Pages

Monday, November 3, 2014

TASWIRA YA VURUGU ZILIZOTOKEA JANA KWENYE MDAHARO WA KATIBA AMBAPO MZEE WARIOBA ALIPIGWA MAKOFI

MDAHALO wa kujadili Katiba inayopendekezwa ulioandaliwa na Taasisi ya Mwalimu Nyerere, jana ulivunjika baada ya kutokea vurugu ambako Mwenyekiti wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba, alipigwa vibao shingoni na watu wanaodaiwa kuwa wanachama wa CCM.

Hali hiyo ilijitokeza kwenye Hoteli ya Blue Pearl iliyopo Ubungo   Dar es Salaam, baada ya kuvunjika  mdahalo huo uliokuwa umehudhuriwa na mamia ya watu, wengi wao wakiwa  vijana.

Baada ya vurugu hizo, waandaji waliamua kuwatoa nje ya ukumbi  wasemaji wa mdahalo huo akiwamo Warioba, Mwenyekiti wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Joseph Butiku, Profesa Palamagamba Kabudi na Profesa Mwesiga Baregu.

Wengine waliokuwa wazungumze kwenye mdahalo huo ni Humphrey Polepole   na Rais wa Chama cha Wanasheria Zanzibar, Awadhi Said, ambao wote walikuwa wajumbe wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba.

Warioba, aliyewahi kushika wadhifa wa Waziri Mkuu na  Makamu wa Rais,   alipigwa vibao viwili shingoni  alipofika kwenye mlango kuu wa kutoka ukumbini ambako kulikuwa na msongamano mkubwa wa watu.  Wakati huo, Warioba na viongozi wenzake walikuwa wakitolewa nje ya ukumbi huo.

Hatua hiyo ilifanya mlinzi wake na baadhi ya watu waliokuwa wakimtoa kiongozi huyo waongeze mwendo na kumkimbiza kiongozi huyo wa taifa kwenye chumba maalumu cha wageni wa heshima (VIP lounge), kilichoko ndani ya hoteli hiyo.

Wakati Warioba akipigwa vibao, miongoni mwa  watu waliokuwa karibu nyuna yake ni Katibu wa Uhamasishaji wa UVCCM, Paul Makonda.

Kwa sababu hiyo,  baadhi ya vijana walichangia kumpiga  kada huyo wa UVCCM aliyekuwa amevalia shati jeupe, huku wakimzuia   kuingia kwenye chumba cha VIP ambako    Jaji Warioba alikuwa amepelekwa.

Kufanikiwa kwa vijana hao kumzuia Makonda kuingia kwenye chumba hicho, kulitoa fursa ya kuendelea kupigwa hadi  alipoponyoka na kukimbilia katika  ofisi moja katika  jengo hilo   na kujifungia.

Baada ya kujificha katika chumba hicho, vijana hao waliitana na kuhamasishana ili wavunje mlango huo na kumtoa Makonda.

Hata hivyo baada kufanikiwa kuvunja mlango huo, vijana hao hawakumuona Makonda hadi walinzi wa hoteli hiyo na askari kanzu walipofika hapo na kuwafukuza.

Vurugu zilivyoanza
Vurugu katika mdahalo huo zilianza muda mfupi kabla ya Jaji Warioba aliyekuwa msemaji wa kwanza, kumaliza hotuba yake.

Baada ya kumaliza kuichambua Katiba inayopendekezwa, Jaji Warioba alisema katika kuitetae katiba hiyo, baadhi ya watu wamekuwa wakimtumia Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu  Nyerere kuunga mkono hoja zao.

“Tunatumia jina la Mwalimu ili kuunga mkono hoja zetu wakati mwingine ninajiuliza hivi tunatumia Mwalimu yuleyule ama…

“Mwalimu amekufa akisema hajaona hata sehemu ya kutia koma katika Azimio la Arusha, kuna watu waliwahi kumletea Mwalimu barua wakimwambia afungue akaunti nje ya nchi ndiyo fedha zake zitakuwa salama… Mwalimu siyo tu   alikataa lakini alitangaza kila kitu hadharani.

“Leo Mwalimu angekuwapo angekubali  watu wafungue akaunti nje ya nchi, angekubali watu wapewe zawadi wakae nazo… nikasema huyo wao siyo Mwalimu, Mwalimu alikuwa ni mtu mwenye uwezo wa kufanya uamuzi mgumu hata unaomhusu yeye,” alisema Warioba.
Vijana na mabango
Baada ya maneno hayo, baadhi ya vijana takriban 20, walisimama na kunyanyua juu mabango yaliyokuwa na ujumbe mbalimbali wa kumtukana Jaji Warioba na mengine yakisifu Katiba inayopendekezwa.

Kitendo hicho kilifanya  baadhi ya watu kujaribu kuwakalisha chini huku wengine wakichana mabango hayo hali iliyozusha  vurugu.

Wakati wote huo  Jaji Warioba alikuwa amesimama akijaribu kuwasihi watu hao kukaa chini, lakini hali hiyo ilionekana kutozaa matunda.

Baada ya muda vijana hao walijitenga pembeni karibu  na jukwaa kuu huku wakiwa na mabango yao, wakiimba nyimbo mbalimbali za CCM.

Hali hiyo ilisababisha  baadhi ya watu watoke  ukumbini  huku  wengine wakiwa wanarudi kuketi kwenye viti vyao.

Wakati vurugu hizo zikiendelea, Profesa Kabudi na Butiku kwa nyakati tofauti, walionekana wakimtaka Makonda kuwatuliza vijana hao wa CCM ambao alidaiwa yeye yeye ndiye aliwaingiza katika  ukumbi huo. 
Wakati viongozi wakimtaka Makonda kufanya hayo, vijana wengine walionekana kumvuta Makonda wakitaka kumpiga hali iliyomlazima kumtumia kama kinga, Amon Mpanju, ambaye alikuwa Mjumbe wa Bunge Maalumu la Katiba akiwakilisha kundi la walemavu.

Hali  iliendelea hivyo hadi baadhi ya vijana waliokuwa wamekaa  walipohamasishana na kuwapiga wale waliokuwa na mabango, kwa kutumia  viti hali iliyofanya wakimbie na kutoka nje ya ukumbi huo.

Baada ya vijana hao kutoka nje, hali iliwageukia Makonda na Mpanju ambao baada ya kuona hali imekuwa tete, walikimbilia kwenye jukwaa kuu na kukaa karibu na Jaji Warioba.

Huku hali ikiwa bado ya taharuki, viongozi hao (Warioba na wenzake)  waliamua kutoka nje ya ukumbi na ndipo zahama ya kupigwa vibao kwa Jaji Warioba ilipojitokeza.

Vurugu zikishika kasi ndani ya Ukumbi wa Ubungo Plaza jijini Dar.
Jaji Warioba (wa pili kushoto waliokaa) akijadiliana jambo na wenzake.


No comments:

Post a Comment