MAAZIMIO YA KAMATI KUU YA CHAMA CHA DEMOKRASIA NA MAENDELEO KUHUSU MCHAKATO WA KATIBA NA KURA YA MAONI KUHUSU KATIBA INAYOPENDEKEZWA
Dar es Salaam, Oktoba 16, 2014
UTANGULIZI
Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) imekutana katika kikao chake cha kawaida na kujadili, pamoja na mambo mengine, mchakato wa Katiba Mpya. Kamati Kuu imepata taarifa ya kina juu ya mchakato ulivyoendeshwa katika hatua mbali mbali wakati wa kutungwa kwa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba na marekebisho yake na, baadaye, Sheria ya Kura ya Maoni.
Aidha, Kamati Kuu imepata taarifa ya mchakato ulivyokuwa katika hatua ya kuundwa kwa Tume ya Mabadiliko, kukusanya maoni ya wananchi na kuandaliwa kwa Rasimu ya Kwanza na ya Pili ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Vile vile, Kamati Kuu imepata na kujadili taarifa ya kina juu ya mchakato wa Katiba katika hatua ya uteuzi wa Bunge Maalum na baadaye ndani ya Bunge hilo. Mwisho Kamati Kuu imepata uchambuzi wa kina wa Katiba Inayopendekezwa iliyopitishwa na Bunge Maalum tarehe 2 Oktoba, 2014.
Uchambuzi huo utatolewa kwa vyombo vyote vya habari na kwa wananchi wa Tanzania kama taarifa hapo baadae.
Baada ya mjadala mrefu na wa kina, Kamati Kuu imeridhika kwamba mchakato wa Katiba katika hatua zake zote ulitawaliwa na nia mbaya iliyokuwa na lengo kuu la kuhakikisha kwamba hakuna mabadiliko yoyote ya maana yatakayofanyika kwenye mfumo wa kikatiba na kiutawala ambao umekuwepo katika nchi yetu kwa zaidi ya miaka hamsini.
Mchakato wa kutunga Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ulitawaliwa na ubabe na usiri uliohakikisha kwamba mchakato wa Katiba unadhibitiwa na Serikali na Chama cha Mapinduzi;
Uteuzi wa wajumbe wa Bunge Maalum kutoka ‘Kundi la 201’ ulifanywa na Rais Jakaya Kikwete kwa lengo la kuhakikisha wajumbe wengi zaidi wa Kundi hilo wanatoka CCM na washirika wake. Kwa sababu hiyo, zaidi ya asilimia 82 ya wajumbe wa Bunge Maalum kutoka Kundi la 201 walikuwa wanachama wa CCM waliochomekwa katika makundi na taasisi mbali mbali;
Sambamba na idadi hiyo ya wajumbe wa Kundi la 201, asilimia 72 ya wajumbe wa Bunge Maalum waliotokana na Kundi la Wabunge na Wawakilishi wa Zanzibar walikuwa wanachama wa CCM;
Katika hatua ya mjadala ndani ya Bunge Maalum, Kamati Kuu imeridhika kwamba mjadala huo ulitawaliwa na ukiukwaji wa wazi wazi wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba na Kanuni za Kudumu za Bunge Maalum.
Bunge Maalum lilijigeuza ‘Tume’ na kuanza kukusanya upya maoni ya wananchi kuhusu Katiba Mpya, wakati kazi ilikwisha kufanywa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba;
Muda wa kuwasilisha taarifa za Kamati mbali mbali ulifupishwa kutoka dakika sitini hadi dakika ishirini na ule wa kuwasilisha maoni tofauti ulifupishwa kutoka dakika thelathini hadi dakika kumi;
Utaratibu wa kupiga kura juu ya Katiba Inayopendekezwa kwa njia ya kifungu kwa kifungu uliondolewa na badala yake kura zilipigwa kwa ujumla ya Sura za Rasimu, yaani kura zilipigwa kwa Sura kumi za mwanzo na baadae kwa Sura tisa mwisho;
Wajumbe waliokuwa nje ya Ukumbi wa Bunge, au nje ya Dodoma na hata waliokuwa nje ya nchi kwa sababu mbali mbali kama vile mahujaji na wagonjwa waliruhusiwa kupiga kura ya kupitisha Katiba Inayopendekezwa;
Kura za wajumbe waliopinga baadhi ya vifungu vya Katiba Inayopendekezwa na kukubali vifungu vingine zilihesabiwa kuwa kura za kukubali Katiba Inayopendekezwa;
Katika mazingira haya, mambo ya ajabu na yenye kuifedhehesha nchi yetu yaliyotokea ndani ya Bunge Maalum yasingeacha kutokea.
