Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akizungumza na waandishi wa habari katika
viwanja vya Bunge, mjini Dodoma jana. Picha na Anthony Siame.
Licha ya Serikali kusisitiza kuwa uandikishaji wa wapigakura nchi nzima kwa mfumo wa BVR utakamilika Aprili 28 na Kura ya Maoni kufanyika Aprili 30, mwaka huu kama ilivyopangwa, hesabu zilizopigwa na Mwananchi zinakataa kuwianisha siku zilizosalia na idadi ya mashine za BVR zilizopo na zinazotarajiwa kuwasili. Hali hiyo imejitokeza zikiwa zimebaki siku 36 kabla ya Kura ya Maoni kufanyika, huku kukiwapo wasiwasi miongoni mwa wadau kuhusu uwezekano wa kufanikisha matukio hayo bila manung’uniko.
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda aliwaeleza waandishi wa habari jana kuwa
uandikishaji nchi nzima utaanza siku sita kuanzia leo na kusisitiza kuwa
Kura ya Maoni kuridhia au kukaa Katiba Inayopendekezwa itafanyika
Aprili 30, mwaka huu kama ilivyopangwa.
Wasiwasi wa kutofanyika kwa kura hiyo katika tarehe iliyopangwa
unatokana na uandikishaji wa wapigakura kwa BVR unaosimamiwa na Tume ya
Taifa ya Uchaguzi (NEC) ulioanza Februari 23, mwaka huu kutokamilika
hata katika mkoa mmoja wa Njombe, wenye wapigakura 392,634 kati ya
milioni 24 wanaotarajiwa kuandikishwa nchini kote.
Hesabu zinavyokataa
Kulingana na takwimu za NEC, BVR moja inaandikisha kati ya wapigakura 80
hadi 100 kwa siku endapo hakuna tatizo lolote, hivyo kwa kadirio la
chini, iwapo BVR 7,750 zilizoagizwa na NEC zitawasili nchini kwa
mafungu, zitahitajika siku 38 kuandikisha wapigakura milioni 24
wanaokusudiwa kama kazi hiyo itaanza leo.
Hata hivyo, katika uandikishaji wa majaribio na baadaye katika Mkoa wa
Njombe mashine hizo zimeripotiwa kukabiliwa na changamoto mbalimbali ama
za kukwama, weledi mdogo wa watumiaji na hali ya hewa, hivyo kufanya
idadi iliyokusudiwa kutokamilika.
Mwandishi wa Mwananchi, Kizzito Noya aliyekuwa Makambako, Njombe wakati
wa uandikishaji hivi karibuni amesema kwa wastani alishuhudia mashine
moja ya BVR ikiandikisha wapigakura 60 kwa siku, idadi hiyo
ikilinganishwa na watu 24,000,000 wanaokusudiwa kuandikishwa kwa BVR
7,750 nchi nzima, shughuli hiyo itachukua siku 52, wakati siku
zilizosalia hadi Kura ya Maoni ni 36.
Jambo jingine linalofanya hesabu hizo kukataa ni kitendo cha mashine
hizo 7,750 za BVR zilizokusudiwa, kutokuwapo zote nchini hadi sasa,
licha ya NEC kusema mara kwa mara kwamba zitawasili wakati wowote.
Jana, Mwenyekiti wa NEC, Jaji Damian Lubuva alisema hata awamu ya kwanza ya mashine 3,100 za BVR bado ziko njiani.
Iwapo mashine hizo pekee zitafika na kutumika kuandikisha wapigakura hao
milioni 24 zitahitajika siku 97 kukamilisha shughuli hiyo.
Mchakato huo ulianza kusuasua tangu wakati majaribio yaliyotumia BVR 250
katika majimbo ya Kilombero, Morogoro; Kawe, Dar es Salaam na Milele
mkoani Katavi na baadaye katika Mji wa Makambako na mkoa mzima wa
Njombe.
Hata hivyo, uchunguzi wa Mwananchi umebaini kuwa mashine hizo 250
zimekuwa hazitumiki zote kwa kuwa baadhi zinatumika kutoa mafunzo kwa
waandikishaji watakaofanya kazi hiyo nchi nzima.
Changamoto nyingine inayokwamisha shughuli hiyo ni ukata, kwa kuwa
Serikali haijatoa fedha za kutosha kufanikisha shughuli hiyo, jambo
ambalo limethibitishwa na Pinda kuwa fedha zilizotolewa hadi sasa ni
asilimia 70 ya kiwango kilichotarajiwa.
Kauli ya Lubuva
Jaji Lubuva alisema: “Tuliamua kuanza na Njombe kutokana na BVR 250
tulizonazo kutosha katika mkoa huo wenye kata 99. Tunasubiri nyingine
7,750 kuwasili wiki ya kwanza hadi ya pili ya mwezi ujao zikitokea
China.”
Alisema uandikishaji Njombe unaendelea vizuri na unatarajiwa kukamilika Aprili 12, kama ilivyopangwa.
