kwa kuwa karibu na
familia yao wakati wa kipindi hiki kigumu, lakini akiomba wanapotaka kutoa
habari kuhusiana na msiba huo wawasiliane na wahusika wa familia ili kupata
taarifa sahihi zaidi.
Ngaluma aliyepata kung’ara na bendi mbalimbali nchini,
alifariki dunia Alhamisi iliyopita kwa shinikizo la damu akiwa Thailand alikokuwa
akifanya shughuli za muziki katika bendi ya Jambo Survivor.
Wakati wa uhai wake alitamba na bendi mbalimbali zikiwemo
African Revolution ‘Tamtam’, Double M
Sound ‘Mshikemshike’ na TOT Plus zote za Dar es Salaam.
Pia alipigia makundi ya Arusha Sangoma, Sayari Band na Less
Mwenge yote ya Arusha na Mangelepa na Sky Sound za Kenya. Pia amepata kufanya
shughuli za muziki kwa miezi sita nchini Uganda.
Baadhi ya nyimbo alizotunga wakati wa uhai wake ni
Manyanyaso Kazini na Mapendo alizotunga akiwa Tamtam, wakati Double M Sound
alitunga nyimbo za Wajane na Ukewenza.
Pia alitoa albamu yake binafsi iitwayo Jitulize yenye nyimbo
kama Vidonge, Pete ya Uchumba, Good Night, Uombalo Hutopata, Jitulize na Mzigo
wa Moto.
No comments:
Post a Comment