Wajumbe Waislamu waliokwenda Makkah kuhiji na ambao uongozi wa Bunge Maalum ulieleza mwanzoni kwamba wangepiga kura kwenye Ubalozi wa Tanzania nchini Saudi Arabia hawakupiga kura Ubalozini na haijulikani walipigia wapi kura zao. Aidha, sasa inajulikana kwamba Mahujaji hao – kama ni kweli walifanya hivyo – walipiga kura siku moja kabla ya siku rasmi ya upigaji kura kwenye Bunge Maalum;
Licha ya Waheshimiwa Mohamed Raza na Salim Turky – wote wa kutoka Zanzibar – kuharibu kura zao, kura hizo zilizoharibika zilihesabiwa kuwa kura halali za ‘Ndiyo’;
Kura za wajumbe waliokufa kama vile Marehemu Shida Salum zilihesabiwa kuwa kura halali za ‘Ndiyo’;
‘Kura za Maruhani’, yaani wajumbe wa UKAWA kutoka Zanzibar na za Wazanzibari wengine waliojitoa na ambao hawajulikani majina yao hadi sasa zilihesabiwa kuwa kura halali za ‘Ndiyo’;
Mheshimiwa Maulida Komu wa UKAWA ambaye alitajwa kwenye Gazeti la Serikali lililotangaza majina ya wajumbe wa Bunge Maalum kuwa anatoka Zanzibar aligeuzwa na kuhesabika kuwa anatoka Tanzania Bara, wakati Mheshimiwa Zakia Meghji wa CCM aliyetangazwa kwenye Gazeti la Serikali kuwa anatokea Tanzania Bara alihesabika kuwa anatoka Zanzibar na hivyo kupiga kura ya ‘Ndiyo’ kama Mzanzibari;
Kura za partly ‘Hapana’ na partly ‘Ndiyo’ zilizopigwa na wajumbe wanne wa kutoka Zanzibar zilihesabika kuwa ni kura za ‘Ndiyo.’
Kamati Kuu imeridhika kwamba, katika mazingira haya, theluthi mbili ya kura za Zanzibar isingeacha kupatikana. Katika mazingira haya, na kwa kipimo chochote, Kamati Kuu imeridhika kwamba upigaji kura ya kupitisha Katiba Inayopendekezwa ulikuwa batili – na matokeo ya upigaji kura huo – yaani Katiba inayopendekezwa haiwezi kuwa halali.
Na katika mazingira haya, ujasiri unaostahili kupongezwa wa Mwanasheria wa Zanzibar, Othman Masoud Othman, na wajumbe wengine nane wa Zanzibar waliopiga kura ya wazi ya ‘Hapana’ kuikataa Katiba Inayopendekezwa licha ya shinikizo kubwa, matusi na vitisho vya kila aina, usingeweza kuzuia uharamia huu wa CCM.
Kwa hali hii, Kamati Kuu inaungana na vyama vingine vya siasa vya UKAWA, taasisi kuu za kidini nchini kama vile Baraza la Maaskofu Katoliki (TEC), Baraza la Kikristo Tanzania (CCT), Baraza la Makanisa ya Kipentekoste Tanzania (CPCT), Shura ya Maimamu, Baraza Kuu la Taasisi za Kiislamu, n.k. kulaani matukio yote yaliyotokea wakati wa mchakato wa Katiba katika hatua zake zote hadi sasa. Kamati Kuu inapondeza na kuunga mkono taasisi, mashirika na vyama vya siasa pamoja na wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba waliosusia tukio la Rais Kikwete kukabidhiwa Katiba Inayopendekezwa siku ya tarehe 8 Oktoba, 2014.
Aidha, Kamati Kuu inatoa rai kwa taasisi na mashirika yasiyokuwa ya kiraia ambayo tayari yameshaonyesha msimamo wa kuiunga mkono Katiba Inayopendekezwa kujifikiria upya na kujiridhisha kama mashirika yao hayatumiki kuhalalisha mambo haramu ambayo yamefanywa na CCM na washirika wao katika mchakato huu.
Kamati Kuu imeazimia kwamba CHADEMA itaungana na vyama na taasisi zilizotajwa hapa pamoja na umma wa Watanzania wenye nia njema na taifa kuhakikisha kwamba wanashiriki katika kampeni kubwa na ya nchini ili kuhakikisha kwamba Katiba Inayopendekezwa inapigiwa kura ya ‘Hapana’ katika kura ya maoni, ambayo ni hatua ya mwisho ya mchakato wa Katiba.
Katika hili, Kamati Kuu inatoa rai kwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi kuhakikisha kwamba inatekeleza ahadi yake kwa Watanzania kwamba Daftari la Kudumu la Wapiga Kura litaboreshwa kabla ya kufanyika kwa kura ya maoni ili kuhakikisha kwamba kila Mtanzania mwenye haki ya kupiga kura anajiandikisha kwenye Daftari hilo na anapata haki ya kushiriki katika maamuzi ya jambo hili muhimu kwa taifa letu.
Kamati Kuu inawakumbusha Watanzania kujiandaa kutimiza wajibu wao wa kihistoria wa kukataa uchakachuaji wa maoni yao uliofanywa na CCM na washirika wake katika Bunge Maalum. Kukataa uchakachuaji huu kitakuwa ni kitendo cha kizalendo cha kila Mtanzania. Kunyamazia au kuunga mkono uchakachuaji huu itakuwa ni kuisaliti nchi yetu na kuendeleza utawala wa kikandamizaji na wa kifisadi ambao umekuwa janga la taifa letu kwa miaka mingi.
——————————————————-
Dr. Willibrod P. Slaa
KATIBU MKUU
No comments:
Post a Comment