Kuhusu uwezekano wa kura ya maoni kufanyika Aprili 30, alisema: “Kazi ya
msingi kabla ya shughuli yoyote ni kuandikisha daftari la wapigakura,
hivyo kama tarehe itafika bado hatujamaliza nitawaeleza, lakini mpaka
sasa bado tarehe ya Aprili 30 haijabadilishwa.
“Vifaa 3,100 kati ya 7,750 viko njiani na vitakapowasili tutatangaza
ratiba, tutaanza na mikoa gani na Njombe kweli wamehamasika kwani
wamejitokeza kwa wingi na sisi kama tunaona hatujamaliza licha ya ratiba
kututaka kuhama tunaongeza siku ili kuhakikisha kila mmoja
anaandikishwa sasa mimi sielewi hao wanaosema kwamba uandikishaji
unakwenda sivyo hata huko bungeni sielewi wana maanisha nini.”
Oktoba 22 mwaka jana, Rais Jakaya Kikwete alipokutana na kufanya
mazungumzo na mabalozi wa Afrika wanaoziwakilisha nchi zao katika
Jamhuri ya Watu wa China, aliwaeleza kwamba kura hiyo itafanyika Aprili
mwaka huu.
Matumaini ya Pinda
Akizungumza na waandishi wa habari katika viwanja vya Bunge jana, Pinda
alisema uandikishaji utaanza siku sita kuanzia leo na Kura ya Maoni
kuridhia au kukaa Katiba Inayopendekezwa itafanyika Aprili 30, mwaka
huu.
Alisema utoaji wa elimu kwa umma sambamba na kampeni za kuiridhia au
kuikataa Katiba hiyo, vinaweza kufanyika wakati uandikishaji ukiendelea.
Waziri Mkuu alisema Serikali imeshalipa asilimia 70 ya fedha kwa
kampuni inayosambaza mashine hizo.
“Tukianza uandikishaji nchi nzima ndiyo tutaona changamoto zaidi zipo
wapi na zinaweza kutupeleka katika uamuzi wa aina gani. Ila hilo
litakuwa jukumu la Tume (NEC), sisi kazi yetu ni kuhangaika ili BVR
zinazotakiwa ziwe zimepatikana kwa wakati,” alisema Pinda.
Akizungumzia muda wa kampeni wa siku 30 kabla ya Kura ya Maoni Pinda
alisema: “Tume ndiyo inaweza kulizungumzia suala hilo kiundani. Unajua
inatakiwa mpaka kufikia Aprili 28 mambo yote yawe yamekamilika na siku
mbili baadaye (Aprili 30) ndiyo siku ya kura. Kama wanasema mwezi mmoja
ni sawa, tunaweza kuendelea na mambo mengine huku elimu ikitolewa kwa
wananchi.”
Alipoulizwa juu ya changamoto zilizojitokeza mkoani Njombe alisema
Serikali iliamua kuanza uandikishaji mkoani humo ili kupata uzoefu
kutokana na hali ya jiografia ya mkoa huo.
“Tulichojifunza ni kwamba katika maeneo ya mijini, tukianza
uandikishaji nchi nzima ni lazima maeneo kama hayo tuyape nafasi kubwa
zaidi tofauti na vijijini,” alisema.
Alisema maeneo ya mijini lazima mashine za BVR ziwe nyingi zaidi kuliko maeneo ya vijijini kwa sababu ya idadi ya watu.
Alisema katika Mkoa wa Njombe zilipelekwa mashine za BVR 250 lakini hazikutumika zote.
“Tumetenga siku saba kwa kila kata kwa ajili ya uandikishaji nadhani
zinatosha na kila kata tutaweka mashine za BVR mbili hadi tatu,” alisema
Waziri Mkuu.
Aliongeza: “Mashine hizo zinatosha kabisa. Kwa uzoefu tulioupata pale
Njombe hatuoni tatizo hata kidogo kwamba tunaweza kushindwa kuandikisha
wananchi na kutofikia malengo tuliyoweka. Zinatosha kwa sababu leo
wanaweza kuandikishia kituo kimoja na watu wakiisha wanahamia kituo
kingine. Kata ina vijiji vinne hadi vitano na kila kijiji kina kitongoji
kati ya vinne hadi vitano, hivyo muda wa siku saba unatosha kabisa.”
Juzi, Mbunge wa Ubungo (Chadema), John Mnyika aliomba mwongozo bungeni
akiitaka Serikali itoe majibu ya kueleweka juu ya hatima ya uandikishaji
wa wananchi katika daftari la Wapigakura ulioanzia Mkoa wa Njombe na
iwapo Kura ya Maoni itafanyika Aprili 30.
Alisema kuwa muda uliobaki ni ndoto kwa Serikali kukamilisha
uandikishaji huo nchini nzima, akitoa mfano kwamba ili wananchi wa Mkoa
wa Njombe waweze kuandikishwa wote, uandikishaji unatakiwa kuongezwa
muda hadi Aprili 28 na Spika alimjibu kuwa Serikali ingetoa maelezo.
Chanzo: Mwananchi
No comments:
Post a Comment