Askofu wa
Kanisa la Ufufuko na Uzima, Josephat Gwajima akiwa katika Chumba cha
Wagonjwa Mahututi (ICU), hospitali ya TMJ ya jijini Dar es Salaam jana.
Wakati
hali ya kiongozi wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Askofu Josephat Gwajima,
ikiwa tete kwa siku mbili mfululizo, Jeshi la Polisi na waumini wa
Askofu huyo wanadaiwa kuvutana hospitali inayofaa kumpa matibabu.
Askofu Gwajima, alizimia ghafla juzi majira
ya saa 2: 45 usiku akiwa kwenye chumba cha mahojiano katika Kituo cha
Polisi Kati, baada ya kutuhumiwa kumkashifu na kumtukana kiongozi wa
kanisa la Katoliki Jimbo kuu la Dar es Salaam, Mwadhama kadinali Polycap
Pengo.
Hata hivyo, mara baada ya kutokea tukio
hilo, Askofu huyo alichukuliwa akiwa katika hali ya kuzirai na kuanza
kuzungushwa katika hospitali tofauti wakati waumini walitaka apelekwe
Hospitali ya TMJ Mikocheni, Jeshi la polisi lilitaka apelekwe hospitali
za Jeshi na Muhimbili.
Tukio hilo ambalo NIPASHE
ililishuhudia, lilianza majira ya saa 3:00 usiku alipopoteza fahamu hadi
majira ya saa 8:00 usiku ambapo walikubaliana apelekwe Hospitali ya TMJ
ambako anaendelea kupatiwa matibabu.
HALI ILIVYOKUWA POLISI KATI
Baada ya kuwasili kituoni hapo majira
ya saa 8:15 alasiri, alikwenda moja kwa moja katika chumba maalumu
kilichoandaliwa kwa ajili ya kuhojiwa tuhuma zinazomkabili.
Mahojiano rasmi yalianza majira ya saa 8:45 mchana.
Ilichukua muda wa saa saba ndani ya chumba hicho, na ilipofikia saa 1.05 usiku, hali ya Askofu Gwajima ilibadilika ghafla.
Baadhi ya askari na viongozi wenzake
walionekana kujaribu kutumia njia mbalimbali ikiwamo kumpeleka chooni
ili kumrudisha hali yake ya kawaida, lakini ilishindikana.
Aliporudi ndani, aliishiwa nguvu na kupoteza fahamu kitu ambacho kilizusha taharuki ndani ya ukumbi huo.
CHANZO CHA KUZIMIA
Taarifa kutoka ndani ya kikao hicho
kilieleza, hali yake ilibadilika ghafla baada ya kuanza kuhojiwa kuhusu
mali anazomiliki ikiwamo helikopta aliyoinunua hivi karibuni.
Aidha mambo mengine aliyotakiwa
kueleza ni uhusiano wake na wanasiasa mashuhuri pamoja na akaunti
anazomiliki na njia anazopata pesa.
“Mahojiano yalikwenda vizuri, lakini
ilipofikia zamu ya kumhoji mali anazomiliki na ile helikopta aliyonunua,
ghafla alibadilika na kuanza kutoka jasho kwa wingi na kuzimia,”
kilisema chanzo hicho. Akithibitisha jambo hilo, Mchungaji Yekonia
Behanaze alikiri kuwepo kwa maswali hayo, lakini alilalamikia namna
alivyokuwa akihojiwa na askari hao kwamba haukufuata hali ya kibinadamu.
“Unajua hawakuwa na misingi mizuri ya
kupata maelezo, walihojia mambo mengi sana hata yale tuliyoamini
yangekuwapo tuliona hayakuzingatiwa badala yake iliegemea umiliki wa
vitu,” alisema Mchungaji Behanaze.
ATEMBEZWA AKIWA AMEZIMIA
Baada ya kuzirai aliondolewa ndani ya chumba hicho ili kumuwahisha hospitali kwa ajili ya kupata matibabu.
Hata hivyo, kulitokea mabishano
makali kati ya polisi na viongozi wa kanisa hilo, ambapo upande wa
polisi ukitaka kumpeleka katika Hospitali za serikali, viongozi hao
waling’ang’ania kwenda Hospitali ya TMJ.
Ilipofika Saa 3:00 usiku, polisi
walimchukua na kumuingiza katika gari lenye namba T 215 aina ya Noah na
kumpeleka Hospitali ya Kilwa Road inayomilikiwa na jeshi hilo.
Hapo alitibiwa kwa muda wa saa tatu
na ilipofika saa 5:08 usiku alichukuliwa na gari la wagonjwa lenye namba
DFP 6309 na kupelekwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
Msafara wote ulikuwa chini ya ulinzi
mkali wa polisi, ambapo wakati akielekea Muhimbili, msafara huo
ulikatisha mitaa ya Kurasini, Kariakoo, Faya na kuishia Hospitali ya
Muhimbili majira ya saa 5:18, usiku. Hata hivyo, pande mbili hizo kati
ya polisi na waumini ziliendelea kushindana kuhusu hospitali inayofaa
kumtibia.
Wakiwa Hospitali ya Muhimbili,
viongozi wa kanisa hilo ndugu na jamaa wa Gwajima waliendelea
kushinikiza kuondolewa hapo ili apelekwe TMJ ambako walidai ndipo
alipokuwa daktari wake.
Hata hivyo, hoja hiyo ilipingwa na
polisi wakiwaeleza Muhimbili ndiyo Hospitali Kuu na watakubaliana nao
endapo madaktari watashauri kuondolewa kwa barua maalum.
Ilipofika majira ya saa 6:00 usiku
gari la wagonjwa kutoka Hospitali ya TMJ lenye namba T 786 BYK
liliwasili na kukaa tayari kumchukua.
Saa 7:00 usiku Askofu Gwajima
alitolewa hospitalini hapo akiwa bado amezirai na kuingizwa katika gari
hilo na kumkimbiza Hospitali ya TMJ. Katika msafara huo, magari yalipita
mitaa ya Upanga, daraja la Selander, Morocco na hatimaye hospitalini
hapo na kulazwa wodi ya wagonjwa mahututi (ICU).
HALI YAKE KWA SASA
Hata hivyo taarifa zilizopatikana kutoka Hospitali ya TMJ, zinaeleza bado hali yake si nzuri kutokana na kutorejewa na fahamu.
Kwa mujibu wa daktari anayempatia
matibabu, Dk. Photonatus Mazigo, hali ya mgonjwa wake bado ni mbaya
japokuwa kuna dalili ya kupata fahamu taratibu.
“Kwa ujumla hali ya mgonjwa siyo ya
kuridhisha, hajazinduka tunachokifanya ni kumpatia tiba ili arejee
katika hali yake ya kawaida,” alisema Dk. Mazigo.
DK. SLAA: TUMUACHIE MUNGU
Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Wilbroad
Slaa, alikwenda kumjulia hali kiongozi huyo na kusema kwa sasa
Watanzania wasitafute chanzo, badala yake wamuachie Mungu amsaidie apone
haraka.
Alisema hawezi kuzungumzia hali ya Askofu Gwajima kwa kipindi hiki kwa sababu jukumu hilo anaachiwa daktari anayemtibia.
Chanzo: NIPASHE
No comments:
Post a Comment