Taifa
Stars na Malawi (Flames) zinapambana Jumanne (Mei 27 mwaka huu) katika
mchezo wa kirafiki utakaofanyika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam
kuanzia saa 11 jioni.
Mechi
hiyo itakuwa ya mwisho kwa Taifa Stars kujipima kabla ya kucheza mchezo
wa marudiano wa michuano ya Afrika na Zimbabwe (Mighty Warriors)
utakaofanyika Juni Mosi mwaka huu jijini Harare.
Stars
inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager ipo kambini Tukuyu mkoani
Mbeya chini ya Kocha wake Mart Nooij kujiandaa kwa mechi dhidi ya Malawi
na ile ya Zimbabwe.
Malawi
imewasili leo mchana (Mei 24 mwaka huu) kwa ndege ya Malawian Airlines
kwa ajili ya mchezo huo ikiwa na msafara wa watu 27, na imefikia kwenye
hoteli ya Sapphire Court iliyopo Mtaa wa Lindi jijini Dar es Salaam.
Flames
inayofundishwa na mchezaji wa zamani wa kimataifa wa Malawi, Young
Chidmozi inatarajia kufanya mazoezi leo jioni Uwanja wa Kumbukumbu ya
Karume.
Baada
ya mechi hiyo, Malawi itakwenda moja kwa moja nchini Chad kwa ajili ya
mechi ya marudiano ya michuano ya Afrika itakayochezwa Mei 30 mwaka huu
jijini Ndjamena.
FAINALI BEACH SOCCER KUCHEZWA JUMAPILI
Fainali
ya michuano ya mpira wa miguu ya ufukweni (beach soccer) kati ya timu
za Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT) na Chuo cha Elimu ya
Biashara (CBE) inachezwa kesho (Mei 25 mwaka huu) kwenye ufukwe wa
Escape One uliopo Mikocheni jijini Dar es Salaam.
Timu
hizo zimepata nafasi ya kucheza fainali baada ya kushinda mechi zao za
nusu fainali dhidi Chuo Kikuu cha Ardhi (AU) na Taasisi ya Uhasibu
Tanzania (TIA) zilizochezwa wikiendi iliyopita.
Mgeni
rasmi katika fainali hiyo itakayooneshwa moja kwa moja na kituo cha
televisheni cha Azam Tv atakuwa Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu
Tanzania (TFF), Jamal Malinzi na itaanza saa 4.15 asubuhi. Fainali hiyo
itatanguliwa na mechi ya kutafuta mshindi wa tatu kati ya AU na TIA
kuanzia saa 3 kamili asubuhi.
Michuano
hiyo ambayo ni ya kwanza kufanyika nchini ilishirikisha vyuo 13 vya Dar
es Salaam, na ilianza Aprili 20 mwaka huu katika fukwe za Escape One na
Gorilla iliyopo Kigamboni.
Vyuo
vingine vilivyoshiriki ni Chuo Kikuu cha St. Joseph Tanzania (SJUIT),
Chuo Kikuu cha Tumaini Dar es Salaam (TUDARCO), Taasisi ya Ustawi wa
Jamii (ISW) na Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere.
Vingine
ni Chuo cha Utumishi wa Umma Magogoni, Chuo cha Usimamizi wa Fedha
(IFM), Chuo cha Utawala wa Kodi (ITA), Chuo cha Taifa cha Usafirishaji
(NIT) na Chuo cha Uandishi wa Habari Dar es Salaam (DSJ).
Tanzania itashiriki katika michuano ya Afrika ya mpira wa miguu wa ufukweni itakayofanyika mwakani nchini Shelisheli.
BONIFACE WAMBURA
OFISA HABARI NA MAWASILIANO
SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA (TFF)
No comments:
Post a Comment